Rafiki yangu mpendwa,

Maisha yetu yanaandamwa na changamoto nyingi. Kuanzia changamoto za ndani yetu, changamoto za wengine na hata changamoto za mazingira.

Watu wengi wanapenda kuwa na maisha bora, maisha yenye utulivu, furaha na mafanikio makubwa. Lakini ni wachache sana wanaofikia hilo. Wengi wamekuwa wanasumbuka na maisha, wakirudia makosa yale yale ambayo yamekuwa yanaleta changamoto kwenye maisha yao.

Kinachopelekea wengi kushindwa kuwa na maisha bora ni kukosa msingi wa kuendesha maisha yao. Wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kwa mazoea, kwa kufanya kile ambacho wamezoea kufanya au wengine wanafanya. Wasijiulize kama ni kitu sahihi kwao kufanya.

Moja ya njia za kumpa mtu msingi wa kuendesha maisha yake ni kupitia falsafa. Falsafa inamfundisha mtu kipi sahihi kufanya na kipi anapaswa kuepuka kwenye maisha yake. Kwa kufuata misingi hii ya falsafa, kila mtu anaweza kuwa na maisha bora.

Zipo falsafa nyingi sana ambazo watu wamekuwa wanazifuata. Na falsafa hizi zimekuwepo kwa miaka mingi, nyingi zina miaka zaidi ya elfu mbili. Na licha ya kwamba misingi hii ya kifalsafa iliwekwa miaka mingi iliyopita, mpaka sasa bado ina msaada mkubwa wa kuwa na maisha bora.

Moja ya falsafa bora za kuendesha maisha bora ni falsafa ya Ustoa. Hii ni falsafa ambayo ilianzishwa na Zeno miaka 300 kabla ya Kristo. Falsafa hii iliweza kukuzwa na wanafalsafa kama Seneca, Epictetus, Marcus Aurelius na wengineo.

Leo tunakwenda kujifunza misingi mitatu ya falsafa hii ya ustoa, ambayo ukiiishi unakuwa na maisha bora, yenye furaha, utulivu na mafanikio makubwa.

Misingi hii tumeshirikishwa kutoka kitabu kinachoitwa  How to Be a Stoic: Using Ancient Philosophy to Live a Modern Life kilichoandikwa na mmoja wa wastoa wa zama zetu Massimo Pigliucci

wigo wa udhibiti.jpg

Kitabu ambacho tutapata uchambuzi wake wa kina kwenye TANO ZA JUMA hili la 33.

Karibu kwenye misingi mitatu ya ustoa ya kukuwezesha kuwa na maisha bora.

MSINGI WA KWANZA; WEMA PEKEE NDIYO KITU SAHIHI.

Kuna mambo mengi ambayo huwa tunayafanya na kuhangaika nayo kwenye maisha yetu, lakini mengi siyo muhimu na wala siyo sahihi.

Wastoa wanatuambia wema pekee ndiyo kitu muhimu na sahihi kuhangaika nacho, vitu vingine havipaswi kutusumbua. Wema ndiyo unatuwezesha kuwa na maisha bora na kuweza kutumia vitu vingine kwenye maisha kwa manufaa yetu.

Kwenye falsafa ya Ustoa, wema unajumuisha vipengele vinne muhimu.

Moja; Hekima.

Hekima ndiyo inayotuwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye maisha yetu.

Mbili; Ujasiri.

Kufanya kile kilicho sahihi mara zote bila ya kujali upo katika hali gani. Bila ya ujasiri ni vigumu sana kuishi maisha ambayo ni sahihi kwako.

Tatu; Haki.

Kumtendea kila mtu kwa usawa na ukarimu bila ya kujali hali au hadhi yake kwenye maisha.

Nne; Kiasi.

Kuwa na udhibiti kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako ni muhimu, kutokufanya chochote kwa kupitiliza au kuzidi kiasi.

Ukisimamia mambo haya manne kila wakati kwenye maisha yako, utakuwa na maisha bora sana. Mengine yote nje ya haya manne yamegawanyika kwenye makundi mawili, maovu na yasiyokuwa muhimu. Maovu ni yale ambayo yapo kinyume na hayo manne ya wema, yaani upumbavu, woga, udhalimu na kukosa kiasi.

Ili kuwa na maisha bora, wema ni msingi muhimu sana kujijengea kwenye maisha yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; HANDBOOK OF EPICTETUS (Mwongozo Wa Maisha Bora, Yenye Furaha Na Mafanikio Kutoka Kwenye Falsafa Ya USTOA)

MSINGI WA PILI; ISHI KULINGANA NA ASILI.

Sisi binadamu tunatofautiana na viumbe wengine wote na hata wanyama kwa kitu kimoja, tunao uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Karibu kila kiungo ulichonacho kwenye mwili wako hata nyani pia anacho, karibu kila unachofanya kwenye maisha yako na nyani pia anafanya hivyo hivyo. Lakini kinachokutofautisha wewe na nyani, ni uwezo wako wa kufikiri na kufanya maamuzi.

Uwezo wa kufikiri ndiyo unatufanya sisi kuwa wanadamu, ndiyo unatupa sisi nguvu ya kutawala na kutumia viumbe wengine wote. Lakini kwa bahati mbaya wengi wamekuwa hawatumii uwezo wao wa kufikiri. Badala yake wanaendesha maisha kwa kuiga wengine au kwa kusukumwa na hisia na hilo ndiyo limekuwa linazalisha matatizo na changamoto nyingi kwenye maisha.

Ili kuwa na maisha bora kwanza unapaswa kutumia uwezo wa kufikiri uliopo ndani yako, kisha unapaswa kufuata misingi ya asili. Asili ina majibu ya kila kitu, asili inajiendesha yenyewe kwa kanuni zake ambazo huwa hazivunjwi.

Kama na wewe utaendesha maisha yako kwa kanuni za asili, yatakuwa bora sana, lakini kama utazivunja au kuzipuuza kanuni za asili, na kufanya kile unachojisikia kufanya wewe au wengine wanachofanya, lazima utakaribisha matatizo mengi kwenye maisha yako.

Tumia uwezo wa kufikiri uliopo ndani yako kujua kipi sahihi kwako kufanya, tumia uwezo huo pia kujifunza kupitia asili ili kuweza kufanya maamuzi bora kabisa kwako.

Kwa kuchagua kuishi kwa msingi wa wema, na kufuata asili utaweza kufanya kile kilicho sahihi mara zote.

SOMA; #TANO ZA JUMA #40 2018; Juma La Ustoa Na Misingi Kumi Ya Maisha Ya Furaha, Hatua Za Kuchukua Pale Unaposhindwa Kwenye Kila Unachofanya, Utajiri Na Falsafa, Na Usifuate Njia, Tengeneza Njia.

MSINGI WA TATU; UPACHA WA UDHIBITI.

Tumekuwa tunasumbuka na mambo mengi sana kwenye maisha yetu, lakini mengi ya mambo hayo hakuna tunachoweza kufanya na hivyo kusumbuka nayo hakuna msaada wowote kwetu.

Katika kuondokana na usumbufu wa mambo yasiyo muhimu, Wastoa wana kitu wanakiita UPACHA WA UDHIBITI. Upacha huu unasema mambo yanayotokea kwenye maisha yako yamegawanyika katika makundi mawili;

Kundi la kwanza ni mambo ambayo yako ndani ya uwezo wako wa kuyadhibiti. Mambo haya unaweza kuyaathiri moja kwa moja na hivyo ndiyo unapaswa kuhangaika nayo. Mambo yaliyo ndani ya udhibiti wako ni fikra zako, maamuzi yako na tabia zako. Haya ndiyo unapaswa kusumbuka nayo.

Kundi la pili ni ambo ambayo yako nje ya uwezo wako wa kuyadhibiti. Mambo haya huna chochote unachoweza kufanya ukayaathiri hivyo hupaswi kusumbuka nayo. Maana hata kama utasumbuka kiasi gani, hakuna matokeo unayoweza kuzalisha. Ukiondoa fikra zako, maamuzi yako na tabia zako, mambo mengine yote yapo nje ya uwezo wako wa kuyadhibiti.

Linapotokea jambo lolote kwenye maisha yako, kabla hujaruhusu likusumbue jiulize kwanza je jambo hilo lipo ndani ya uwezo wako au nje ya uwezo wako. Kama lipo ndani ya uwezo wako basi chukua hatua sahihi kulitatua. Na kama lipo nje ya uwezo wako basi achana nalo, maana hata ufanye nini, hutaweza kuliathiri.

Kwa msingi huu wa upacha wa udhibiti, hakuna kitu chochote kinachoweza kutusumbua au kutukwamisha. Kwa sababu kutakuwa na hatua za kuchukua na hivyo kuzichukua au hakuna hatua tunazoweza kuchukua na hivyo kuachana nayo.

Rafiki, ukichagua kuwa mwema, kwa kuishi kwa hekima, ujasiri, haki na kiasi, kisha ukachagua kuishi kwa asili, kwa kutumia uwezo wako wa kufikiri na kufanya maamuzi na ukajua yale yaliyo ndani ya uwezo wako na yaliyo nje ya uwezo wako, hakuna chochote kitakachoweza kukusumbua kwenye maisha yako. Utakuwa na maisha bora, yenye utulivu, furaha ya kudumu na mafanikio makubwa.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE HEALING POWER OF MIND (Nguvu Ya Tahajudi Kwenye Afya, Uzima Na Uamsho)

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA LA 33 la mwaka huu 2019, tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu falsafa hii ya ustoa na jinsi ya kuiweka kwenye maisha yetu na kukabiliana na changamoto mbalimbali kama hasira, upweke, magonjwa, kifo (kwetu na kwa watu wa karibu), mahusiano na mafanikio kwa ujumla. Usikose makala ya TANO ZA JUMA hili la 33.

MUHIMU; DARASA LA USTOA KWENYE KISIMA CHA MAARIFA.

Kama unapenda kujifunza kwa kina na kuweza kuiweka falsafa hii ya ustoa kwenye maisha yako, basi kuna madarasa mbalimbali na miongozo inayoendelea kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Karibu sana ujiunge na KISIMA, ili uweze kujijengea msingi sahihi wa kuwa na maisha bora, yenye utulivu, furaha ya kudumu na mafanikio makubwa, bila ya kujali unaanzia wapi au unapitia nini kwenye maisha yako. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap kwenda namba 0717 396 253 na utatumiwa maelekezo. Karibu sana.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha