Kila mtu ana nishati ambayo inachochea hamasa yake, kitu ambacho kinampa ari ya kuendelea zaidi hata kama mambo yanaonekana kuwa magumu.
Hatua ya kwanza kwako ni kujua nishati ya hamasa yako, ili uweze kuitumia kila wakati, hasa pale unapotaka kukata tamaa au kuahirisha kile ambacho umepanga kufanya.

Ukishaijua nishati ya hamasa yako, hakikisha wakati wote inakuwa karibu yako.
Inaweza ikawa mwandishi fulani ndiyo nishati ya hamasa yako, hivyo kila mara unapojisikia kukata tamaa au kuahirisha, ukisoma kazi yake unapata hamasa ya kuendelea tena. Hivyo hakikisha kazi za mwandishi huyo unakuwa nazo wakati wote.
Inaweza kuwa pia nishati ya hamasa yako ni muziki wa aina fulani au wa mwimbaji fulani. Hakikisha unakuwa na mkusanyiko wa miziki hiyo na kuweza kuisikiliza kwa wakati ambao unahitaji hamasa ya kusukuma zaidi.
SOMA; UKURASA WA 970; Hamasa Haisubiriwi, Hamasa Inatengenezwa…
Pia tabia zako binafsi na yale unayofanya yanaweza kuwa nishati ya hamasa yako, labda ni mazoezi, tafakari, tahajudi na hata kujikumbusha ulikotoka na unakokwenda.
Hakikisha unaijua nishati ya hamasa yako na kuwa nayo karibu ili kuweza kuitumia wakati unapoihitaji.
Ni muhimu sana kuijua nishati ya hamasa yako kwa sababu usipoijua, utapotezwa na kelele nyingi za dunia. Utaishia kwenye mitandao ya kijamii ukidhani ndiyo nishati ya hamasa kumbe ndiyo kitu kinachokunyonya hata ile hamasa ndogo uliyokuwa nayo.
Pia kilevi chochote kile, au kitu kinacholeta uteja ambacho siyo cha asili kwako, usikubali kiwe ndiyo nishati yako ya hamasa. Kwa sababu ukishakuwa mteja, matatizo yanakuwa makubwa kuliko hamasa unayoipata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog