Linapokuja swala la imani na kiroho, wengi hufikiri ni kazi ya dini ambazo tunazo. Fikra hiyo inaweza kuwa sawa kwa mtazamo wetu, hasa pale ambapo tunakuwa hatujajua tunahitaji nini ili kuwa na uamsho wa kiroho.

Uamsho wa kiroho, hasa kwa zama tunazoishi sasa, ni jukumu la mtu binafsi na linahitaji mtu aweke juhudi ili kufikia. Kusali na kufanya tahajudi pekee hakutoshi kumfikisha mtu kwenye uamsho wa kiroho.

Badala yake mtu anapaswa kujijua yeye mwenyewe kwanza, kujua alipotoka na hata kujua kwa nini yupo hapa duniani. Hili ni changamoto kwa zama tunazoishi sasa, zama ambazo watu wanajulikana kwa vyeo vyao, sifa zao au mali zao. Kiasi kwamba ukimvua mtu vyeo vyote, ukamnyang’anya mali zake zote, hawezi tena kusimama yeye kama yeye.

Uamsho wa kiroho unatutaka tujue ya kwamba, sisi tumekuwepo hapa duniani kwa muda mrefu kuliko tunavyokumbuka. Kwamba sisi ni zaidi ya vyeo tulivyonavyo, sisi ni zaidi ya mali tulizonazo, na sisi kwa kujua au kutokujua, tunachangia kuijenga dunia vile ilivyo sasa.

Mwandishi na mwalimu wa kiroho Andrew Cohen kupitia kitabu chake cha EVOLUTIONARY ENLIGHTMENT anatushirikisha jinsi ambavyo tunaweza kufikia uamsho wa kiroho katika zama tunazoishi sasa.

evolutionary enlightment

Kitu kikubwa ambacho nimejifunza kwenye kitabu hichi ni kwamba, kama hutakuwa tayari kuweka hadithi nyingi ambazo tumejifunza kwenye dini mbalimbali ambazo tumekuwa nazo, ni vigumu sana kuelewa uamsho wa kiroho.

Ambacho ameeleza Andrew kwenye kitabu hichi, na ambacho nimeona kina mashiko sana ni kwamba, wazee wetu wa zamani, walikuwa wakijitahidi kuelewa mambo haya ya kiroho wakiwa na ushahidi mdogo sana. Hivyo walitumia sababu walizoweza kupata kwa kipindi hicho kama ushahidi. Lakini kwa sasa ushahidi upo na mkubwa, kwani hata sayansi ambayo mwanzo ilionekana kama inapingana na mambo ya kiroho, sasa inaonekana kukubaliana na mambo ya kiroho.

Ukuaji na uamsho wa kiroho ni kitu muhimu kwa kila mmoja wetu kufikia, kama kweli tunataka kuwa na maisha bora na yenye maana kwetu na wale wanaotuzunguka.

Bila ya kujali dini au falsafa unayoamini au kuishi, uamsho wa kiroho ni muhimu. Hivyo karibu tujifunze kupitia uchambuzi huu wa kitabu cha EVOLUTIONARY ENLIGHTMENT.

SAFARI YA KIROHO YA KUFIKA HAPA TULIPO SASA.

 1. Ulimwengu umetoka kwenye utupu, na ndani yetu kuna utupu.

Hapo mwanzo, kabla ya kuwepo kwa chochote hapa ulimwenguni, palikuwa tupu. Na utupu huu haujaondoka, bali umeendelea kuwa ndani yetu. Kujua jinsi utupu huu ulivyo ndani yetu, fanya tahajudi, kwa kuyaachanisha mawazo yako na kila kitu unachojua au kinachokuhusu. Futa kabisa mawazo yote uliyonayo kwa muda, na utajikuta kwenye hali ya utupu, lakini katika utupu huo, bado wewe upo.

Utupu huu wa mwanzo wa ulimwengu, na hata kuendelea kuwepo kwa utupu huu ndani yetu, kunaonesha kwamba, tumekuwepo hapa ulimwenguni kwa kipindi kirefu kuliko tunavyofikiri na pia tumechangia kuufanya ulimwengu kuwa kama ulivyo sasa.

 1. Sehemu mbili za uhalisia.

Uhalisia, kile ambacho tunakijua kuhusu ulimwengu na hata maisha kimegawanyika kwenye sehemu kuu mbili.

Sehemu ya kwanza ni ule uhalisia tunaoujua na kuuishi, haya ni yale ambayo tumeyazoea kila siku na hivyo siyo mageni kwetu.

Sehemu ya pili ni ule uhalisia ambao hatuujui na hivyo hatuwezi kuuishi. Hii ni sehemu kubwa ya uhalisia ambayo imebeba maisha yetu lakini hatujijui. Huu ni uhalisia ambao ili tuweze kuufikia ni lazima tuachane kwanza na ule uhalisia ambao tumezoea kuuishi kila siku.

 1. Utupu uliojaa.

Ukiangalia uhalisia wa ulimwengu, tulipoanzia na mpaka tulipo sasa, utaona hali mbili zinazokinzana. Hali hizo ni utupu wa ulimwengu, kwa namna kwamba kila kitu kinatokana na utupu. Na hali ya pili ni utele wa dunia, utele ambao unatoka ndani ya utupu. Hivyo tunaweza kusema dunia ni utupu uliojaa, kwamba sisi tunaijaza dunia, kutoka kwenye utupu kwenda kwenye utele, lakini utele tunaoleta, hauondoi ule utupu.

HAKUNA UPACHA.

 1. Dunia ya upacha haipo.

Kwenye maisha yetu ya kawaida, tumekuwa tunaiona dunia katika upacha, kuzaliwa na kufa, usiku na mchana, uzuri na ubaya, urefu na ufupi, weusi na weupe. Lakini katika ulimwengu wa kiroho, hakuna upacha, bali kuna umoja. Wewe ni mmoja na kudhibitisha hilo rudi kwenye kutahajudi kwa kina na kurudi kwenye utupu, utagundua kwamba utupu umezalisha kitu kimoja.

Hivyo wewe ni kitu kimoja na upo kwenye umoja na dunia nzima. Kila kitu hapa duniani kipo kwenye umoja na wewe. Hii ni dhana ngumu kuielewa, lakini ni dhana muhimu sana. Hata wanasayansi wanadhibitisha hili kupitia maada, kwamba kila kitu kimetengenezwa na maada ambayo ndiyo msingi mkuu wa kila kitu.

 1. Hukuzaliwa na wala hutakufa.

Kwenye upacha wa dunia, tunajua tulizaliwa na hivyo tutakufa, ni lazima, ndivyo tumekuwa tunaona kwa wengine. Lakini katika uamsho wa kiroho, unapotahajudi kwenye utupu wa dunia, unagundua kwamba, hukuzaliwa na hivyo hutakufa.

Kiroho ulikuwepo kabla ya kitu chochote kuwepo hapa duniani, na hivyo utaendelea kuwepo, kwa sababu hajawahi kuwa chochote kiroho.

Kimwili tunayaona maisha kama mstari, wa kuzaliwa, kuishi, kukutana na changamoto kisha kuzeeka na kufa. Lakini kiroho, yote hayo hayapo, ulikuwepo, upo na utaendelea kuwepo.

 1. Ufahamu wa ulimwengu ni mkubwa kuliko uelewa wetu.

Ufahamu wa ulimwengu, kwa uhalisia unaoonekana na usioonekana ni mkubwa sana, lakini uelewa wetu sisi binadamu ni mdogo. Ndiyo maana hatuwezi kuelewa wala kuona vitu vingi vinavyokuwa vinaendelea hasa kwenye ulimwengu wa kiroho.

Ukichanganya na changamoto za maisha ya kila siku, tunakuta akili na fikra zetu zimebanwa kwenye matatizo yetu binafsi na kushindwa kuona ukubwa wa ufahamu wa ulimwengu.

Tunashindwa kuishi ufahamu huu wa kiroho kwa sababu hatujui hata kama upo.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Harmonic Wealth (Siri Ya Kuvuta Maisha Unayoyataka).

TULIKUWEPO WAKATI DUNIA INAANZA.

 1. Miaka bilioni 14 iliyopita ulikuwepo kiroho.

Wanasayansi wanatuambia dunia ilianza miaka bilioni 14 iliyopita. Katika kipindi hicho kulikuwa na nguvu kubwa ambayo ilijikusanya na kuyatengeneza maisha mpaka hapa tulipofika sasa.

Kiroho, tulikuwepo wakati yote haya yanaanza. Msingi wa uamsho mpya ni kwamba, kama dunia imetoka kwenye utupu, na ndani yetu bado kuna utupu, basi sisi ni sehemu ya utupu, hivyo wakati maisha yanaanza hapa duniani, tulikuwepo.

 1. Chanzo cha maisha, kilianza na sisi.

Haijalishi nini kilianzisha maisha hapa duniani, tulikuwa sehemu ya chanzo hichi. Kama ambavyo imani za kidini zinatufundisha kwamba Mungu aliumba dunia na kisha kutuumba sisi kwa mfano wake, kiroho hili lipo sahihi kabisa. kwa sababu hakuna namna sisi tunaweza kutengwa na kilichoanzisha maisha hapa duniani. Tulikuwepo kiroho na tutaendelea kuwepo kiroho hata baada ya kila kitu kupita.

NDIYO KUBWA.

 1. Je unayachukuliaje maisha?

Kulingana na imani mbalimbali za kidini na hata falfasa, maisha yanaweza kuchukuliwa kwa njia tatu;

Njia ya kwanza ni kwamba maisha ni mateso, maisha hayana maana na hapa duniani tunapita ili kwenda kwenye yale maisha yanayotufaa. Hali hii inayafanya maisha yetu yasiwe na maana kubwa na hivyo kushindwa kuyaishi kwa ukamilifu.

Njia ya pili ni kwamba maisha yapo tu, siyo mabaya wala siyo mazuri, tupo hapa duniani na muda wetu ukiisha basi hakuna tena jipya. Mtazamo huu pia unawafanya watu kukosa sababu kubwa ya kuisha na kuzisukuma siku zao hapa duniani, kusubiri muda wao uishe na waondoke.

Njia ya tatu ni maisha ni kitu kizuri, maisha ni nafasi yetu ya kujenga dunia na kuifanya kuwa bora zaidi. Kwa mtazamo huu tunaona tuna mchango mkubwa hapa duniani, tuna jukumu kubwa la kuifanya dunia kuwa bora.

 1. Ndiyo kubwa kwa maisha mazuri.

Kwenye uamsho wa kiroho, tunapaswa kusema ndiyo kubwa kwenye maisha mazuri, badala ya kuishi maisha kama mateso na kusubiri kuondoka, tuyaishi maisha kama sehemu muhimu inayohitaji mchango wetu. Haimaanishi kila kitu kitakuwa rahisi, haimaanishi kutakuwa hakuna changamoto, lakini kiroho hivyo vinakuwa vitu vidogo sana kwako.

KUAMSHWA KWA MAGEUZI.

 1. Nguvu ya mageuzi ipo ndani yako.

Dunia imekuwa inapitia mageuzi mbalimbali mpaka kufika hapa ilipo sasa. Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba, nguvu ya mageuzi ya dunia ipo ndani yako pia. Ukitaka kudhibitisha hili, angalia nguvu ya kufanya mapenzi jinsi ilivyo kubwa. Hii ni nguvu ambayo ipo ndani ya kila mwanadamu na kila kiumbe hai, na jukumu lake kubwa ni kuhakikisha viumbe hai tunaendelea kuzaliana. Nguvu hii ni kubwa na kiumbe hai anaweza kufanya mambo ya hatari sana kuhakikisha anatimiza nguvu hii.

Kadhalika kwenye nguvu za ubunifu, mtu anapokuwa na wazo kubwa la kubadili mambo, anaweza kufanya kazi usiku na mchana, asipumzike na wala hata asile na wala hataona njaa au kupata usingizi, nguvu ile iliyoifikisha dunia hapa ilipo, ipo kwa kila mmoja wetu.

 1. Nguvu ya mageuzi kiroho.

Kama ambavyo tumeona nguvu ya mageuzi ambayo tunayo kimwili, kwenye nguvu ya kufanya mapenzi na nguvu ya ugunduzi, pia nguvu hii ipo kiroho. Nguvu hii ya kiroho ipo kwa kila mmoja wetu, na ndiyo imekuwa inatusukuma kutaka kujua zaidi kuhusu dunia na kuhusu sisi wenyewe. Kujua kwa nini tupo hapa duniani, na je dunia inaelekea wapi. Kutaka kujitofautisha na wengine, na hata kujijua sisi wenyewe, ni matokeo ya nguvu hii.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; HANDBOOK OF EPICTETUS (Mwongozo Wa Maisha Bora, Yenye Furaha Na Mafanikio Kutoka Kwenye Falsafa Ya USTOA)

KUJIUA NAFSI; NAFSI HALISI NA ISIYO HALISI.

 1. Hujijui kama unavyofikiri unajijua.

Huwa tunafikiri tunajijua vya kutosha, kwamba tunazijua nafsi zetu vya kutosha. Lakini ukweli ni kwamba tunajidanganya.

Kuna aina mbili za nafsi, ya kwanza ni nafsi isiyo halisi. Hii ni ile nafsi ambayo unafikiri unajijua kumbe hujijui. Hapa ni pale unapojitambulisha kwa vitu vya nje, elimu yako, cheo chako, mali zako na vingine unavyojihusisha navyo. Hii siyo nafsi halisi kwa sababu vitu hivyo vikiondoka, utakuwa hujijui kwa hakika.

Aina ya pili ya nafsi ni ile nafsi halisi, hii ni ile nafsi yako hasa, yaani wewe kama wewe, bila ya kujali una nini au unajihusisha na nini. Hii ndiyo nafsi muhimu kuijua na kuiishi kwa sababu ndiyo utakayodumu nacho. Vitu vya nje vinakuja na kuondoka, lakini wewe unabaki. Kuijua nafsi yako halisi ni muhimu kwa maisha yako.

 1. Kuijua nafsi yako halisi, ondokana na ubinafsi.

Changamoto inayowazuia wengi kufikia uamsho wa kiroho ni ubinafsi. Huwa tunatumia muda mwingi kujifikiria sisi wenyewe, kufikiria mambo yetu, vitu vyetu, changamoto zetu na hata mali zetu na kusahau kwamba ulimwengu wote ni sehemu yetu pia.

Tangu enzi na enzi, ukuaji wa kiroho umekuwa unahusishwa na kujiepusha na tamaa za mwili, kuwa tayari kupoteza kila kitu lakini kubaki wewe kama wewe. Viongozi wakubwa wa kiimani ambao wamekuwa nguzo za dini tulizonazo sasa, walikuwa siyo watu wenye mali nyingi, lakini waliweza kuwa na maisha yanayowagusa wengine wengi.

Ukiweza kuondoka kwenye ubinafsi, unaweza kufikia uamsho wa kiroho na kuweza kuisaidia dunia kwa nafasi kubwa.

 1. Uhuru mkubwa ulionao kiroho.

Moja ya vitu ambavyo sisi binadamu tunaweza kujivunia, ambavyo viumbe wengine hapa duniani hawajapata nafasi ya kuwa navyo, ni uhuru wa kuchagua. Kila mmoja wetu, anao uhuru wa kuchagua, hata kama siyo mkubwa, lakini upo na tunaweza kuutumia. Hata kama mtu hana kitu kabisa, hata kama mtu yupo gerezani, bado anao uhuru wa kuchagua mawazo na fikra zake aziweke wapi.

Huu ndiyo uhuru mkubwa sana ambao tunao, ambao kama tukiweza kuutumia vizuri, tunaweza kufikia uamsho wa kiroho. Kwa sababu ni kwa uhuru huu tunaweza kuondokana na ubinafsi, na pia kuweza kuungana na nguvu kubwa ya mageuzi ambayo inaendesha dunia.

 1. Changamoto kubwa inayotuzuia kutumia uhuru tulionao.

Zama tunazoishi, zinaonekana kuwa zama nguvu sana kufikia uamsho wa kiroho kutokana na kelele nyingi na uhuru wa watu kuishi vile watakavyo. Kwa watu kupeleka mawazo na fikra zao kwenye matatizo madogo madogo yanayowasumbua kila siku, inawazuia kuweza kutumia uhuru wao kufikia uamsho wa kiroho. Pamoja na uhuru mkubwa wa wapi tupeleke mawazo yetu, wengi wetu tunayaweka kwenye hofu na tamaa ambazo tunazo kwenye maisha yetu.

Hofu na tamaa ni matokeo ya ubinafsi, hivyo tukiweza kufanyia kazi ubinafsi, na tukaacha kujiangalia sisi wenyewe, tutaweza kupiga hatua kiroho.

Unachopaswa kujua ni kwamba kiroho, maisha yako si yako, bali ni maisha ya ulimwengu mzima, hivyo kukazana na changamoto ndogo ndogo unazopitia ni kuinyima dunia kile ambacho ingepeta kutoka kwako.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Katika Kwenye Kitabu Cha The Art Of Living.

NJIA NA LENGO LA KUFIKIA UAMSHO WA KIROHO.

Njia na lengo la kufikia kwenye uamsho wa kiroho ni kitu kimoja. Na hapa kuna sayansi na sanaa moja, na vitu vitano vya kufanyia kazi.

 1. Sayansi na sanaa ya utulivu.

Njia ya uhakika ya kuifikia ile nafsi halisi iliyopo ndani yetu, njia ya kuweza kurudi kwenye umoja wetu na dunia, ni kukaa kwenye utulivu, kitu ambacho tunaweza kukifanya kupitia tahajudi (meditation).

Kupitia tahajudi, unayafuta kabisa mawazo yako ambayo kwa muda mwingi yamejishikiza kwenye vitu na ubinafsi. Unaondokana na kila unachofikiri na kuyarudisha mawazo yako ndani yako. Hapa ndipo unaporudi kwenye utupu wa dunia, na kuifikia ile nafsi yako halisi, nafsi ambayo haijajishikiza na kitu chochote. Hii ndiyo nafsi ambayo inaweza kufikia uamsho wa kiroho.

Ili kuweza kuishi kwenye nafsi hii halisi, zoezi la tahajudi linahitaji kuwa la mara kwa mara. Kulifanya mara nyingi tuwezavyo, na kulifanya kila siku kunatufanya tuweze kuwa karibu na uhalisia wetu na kuondokana na nafsi isiyo halisi. Pia linatuonesha jinsi ilivyo muhimu kwetu kuishi kwa ajili ya ulimwengu na siyo kwa ajili yako binafsi.

MAMBO MATANO YA KUZINGATIA ILI KUFIKIA UMASHO WA KIROHO.

 1. MOJA; USAHII WA NIA.

Kitu cha kwanza unachohitaji ili kufikia uamsho wa kiroho ni nia sahihi na iliyo wazi ya kufikia uamsho wa kiroho. Siyo zoezi rahisi na siyo wengi wanaoliweza. Lakini unapokuwa na nia sahihi na iliyo wazi, inakuwa rahisi kwako kuchukua hatua. Na hata unapokutana na magumu na changamoto, inakuwa rahisi kuyavuka.

Mtu anapokuwa na nia ya kweli, na anapojitoa hasa, hakuna kinachoweza kumzuia.

 1. MBILI; nguvu ya hiari.

Jambo la pili kuzingatia ni kujitoa kwa hiari kwa ajili ya kufikia uamsho wa kiroho. Huhitaji kufanya hili kwa ajili ya mtu mwingine, huhitaji kufanya ili kuonekana au kwa sababu kila mtu anafanya. Bali unahitaji kufanya, kwa sababu umechagua kwa hiari yako mwenyewe kufanya.

Hili ni jukumu unalokuwa umechagua, hivyo unapokutana na magumu hulalamiki au kutafuta njia ya kukimbia, badala yake unaendelea kupambana.

 1. TATU; Kabili kila kitu na usiogope chochote.

Katika maisha ya kawaida ya mwili, tumejiwekea vikwazo na vizuizi vingi, kuna vitu tumejiambia tunaweza kufanya na vingine hatuwezi. Kuna vitu tunavikubali na vingine tunavikwepa.

Katika kufikia uamsho wa kiroho, tunahitaji kukabili kila kitu na kutokuogopa chochote. Kwa sababu kama tulivyoona, kiroho tumekuwepo kabla ya kuwepo kwa chochote, hivyo kuongopa chochote au kukwepa chochote ni kujishusha kiroho.

Unapokuwa tayari kukabili kila kitu kwenye maisha, unakuwa huna ukomo tena, bali kufikia uamsho wa kiroho.

 1. NNE; Mtazamo wa mchakato.

Hatua muhimu sana katika kufikia uamsho wa kiroho ni kuangalia kila jambo kwa mtazamo wa mchakato. Chukulia kila kitu kama kilivyo na acha kujihusisha nacho. Yaangalie maisha kama yalivyo na acha kuyaangalia kama maisha yako. Unapokiona kila kitu kama kilivyo, na kuacha kujihusisha moja kwa moja, unajipa uhuru wa kuona kwa uhalisia badala ya kuzibwa na hisia ambazo huwa tunakuwa nazo kwenye yale tunayofanya.

 1. TANO; Dhamira ya ulimwengu.

Jambo la tano muhimu la kuzingatia kwenye uamsho na mageuzi ya kiroho ni kuwa na dhamira ya ulimwengu. Unafanyia kazi uamsho siyo kwa sababu unataka kuwa mtakatifu, au unataka kupata mali au kingine chochote, ila kwa sababu wewe ni ulimwengu na ulimwengu ni wewe. Unakumbuka ile tahajudi ya kina ambayo inaonesha tumetoka kwenye utupu wa dunia, kwamba wakati dunia inaanza tulikuwepo? Hivyo basi haya lengo la uamsho wa kiroho, siyo kwa ajili yetu, bali kwa ajili ya ulimwengu wote.

Kufikia uamsho wa kiroho, kuwa na mapinduzi ya kiimani ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukifikia kama ataweka juhudi katika kujifunza na kufanyia kazi misingi hii tuliyojifunza. Na maisha ya uamsho wa kiroho ndiyo maisha yenye maana na kusudi la kuishi. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kufanyia kazi uamsho wa kiroho ili kuwa na maisha bora yenye maana kwetu na kwa wanaotuzunguka pia.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji