How much time he saves who does not look to see what his neighbor says or does or thinks. – Marcus Aurelius
Ni asubuhi nyingine nzuri kwetu, siku mpya kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio kwa mwaka huu 2018.
Asubuhi ya leo tutafakari UKIACHA KUFUATILIA YA WATU UTAPATA MUDA WA KUTOSHA…
Utakuta watu wanalalamika hawana muda kwenye maisha yao, lakini wakati huo huo wanajua kila kosa la kila mtu, wana cha kukosoa kwa kila mtu na wanafuatilia kila kinachoendelea kwa wengine.
Kama mtu utaacha kufuatilia maisha ya wengine, ukaacha kutafuta kila aina ya makosa, ukaacha kutafuta kila cha kukosoa utakuwa na muda mwingi wa kufuatilia mambo yako mwenyewe.
Changamoto kubwa ya zama hizi, huhitaji hata kwenda kwa mtu ili kujua nini kinaendelea kwenye maisha yake, wala huhitaji kuuliza wengine, bali kila kinachoendelea kwenye maisha ya wengine kipo kwenye mikono yako, kupitia simu yako, kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa kuwa sasa mitandao ya kijamii ndiyo kioo cha kila mtu, ni rahisi kujikuta unapoteza muda kuangalia fulani anafanya nini, au yupo wapi na kadhalika.
Sasa taarifa hizi za mitandao ya kijamii ndiyo mbovu zaidi, kwa sababu nyingi zinaonesha upande mmoja na mdogo sana wa maisha, ule upande wa furaha.
Hivyo unaweza kuona wengine maisha yao yako vizuri mno, lakini ya kwako ndiyo yako hovyo, na huwezi kukosea zaidi ya hapo.
Muda wako ni mchache, nguvu zako ni ndogo sana kuweza kujua kila kinachoendelea kwa wengine na bado ukapata muda wa kufanya yale muhimu kwako.
Hili halimaanishi usijali wengine na kuwa mbinafsi, jali wengine kwa kujua wanaendeleaje, lakini usipoteze muda wako kuanza kuchunguza kila kitu cha maisha yao, hasa kwenye mitandao ya kijamii, au kupitia maneno ya wengine.
Chochote utakachokazana kujua kuhusu wengine, hakitakuwa na msaada mkubwa kwako.
Elekeza muda na nguvu zako kwenye ndoto na maono makubwa ya maisha yako.
Uwe na siku njema ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha