We should give as we would receive, cheerfully, quickly, and without hesitation; for there is no grace in a benefit that sticks to the fingers. – Lucius Annaeus Seneca
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile tunachofanya ili kuweza kupata matokeo bora.
Kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na TATUA, AMUA NA ONGOZA tunaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari TOA KAMA UNAVYOPOKEA…
Kwa asili, binadamu huwa tunapenda kupokea kuliko tunavyopenda kutoa.
Inapotokea fursa ya kupokea, basi huwa tunaharakisha, na wala hatusiti wala kujiuliza mara mbilimbili.
Lakini inapokuja kwenye kutoa, huwa tunakuwa taratibu, tunasitasita na kujiuliza mara mbilimbili. Inakuwa sana vigumu kutoa na hili linatuzuia kupata zaidi.
Kikubwa kinachowafanya wengi kutokuwa tayari kutoa siyo kwa sababu hawana, kila mtu ana kitu anachoweza kutoa. Kinachowafanya watu wasitoe ni mtazamo wa uhaba, wengi hufikiri dunia ina uhaba, kwamba wakitoa hawatapata tena.
Lakini ukweli wa dunia ni kinyume, dunia haina uhaba, dunia ina utele. Chochote ulichonacho sasa, dunia inautele wa kitu hicho, na inaweza kukupa zaidi na zaidi.
Na pia asili ina tabia ya kurudisha kile kinachotolewa, asili ina tabia ya kujaza kwenye utupu, kwa sababu kuna utele.
Kudhibitisha hili, lima shamba, ondoa kila aina ya uoto, kisha weka maji na mbolea, utashangaa baada ya muda kunakuwa na uoto wa kutosha.
Asili ina utele na asili inajaza popote penye utupu, hivyo unapotoa, unaipa asili kazi ya kujaza kile kilichoondoka.
Uwe na siku bora ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha