Whatever the universal nature assigns to any man at any time is for the good of that man at that time. – Marcus Aurelius
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii mpya kwetu.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa mafanikio kwa mwaka huu 2018.
Asubuhi ya leo tutafakari ULICHONACHO SASA, NDIYO UNACHOHITAJI KWA SASA…
Kwenye maisha yetu, tunapitia hatua mbalimbali.
Mara nyingi huwa tunaanzia chini kuliko tunavyotaka, huwa tunakutana na mambo ambayo hatukutegemea kukutana nayo.
Wengi tunapokuwa kwenye hali hizi, huwa tunafikiri zimetokea kwa bahati mbaya na siyo hali zetu. Hivyo tunakazana kuondokana nazo haraka sana, bila hata ya kuzitumia vizuri. Kinachotokea ni kushindwa kuondokana nazo na kuwa kikwazo kwetu kwa muda mrefu.
Chochote ulichonacho sasa, ndiyo unachohitaji kwa sasa.
Changamoto yoyote unayopitia sasa, ndiyo unayohitaji kwa sasa.
Vyote vimekuja siyo kwa bahati mbaya, bali kama sehemu ya safari yako ya mafanikio.
Hivyo usikatae popote ulipo, usikatae chochote unachopitia, bali jiulize kuna kipi cha kujifunza hapo.
Huwa nasema maisha ni kama darasa, kuna darasa la kwanza mpaka shahada za uzamivu. Kutoka darasa moja kwenda jingine, kuna mtihani, ambao kwenye maisha ni changamoto.
Kufaulu mtihani kwenye maisha ni kutatua changamoto, ukiitatua vizuri unasonga mbele.
Ukishindwa kuitatua itaendelea kujirudia, hivyo unakuwa umeshindwa mtihani na hivyo kurudia darasa. Kwenye maisha hakuna ukomo wa kurudia darasa, utarudia mpaka ufaulu. Utaendelea kukutana na changamoto hiyo hiyo mpaka utakapoitatua.
Hivyo, popote ulipo sasa kimaisha, chochote unachopitia sasa kwenye maisha yako, ndiyo unachohitaji kupotia ili kuweza kupiga hatua zaidi. Tumia vizuri kila unachopitia ili kuweza kupiga hatua kwenye maisha yako.
Usikatae kile unachopitia na kusema hakikustahili, bali kitumie vizuri kufika kule unakotaka kufika.
Siku hii ikawe bora sana kwetu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha