Wanasayansi wanaanza kukubaliana na kitu ambacho viongozi wa kiroho na wanafalsafa wamekuwa wakisema tangu enzi na enzi. Kwamba upo uwezekano kwamba mtu kama mtu siyo nafsi moja. Yaani kuna uwezekano ndani yako zipo nafsi nyingi. Na ubaya ni kwamba, nafsi hizi hazikubaliani kwenye jambo lolote kwa wakati mmoja, labda mpaka iwe ni hatari kubwa.
Na unaweza kuona hili kwenye mipango mbalimbali unayoweka. Kwa nini unapanga kitu lakini wakati wa kuchukua hatua ukifika unaahirisha? Yaani wewe mwenyewe upange, halafu wewe mwenyewe ujipinge? Uwezekano mkubwa ni kwamba nafsi moja imepanga, lakini nafsi nyingine haitaki.

Pia kila mmoja wetu amekuwa na mijadala ambayo inaendelea kwenye mawazo yake. Ni kama unabishana na wewe mwenyewe, na hili linaonesha siyo tu unabishana na wewe, bali unabishana na nafsi nyingine zilizopo ndani yako. Na pale hisia kali zinapokutawala, ni kama anakuja mtu mwingine tofauti kabisa na kuishi ndani ya mwili wako. Unajikuta unafanya mambo ambayo umewahi kukataa kabisa kwamba hutafanya.
Sasa kusikia hili, kwamba upo uwezekano kuna nafsi nyingi ndani yako lisikufanye uwe mzembe. Kwamba uamue tu kuahirisha mambo kwa sababu kuna nafsi ndani yako haikubaliani na ulichopanga.
Badala yake unapaswa kuchagua nafsi moja itakayotawala, na hii ni ile nafsi inayoelewa vizuri maono na ndoto kubwa za maisha yako. Hii ndiyo nafsi ambayo itazilazimisha nafsi nyingine ziweze kuchukua hatua, hata kama hazitaki.
SOMA; #TAFAKARI YA LEO; UHURU NI KUWEZA KUJITAWALA…
Lazima uwe na mfalme ndani yako, ambaye neno lake ni sheria, ambaye hana mjadala, akishaagiza kinafanyika. Hivyo pale unapopanga kwamba muda fulani utafanya kitu fulani, halafu muda huo unafika, ila unaanza kujishauri kwamba siyo sahihi kufanya kwa wakati huo, jua nafsi nyingine zinataka kuleta mjadala. Hapo sasa ndipo mfalme anapaswa kuinuka na kusema hakuna mjadala, tunafanya kama nilivyopanga.
Swali ni je unawezaje kumfikia mfalme? Kwa sababu nafsi zipo nyingi, unajaje na kufikiaje ile nafsi ambayo ndiyo inayotawala?
Na njia ni moja, fanya TAHAJUDI YA UWEPO KIAKILI (MINDFUL MEDITATION). Hii ni tahajudi ambayo inatuliza mawazo yako, kuyaondoa kwenye kuzurura na kuyaleta kwenye eneo moja ambalo umechagua. Kwa kufanya tahajudi hii, unailazimisha akili na mawazo yako kutulia na hivyo zile nafsi nyingine zote zinazokuletea changamoto zinatulia kabisa. Na hapo sasa ndiyo unaweza kupata nafasi ya kupitia ndoto na maono makubwa ya maisha yako, kupitia mipango uliyojiwekea na kuchukua hatua ulizopanga kuchukua.
Kama hutachagua nafsi moja itakayokutawala, kama hutaweza kutuliza akili na mawazo yako ili kuweza kuchukua hatua, utajikuta unatumia muda wako mwingi wa siku kubishana na wewe mwenyewe kama ufanye au usifanye, hilo litakuchosha na mwisho wa siku utachoka na hutafanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog