Asili ya akili na mawazo yetu ni utulivu na uamsho, lakini pale tunapong’ang’ana na hisia mbalimbali ndipo tunapoteza ule utulivu na uamsho wa akili zetu. Tunachokipata ni msongo wa mawazo, uchovu na mateso.

Akili zetu zina nguvu kubwa ya kuponya maumivu na msongo wa mawazo, kuwa na utulivu wa akili na kuwa na furaha wakati wote kama tutaacha kujishikiza na vitu ambavyo ni vya nje kwetu.

Tulku Thondup kwenye kitabu chake cha THE HEALING POWER OF MIND anatushirikisha jinsi tunavyoweza kutumia nguvu ya akili zetu kutuliza akili, kuondoa changamoto za mwili na kuwa na furaha wakati wote.

healing power

Kitabu hichi kimeandikwa kwa msingi wa falsafa ya Ubuddha na zoezi la tahajudi ambalo ni zoezi ambalo kila mtu anaweza kufanya, awe ni Mbuddha au hata asiye Mbuddha.

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu, tujifunze jinsi ya kutuliza akili zetu na kuponya miili yetu kwa kutumia nguvu ya akili.

 1. Akili zetu ndizo zinatengeneza hali ya furaha na mateso, vyote hivi ni hali ya akili na hivyo uwezo wa kuwa na utulivu na amani upo ndani yetu. Yeyote anayejua kwamba akili ina nguvu ya utulivu na uamsho, tayari yupo kwenye njia ya kuelekea kwenye hekima na uamsho.
 2. Nafsi ni udanganyifu, ni kitu ambacho siyo asili, kitu ambacho hakipo kwa uhalisia. Kujitengenezea nafsi ndiyo chanzo kikuu cha mateso kwenye maisha. Unapoanza kusema hichi ni changu unajiandaa kuumia pale unapokikosa. Kila kitu hapa duniani kinategemeana na vitu vingine, hakuna hata kitu kimoja ambacho kinamilikiwa na mtu mmoja.
 3. Wewe ni mmoja na dunia, watu wote duniani ni kitu kimoja na tuna umoja na asili ya dunia. Katika hali hiyo ya umoja, kila kitu ni tulivu na kwenye hali ya uamsho. Ni pale watu wanapojitenga na umoja wao ndipo wanapotengeneza matatizo na mateso kwenye maisha yao.
 4. Uamsho ni umoja, katika uamsho hakuna raha wala shida, hakuna kizuri wala kibaya, hakuna kuumwa wala kupona. Kama ukiweza kufikia hatua hii ya kuona kila kitu kama kilivyo, badala ya kukiweka kwenye makundi ya upacha, unakuwa umefikia uamsho na unaweza kutumia nguvu ya akili yako kufanya akili na mwili wako kuwa imara hata kama unapitia magumu kiasi gani, kwa sababu kwenye uamsho, hakuna ugumu.
 5. Ishi ndani ya siku moja. Tunapenda kuweka malengo makubwa ya siku zijazo, na kuyaangalia malengo hayo wakati wote. Hatari ya malengo ya aina hiyo ni kutufanya tuangalie sana siku zijazo na kushindwa kuishi kwenye wakati tulionao. Haijalishi unapanga makubwa kiasi gani, unapaswa kuishi ndani ya siku moja. Kwenye kila muda wa siku unaoupata, ishi muda huo. Kila unachokifanya, weka akili na nguvu zako zote hapo, weka maisha yako hapo na utaweza kuituliza akili yako na ikakupa matokeo bora sana.
 6. Kutangatanga kwa akili ndiyo chanzo cha msongo wa mawazo, uchovu na hata mateso kwenye maisha. Kama huwezi kuituliza akili yako sehemu moja, kwenye kile unachofanya, na ukaicha izurure kadiri iwezavyo, utaishia kuwa na msongo wa mawazo, uchovu na hata mateso. Kazi yako ya kwanza ni kuhakikisha akili yako inatulia pale ulipo, kwa kile unachofanya, weka akili yako yote hapo.
 7. Kwenye falsafa ya Ubuddha, kutambua magonjwa au mateso na kuyatatua kunategemea misingi mikuu minne;

Msingi wa kwanza ni kutambua ukweli kwamba tunateseka.

Msingi wa pili ni kutambua ukweli kwa nini tunateseka

Msingi wa tatu ni kutambua ukweli kwamba tunaweza kumaliza mateso yetu.

Msingi wa nne ni kutambua ukweli kuhusu njia inayotupeleka kwenye uhuru.

Kwa kutumia misingi hii minne, tunaweza kuondokana na matatizo yoyote ambayo tunajikuta nayo kwenye maisha yetu.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Evolutionary Enlightment (Njia Mpya Ya Uamsho Wa Kiroho).

 1. Furaha ya kweli na ya kudumu haitokani na vitu vya nje ambavyo unaweza kuvimiliki, au hali fulani za nje unazoweza kutengeneza, bali ni zao la akili iliyotulia na iliyo imara. Hivyo kama unakazana kutafuta vitu au watu ili wakupe furaha, unapoteza muda wako bure. Furaha ya kweli inaanzia ndani ya akili yako, kama ukiweza kuituliza na kutumia vizuri nguvu zilizopo ndani ya akili yako.
 2. Kuachilia ni njia rahisi ya kufikia utulivu wa akili yako. Kinachofanya watu wanakuwa na msongo wa mawazo, wanakuwa na hofu ni kushikilia vitu ambavyo havina umuhimu wowote. Kama utaweza kuachilia vitu ambavyo umeshikilia, utaipa akili yako uhuru na hilo litakupa furaha ya kweli na ya kudumu.
 3. Hakuna hali inayodumu kwenye maisha, ila kitu kinabadilika. Watu wamekuwa wanajitesa kwa hali fulani wanazopitia kwenye maisha yao, hasa zile wanazoona ni hali mbaya au hali ngumu. Lakini ukweli ni kwamba hakuna hali inayodumu kwenye maisha yetu, kila kitu kinapita. Hivyo chochote kinachokusumbua leo, jua kwamba kitapita, hakitadumu milele hivyo usikubali kiwe chanzo cha mateso na kukosa furaha.
 4. Jua vile vitu muhimu kwa maisha yako kwenda, kisha usikubali vingine vikusumbue, kwa sababu siyo muhimu kwako. Kila mtu ana vitu ambavyo ni muhimu kabisa kwenye maisha yake, chakula, mavazi, malazi, afya na elimu ni vitu ambavyo ni muhimu kwa kila mtu. Na kila mtu ana kiasi katika vitu hivyo ambacho kinafanya maisha yake kwenda vizuri. Kinachotusumbua kwenye maisha, ni pale tunapojilinganisha na wengine na kuona kwa sababu wengine wana zaidi, basi na sisi tunapaswa kuwa na zaidi. Tunakazana kupata zaidi, siyo kwa sababu tunahitaji, ila kwa sababu wengine wana zaidi. Haya ni mateso ya kujitakia kwenye maisha.
 5. Pamoja na watu kukazana na kuwa na mali nyingi kwenye maisha yao, huwa hawapati utulivu wa nafsi na kuridhika na maisha yao, kwa sababu wanatumia muda mwingi kuangalia nje wana nini badala ya kuangalia ndani yao wana nini na kuimarisha kile kilichopo ndani. Watu wanaishi kwa mtiririko huu, kwanza kuwa na VITU, kisha kuangalia MWILI na mwisho kuangalia AKILI. Mtiririko sahihi ni kuanza na AKILI, kisha MWILI halafu VITU vitakuja vyenyewe kama akili na mwili viko vizuri.
 6. Usiishi kama nyuki, ambaye anatumia maisha yake yote kutengeneza asali halafu hali yeye asali hiyo, ila inaliwa na wengine. Watu wamekuwa wanatoa maisha yao yote kutafuta mali, ambazo hawapati hata muda wa kuzitumia na kuzifurahia, katika harakati hizo wanakufa na kuwaacha wengine wakitumia hovyo mali ambazo wamekazana kutafuta. Tafuta mali, lakini pia hakikisha unayaishi maisha yako, kwa ukamilifu.

SOMA; MINDFULNESS; Jinsi Kuzurura Kwa Akili Zetu Kunavyotugharimu Kwenye Maisha Na Jinsi Ya Kuzituliza Akili Zetu.

ZOEZI LA KUFANYA TAHAJUDI.

 1. Tahajudi ni zoezi kuu la kiroho lililoanzia kwenye falsafa ua Ubuddha na sasa linatumika na kila mtu katika kutuliza akili na mtu kuweza kujijua yeye mwenyewe. Tahajudi ni kitu ambacho kila mtu anaweza kufanya, iwe ana dini au hana, kwa sababu ni zoezi linalohitaji mtu kuchukua hatua ya kudhibiti akili na mawazo yake na kuishi maisha yenye maana kwake.
 2. Hatua ya kwanza muhimu kwenye Tahajudi ni kujitoa, kutenga muda wa kuweza kufanya zoezi hili na kuhakikisha unafanya kweli, usikubali kitu chochote kikuzuie kufanya. Ni rahisi sana kuona huna muda wa kufanya tahajudi au kuahirisha kufanya, lakini pale unapoweka tahajudi kama zoezi muhimu la kiroho kwenye maisha yako, na kuhakikisha unafanya kweli kila siku, itakusaidia sana.
 3. Kitu kingine muhimu kwenye tahajudi ni kuchagua eneo ambalo ni tulivu na halina usumbufu. Siyo lazima uende mbali kupata eneo hilo, unaweza kuchagua chumba ndani ya nyumba na ukakitumia kufanya tahajudi, na hata ndani ya chumba kimoja, unaweza kuchagua kona ambayo utaitumia kufanya tahajudi. Na kama kila eneo lina usumbufu, unaweza kuchagua muda ambao hakuna usumbufu sana, labda asubuhi na mapema ambapo wengine bado wamelala. Eneo lenye utulivu ni muhimu hasa unapoanza kufanya tahajudi, kwa sababu inapunguza kazi ya akili kupambana na usumbufu.
 4. Mkao mzuri wa kufanya tahajudi ni kukaa wima na mgongo kuwa umenyooka. Ni vizuri mgongo usiegemee popote na miguu yako kuwa imekunjwa. Katika mkao wako, hakikisha misuli yako imekaa vizuri na hakuna eneo lililokaza au lenye maumivu. Unapoanza tahajudi, akili yako haipaswi kuwa inafikiria maumivu fulani kwenye eneo la mwili kwa sababu ya mkao uliochagua.
 5. Msingi mkuu wa zoezi la tahajudi ni kupeleka akili na mawazo yako kwenye kitu kimoja na kuepuka kuruhusu akili izurure. Pia kitu hicho ambacho unapeleka mawazo yako, kinahitaji kuwa kitu tulivu. Hivyo sehemu nzuri ya kuanzia ni kupeleka mawazo yako kwenye pumzi zako. Ukiwa umekaa eneo tulivu la kufanyia tahajudi, weka akili na mawazo yako kwenye pumzi zako, hesabu jinsi unavyopumua ndani na kupumua nje. Mawazo yako yote yawe kwenye pumzi zako, usikubali kufikiria kitu kingine nje ya pumzi zako.
 6. Kutumia taswira. Njia nyingine ya kutuliza mawazo yako wakati wa tahajudi ni kutumia taswira. Kuwa na kitu ambacho unakiangalia, iwe ni kwenye akili yako au mbele yako. Kitu hicho kinaweza kuwa picha au hata mwanga. Muhimu ni mawazo yako yote yawe kwenye kitu hicho kimoja na usiruhusu yahame kwenda kwenye kitu kingine.
 7. Mawazo yako yatajaribu kuondoka pale ulipoyaelekeza, iwe ni kwenye kupumua au kwenye taswira, hilo likitokea haimaanishi kwamba umeshindwa kwenye kufanya tahajudi, hiyo ni hali ya kawaida, hasa unapoanza. Unachofanya ni kurudisha akili na mawazo yako kwenye kile kitu ulichochagua. Hata baada ya kurudisha mawazo yako, bado yataendelea kukutoroka, kikubwa ni kuendelea kurudisha mawazo yako kwenye kile ulichochagua.
 8. Kadiri unavyotuliza mawazo yako, na kuyazuia yasizurure, unaimarisha nguvu za akili yako katika kuponya mwili wako. Maradhi mengi tunayopata ni matokeo ya msongo wa mawazo au kutokuwa makini na afya zetu. Tunapofanya tahajudi, tunatuliza akili zetu na hivyo kuwa makini zaidi na maisha yetu kwa kila hatua tunayochukua. Wakati mwingine fikra hasi tunazokuwa nazo ndiyo zinafanya maisha yawe magumu, kwa kufanya tahajudi unaondokana na fikra hasi na kuona kila kwa jinsi kilivyo na kama sehemu ya maisha.

Jifunze kufanya tahajudi na kila siku tenga muda wa kufanya tahajudi, tafiti za kisayansi na kiafya zinaonesha tahajudi ina manufaa mengi sana kiafya. Ni zoezi ambalo halihitaji uwe mtu wa aina gani, uwe na nini au hata uwe na elimu gani, unachochagua ni kutuliza mawazo yako na unavuna faida hizo nzuri za tahajudi.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji