“The world turns aside to let any man pass who knows where he is going.” -Epictetus
Hongera mwanamafanikio kwa nafasi hii nzuri ya siku mpya ya leo.
Ni fursa ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; DUNIA ITAKUPISHA…
Kila mmoja wetu amewahi kuwa na mipango mikubwa ya kuyafanya maisha yake kuwa bora sana.
Na wakati wa kupanga huwa hakuna shida kubwa, ni katika utekelezaji ndipo kila kitu huanza kuonekana ni kigumu na hakiwezekani.
Tunapoanza kutekeleza kile tulichopanga, ndipo tunaona kama dunia nzima ipo kinyume na sisi, hata watu tuliotegemea wawe msaada, wanakuwa vikwazo.
Hapa ndipo wengi wanapokata tamaa na kushindwa kupiga hatua.
Lakini pia wapo wengine wanaokutana na hali hizo, lakini wanaendelea na kile walichopanga na mwishowe wanavuka kila aina ya changamoto na kupata kile wanachotaka.
Watu hawa wanakomaa licha ya vikwazo na changamoto wanazokutana nazo, na dunia inawashindwa na kuwaachia wapate kile wanachotaka.
Tofauti kubwa ya wale wanaoendelea na wanaoishia njiani inaanzia kwenye kujia hasa kile ambacho mtu anataka na kujitoa kutaka.
Kama unajua kwa hakika nini unataka, na umejitoa kukipata, dunia itakupisha upate hicho unachotaka. Dunia haiwezi kabisa kukuzuia wewe kupata kile unachotaka, kama unakijua hasa na umejitoa kukipata hata iweje.
Lakini kama huna uhakika na unachotaka na hujajitoa hasa kukipata, dunia haitakuruhusu kamwe ukipate. Kila kitu kitakuwa kikwazo kwako, kuanzia wewe mwenyewe. Kila hatua utakayoanza kupiga itakuwa ngumu na utaacha haraka sana.
Rafiki, jua kile unachotaka hasa, jua kwa nini unakitaka, kisha jitoe kweli kukipata, jiahidi hakuna kitakachokurudisha nyuma usipate kitu hicho. Dunia itakujaribu kwa kukuletea magumu na changamoto, halafu wewe utaendelea kupambana maana umejitoa, mwishowe dunia itaona wewe hufai kuzuiwa, itakuachia upate kile unachotaka.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha