Ukitaka usisumbuane na watu, wewe fanya mambo ya kawaida kabisa. Usipange kufanya makubwa na wala usijisumbue kupiga hatua kubwa. Hapo utakuwa na marafiki wengi, lakini wote ni wale ambao hakuna hatua kubwa wanayopiga kwenye maisha yao.

Lakini pale utakapoanza kupanga kupiga hatua kubwa, pale utakapoanza kufanya makubwa, jua utaamsha kila aina ya hisia kutoka kwa wale wanaokuzunguka.

Wengi watakupinga na kukukatisha tamaa, watakupa kila sababu kwa nini unachotaka hakiwezekani, hukiwezi au hakina maana.

Sasa unaweza kuchagua kuwaelezea watu hawa nini unafanya, unaweza kuchagua kubishana nao mpaka uhakikishe wamekuelewa, kuwaeleza kwa kina. Hili litakuchukua muda wako mwingi na kukuzuia kufanya kile unachotaka kufanya.

wp-image--1475273682

Au unaweza kuchagua kufanya kile unachotaka kufanya, kukifanya kwa kina, kuwaacha wale wanaosema waseme, kwa sababu ndicho wanachoweza kufanya, huku wewe ukifanya unachopanga kufanya. Kwa njia hii utawaacha wabishane na matokeo unayopata, wewe hutakuwa na muda wa kubishana nao.

SOMA; UKURASA WA 486; Watu Dhaifu…

Njia ya pili, ndiyo njia bora kabisa ya kuwajibu wale ambao wanakukatisha tamaa na kukupinga. Waache wapambane na matokeo unayozalisha, na siyo wapambane na maneno yako. Kwa sababu maneno yanachochea maneno zaidi, lakini matokeo yanawanyamazisha wote.

Kama watu wanakuambia lengo uliloweka ni kubwa na huwezi kulifikia, kaa kimya na weka juhudi kufikia lengo hilo, unakuwa umewafunga midomo yao kabisa.

Wala usitamani wale wanaokupinga na kukukatisha tamaa wangekuwa upande wako, bali watumie wao kama hamasa ya wewe kupiga hatua. Watumie wao kama sababu ya kufanya kile wanachosema huwezi kufanya, siyo kwa sababu yao, bali kwa sababu yako, lakini wao wanachochea zaidi.

Kujibu maneno kwa maneno ni kujichosha, kupoteza muda na nguvu. Kujibu maneno kwa matendo ni njia bora ya kukuwezesha wewe kupiga hatua na kuwanyamazisha wale wanaosema yasiyo sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog