Huhitaji ushuhuda wa kuthibitisha kama afya ni kitu muhimu katika maisha yako. Utajiri namba moja duniani ni afya kwani tukiwa na afya tutaweza kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea lakini pia tutaweza kuyafurahia mafanikio yale tunayotafuta.

Huwezi kuona umuhimu wa afya mpaka pale utakapo ikosa. Wengi wamekuwa hawajali sana afya zao, watu wako radhi wajali mali, fedha kuliko hata afya zao binafsi. Wengine wanashindwa kuyafurahia mafanikio waliyonayo kwa sababu ya kuwa na afya mbovu.

Kuna raha gani ya kutafuta mafanikio kwa shida halafu unakuja kuyaona hayana maana wakati ukiwa na afya mbovu? Kumekuwa  na magonjwa mengi siku hizi yanayowashambulia wote kutokana na mtindo tu wa maisha na haya magojwa ni life style diseases. Kuna magonjwa mengine ukiyapata basi unakuwa ni mtu wa kumeza dawa maisha yako yote yaliyobakia hapa duniani.

Maisha Bora

Rafiki, makosa makubwa wanayofanya watu siku hizi ni kutolinda afya zao wakati wakiwa na nguvu. Badala yake watu wako bize kuandaa pesa za kuja kujitibu wakati wakiumwa lakini hawana muda wa kuchukua tahadhari wala kinga dhidi ya afya zao wakiwa wazima.

Wengine wanajisifu kwa sababu wana bima hata wakiumwa ghafla wana uhakika wa matibabu. Kama unaweza kuweka gharama za matibabu  au kujikatia bima kwanini usilipe na gharama ya kulinda afya yako mapema? Kwanini usichukue tahadhari mapema kama ya kutopata magonjwa badala yake unaweka tahadhari ya kujitibu na magonjwa?

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE HEALING POWER OF MIND (Nguvu Ya Tahajudi Kwenye Afya, Uzima Na Uamsho)

Kila mtu anatakiwa kuweka juhudi kulinda afya yake sasa hivi siyo kuweka juhudi ya kuweka fedha na kujikatia bima halafu unajiachia tena bila hata kulinda afya yako  wakati ukiwa mzima. Unaona ukiwa na bima umemaliza kila kitu, ujanja ni kuchukua hatua ya kulinda afya yako wakati ukiwa hujapata ugonjwa siyo kuweka hela ili ukipata magonjwa uje kujitibu.

Kinga ni bora kuliko tiba kama wasemavyo waswahili. Pendelea kutafuta kinga dhidi ya afya yako badala ya kujianda na tiba. Chukua tahadhari ya kila ugonjwa unaoujua na fuata kanuni elekezi  za kiafya  dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Hatua ya kuchukua leo, kama unataka kufurahia maisha ya mafanikio yako basi hakikisha una linda afya yako. weka gharama kubwa ya kinga dhidi ya afya yako kwani usipoweka gharama ya kinga utakuja kulipa gharama kubwa tena yenye riba wakati umepata ugonjwa. Linda afya yako kwani afya yako ndiyo uhai wako.

Hivyo basi, afya yako ipe kipaumbele kama vile unavyovipa vipaumbele vitu vingine. Ingia gharama kwenye kinga  ili uepuke kulipa gharama yenye riba kubwa kwenye matibabu.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu  kwa kutembelea tovuti  hii hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !