“He who is most slow in making a promise is the most faithful in performance of it.” -Jean-Jacques Rousseau
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio kwa mwaka huu 2018.
Asubuhi ya leo tutafakari AHADI ZA HARAKA…
Kitu chochote ambacho mtu utaahidi kwa haraka, bila ya kujitafakari na kujipima utakitekelezaje, huwa kigumu sana kwenye utekelezaji.
Na wale wanaokutaka uahidi kitu, huwa hawapendi ukae na kukifikiri kitu hicho kwa muda, badala yake wanataka uahidi haraka.
Wanajua ukijipa muda wa kufikiri utaona kila kitu na kufanya maamuzi sahihi.
Hivyo wanakuweka kwenye mazingira ya wewe kuahidi haraka halafu wakusumbue kwenye utekelezaji wa ulichoahidi.
Mara zote, usikimbilie kuahidi, hata kama kitu kinaonekana ni rahisi na muhimu kiasi gani.
Jipe muda wa kukitafakari na kukijua kitu kabla hujakiahidi.
Kadiri unavyochukua muda na kukielewa kitu kabla ya kuahidi, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kufanyia kazi katika kutekeleza.
Usikimbilie kuahidi kile ambacho bado hujakielewa.
Hakuna popote unapochelewa, hakuna chochote kinachokupita.
Jipe muda wa kutafakari na kujua kwa kina kabla ya kuahidi.
Siku ya leo iwe bora sana kwako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha