Kila kitu unachokutana nacho kwenye maisha yako, kinachangia namna ambavyo maisha yako yanakwenda. Hata kama unaona ni kitu kidogo kiasi gani, hakuna kisichokuwa na madhara kwako.
Kwa mfano kila mtu yupo pale alipo sasa, kutokana na hatua alizochukua au kutokuchukua huko siku za nyuma. Na atakapokuwa mtu kesho, ni matokeo ya hatua ambazo mtu amechukua leo.
Sasa unapoiangalia kesho, wengi hufikiri inatokea tu, kwa sababu lazima kesho ije. Ni kweli kesho lazima ije, lakini maisha yako yatakuwaje kesho, hichi ndiyo unapaswa kukifanyia kazi leo.
Tumekuwa tunajifunza kwamba watu tunaokuwa nao muda mrefu ndiyo wanatengeneza tabia zetu. Na mara nyingi, hatua tunazopiga kwenye maisha huwa hazitofautiani sana na wale wanaotuzunguka.

Wapo ambao wakisikia hilo wanaona wao ni wajanja, wanaweza kwenda mbali zaidi kuliko wale ambao wamewazunguka. Wanaamini kwamba wanaweza kukaa na watu lakini wasisikilize kile wanachosema au wasifuate ushauri wao.
Hapo ndipo watu wanajidanganya kwa sababu athari za watu kwako hazitokani na kile wanachokuambia au kukushauri pekee. Upo mlolongo mrefu ambao unazalisha athari hizi.
SOMA; UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…
Na kwa hakika mlolongo huo uko hivi;
Watu wanaokuzunguka, wale ambao unatumia nao muda wako mwingi, wanatengeneza mazingira ambayo utakuwa ndani yake. Kwa jinsi watu wanavyochukulia mambo yao, jinsi wanavyohusiana na wengine na hata hatua wanazochukua, zinatengeneza aina ya mazingira ambayo wewe unakuwa ndani ya mazingira hayo.
Mazingira hayo unayoishi ndiyo yanatengeneza na kuamua mtazamo ambao unakuwa nao. Najua kabisa ya kwamba kama umezungukwa na watu waliokata tamaa, haikuchukui muda na wewe utakata tamaa, hata kama hawakuambii lolote. Ni ile nguvu hasi inayokuzunguka ndiyo inakuzamisha.
Ni mtazamo wako wa leo ndiyo unatengeneza kesho yako. Mtazamo ndiyo unakufanya uchukue au usichukue hatua fulani.
Sasa umeona hapo, namna watu wanavyoweza kukuathiri hata kama hawakuambii lolote moja kwa moja. Na ndiyo maana mtu akishaingia eneo fulani, haimchukui muda anakuwa kama wale aliowakuta kwenye eneo lile, hata kama hakuna anayemfundisha. Ni kwa sababu mazingira yaliyotengenezwa pale, yanaleta aina hiyo ya matokeo.
Kuwa makini na aina ya watu unaokubali kuwa nao na aina ya mazingira ambayo wameshayatengeneza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog