Hongera rafiki yangu kwa juma hili namba kumi, juma ambalo tunakwenda kulimaliza, juma ambalo ninaamini umepiga hatua kubwa, na kujifunza mengi pia.

Karibu kwenye #TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu niliyojifunza na ambayo nimekutana nayo, ambapo nina hakika wewe rafiki yangu yatakuwa na msaada kwako.

Jukumu nililojipa ni kukupa wewe maarifa sahihi, ila wewe una jukumu la kuchagua kutumia maarifa hayo kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Karibu kwenye tano za juma, soma mambo haya matano, yafanyie kazi na maisha yako hayatabaki pale yalipo sasa.

#NENO; SABABU HAZITALIPA BILI.

Labda kwa dakika moja tukubaliane na sababu zote ambazo unatoa;

Kwamba mambo ni magumu,

Uchumi ni mgumu,

Kwamba mshahara wako ni mdogo na hautoshelezi,

Kwamba biashara zina changamoto na hakuna faida,

Kwamba unanyonywa na kuonea na wengine,

Unaweza kuendelea kuorodhesha kila sababu kama utakavyo,

Lakini sasa ni kuulize sababu moja, unapoenda dukani kununua kitu unaenda na sababu? Vipi unapotafuta chakula, unapata kwa sababu? Je ukitaka umeme uwake nyumbani kwako, unaingiza sababu kwenye luku?

Kama hujajibu ndiyo kwenye maswali hayo hapo juu, basi jua sababu hazina maana. Ni ujinga na upotezaji wa muda. Sababu hazitalipa bili yoyote unayopaswa kulipa.

Kinacholipa bili ni fedha, hivyo kama huna fedha, jibu ni utafute fedha, na siyo sababu. Kuna ugumu gani kwenye hilo?

Kama kipato chako hakitoshelezi ongeza kipato, unataka uambiwe hilo kwa kilugha gani?

Chagua leo, kuweka juhudi zako kwenye kuongeza kipato chako, au kuweka juhudi hizo kwenye kutafuta sababu. Mwisho wa siku uhuru wa kuchagua ni wako na kila mtu anapata kile anachochagua.

#1 KITABU NILICHOSOMA; WHEN BREATH BECOMES AIR.

Kazi kubwa ya falsafa na hata imani mbalimbali imekuwa kujua nini maana ya maisha, kwa nini tupo hapa duniani, na baada ya maisha haya ya dunia nini kinafuata? Haya ni maswali ambayo kila mtu anajaribu kuyajibu kwa namna anavyofikiri na kwa uelewa alionao. Lakini kwa sehemu kubwa yanabaki kuwa siri, kwa sababu hakuna aliye na hakika juu ya mambo hayo.

Ni kama giza kubwa ambalo lipo mbele yetu, kwa nini mtu azaliwe na kufa hapo hapo, mwingine aishi miaka 10 afe, mwingine miaka 90. Ni maswali mazito ambayo hayana majibu sawa kwa wote.

Aliyekuwa mwandishi na daktari Paul Kalanithi, alijipa kazi ya kutafuta majibu ya maswali hayo. Lakini kilichotokea kwenye maisha yake, kilikuwa ni zaidi ya jibu. Safari ya maisha yake ilikatika wakati ambapo ndiyo alikuwa anafikia kilele cha mafanikio ya maisha yake. Aligundulika kuwa na kansa ya mapafu wakati ambapo ndiyo alikuwa anakaribia kuhitimu masomo yake ya udaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.

Katika kitabu chake cha WHEN BREATH BECOMES AIR, Paul anatushirikisha safari hii ya maisha yake. Na kikubwa ambacho tunaweza kujifunza kwenye safari yake hiyo, na hata kupitia mafunzo ya falsafa na imani ni kwamba, maisha ni kuishi sasa na kifo ni uhakika. Kwa kuwa wote tuna uhakika tutakufa, na kwa kuwa hatujui ni lini kifo hicho tutakutana nacho, basi kitu pekee tunachoweza kufanya ni kuishi sasa. Tusiache chochote tunachoweza kufanya leo kwa ajili ya kesho,  siku ya furaha ni leo, siku ya kufanya kile tunachojali ni leo. Inawezekana una mwaka mmoja, miaka 10 au hata miaka 50, huwezi kwa hakika.

Ishi sasa, fanya yale ambayo ni muhimu, yenye maana kwako na kwa wengine, na usipoteze hata dakika yako moja kwa jambo lisilo na maana kwako.

#2 MAKALA YA WIKI; Kila unachopaswa kujua kuhusu cryptocurrency na bitcoin.

Tangu enzi na enzi, binadamu tumekuwa tunakazana na kitu kimoja, kutafuta njia ya mkato ya utajiri. tumekuwa tunakazana kutafuta njia ya kupata fedha nyingi kwa haraka na bila ya kufanya kazi. Lakini katika kipindi chote ambacho dunia imekuwepo mpaka sasa, haijawahi kutokea njia ya aina hiyo, na hata inapopatikana kwa muda mfupi, basi huishia kuanguka.

Kwenye makala ya wiki hii nimeeleza jinsi ambavyo fedha za kidijitali, kama zinavyojulikana kama CRYPTOCURRENCY na kiongozi wa sarafu hizi ikiwa BITCOIN zitakavyowaponza wale wasio na uelewa wa mambo ya fedha na uwekezaji. Nimeeleza kila unachopaswa kujua kuhusiana na fedha hizi na sababu tano kwa nini usihangaike nazo kwa sasa.

Unaweza kusoma makala hiyo hapa; Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Cryptocurrency Na Bitcoin (Fedha Za Kidijitali) Na Kwa Nini Siyo Uwekezaji Mzuri Kwako Kwa Sasa. (https://amkamtanzania.com/2018/03/07/kila-kitu-unachopaswa-kujua-kuhusu-cryptocurrency-na-bitcoin-fedha-za-kidijitali-na-kwa-nini-siyo-uwekezaji-mzuri-kwako-kwa-sasa/ )

Imani yangu ni kwamba utajifunza na kisha kufanyia kazi yale unayojifunza. Usikubali kudanganywa na kuingia kwenye kitu ambacho hukielewi, wengi wamepotezwa kwa kufuata mkumbo.

#3 NILICHOJIFUNZA; DUNIA INA MABILIONEA WAPYA 259.

Kila mwaka, mwezi machi, jarida la Forbes, ambalo ni maarufu kwa habari za fedha, uwekezaji na utajiri, limekuwa linatoa orodha ya watu matajiri zaidi duniani. Katika kipindi hichi cha mwaka, huwa wanatoa orodha ya mabilionea wote duniani, kwa kiasi chao cha fedha na vyanzo vyao vya kipato.

Mtu anapoitwa bilionea, maana yake utajiri wake wote, kuanzia fedha mpaka mali anazomiliki unazidi dola bilioni moja za kimarekani, sawa na shilingi za kitanzania trilioni mbili na bilioni mia mbili hamsini na tano.

Katika orodha ya mwaka huu 2018, kuna mabilionea wapya 259. Jumla ya mabilionea wote duniani kwa sasa ni 2,208. Kwa pamoja mabilionea wote utajiri wao ni dola  trilioni 9.1 ambapo ni ongezeko la 18% ukilinganisha na mwaka uliopita. Hii ni dalili kwamba utajiri unaongezeka duniani.

Mtu tajiri namba moja kwenye orodha hii ya mwaka 2018 ni Jeff Bezos ambaye ni mmiliki wa kampuni ya amazon ambayo inajihusisha na kuuza vitu kwenye mtandao wa intaneti. Ndiye bilionea wa kwanza kuwa na kiasi cha fedha kinachozidi bilioni 100, kwa sasa utajiri wake ni dola bilioni 112, akifuatiwa na Bill Gates ambaye ni mmiliki wa Microsoft mwenye utajiri wa dola bilioni 90. Warren Buffet, mwekezaji mkubwa duniani anashika nafasi ya tatu akiwa na utajiri wa dola bilioni 80. Unaweza kuangalia orodha nzima ya mabilionea hawa kwenye kiungo hichi; https://www.forbes.com/billionaires/list/

Tunajifunza nini kwenye orodha hii ya bilionea?

Tunaposoma orodha hii ya mabilionea, hatuishii tu kufurahia kwamba fulani kapanda na nani kashuka, wala lengo siyo kujua kama kuna wengine wenye utajiri zaidi lakini hawapo kwenye orodha. Tunachopaswa kujifunza ni kwamba, wapo watu wanaotengeneza utajiri mkubwa duniani, ambao unaweza kudhibitishwa ni kwa njia halali na sahihi.

Hivyo basi, na sisi tunayo nafasi ya kuingia kwenye orodha hii, kama tutajifunza yale wanayofanya wale waliopo kwenye orodha, na kujitoa kama ambavyo wao wamejitoa, bila ya kusahau muda ambao wamewekeza. Kwa mfano amazon ilianzishwa mwaka 1993, lakini ni miaka 20 baadaye ndiyo imeweza kumwezesha mwanzilishi wake Jeff Bezos kuwa tajiri namba moja duniani. Kwa mwaka mmoja pekee, kutoka 2017 mpaka 2018, hisa za kampuni ya Amazon ziliongezeka thamani kwa asilimia 59, na kumwingizia Bezos dola bilioni 39.2 ndani ya mwaka mmoja tu. Kama huijui safari hiyo ya miaka 20, utasema jamaa ana bahati, amelala masikini na kuamka tajiri, kitu ambacho hakijawahi kuwepo na wala hakitakuja kuwepo.

Tujue wapi tunakwenda, tuweke juhudi na tujipe muda, hakuna cha kutuzuia bali sisi wenyewe.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KISIMA CHA MAARIFA NDIPO UTAKAPONIPATA.

Kadiri huduma ya uandishi na ushauri ninayotoa inavyozidi kukua, ndivyo watu wengi wanahitaji kupata muda wangu kwa ajili ya mahitaji yao mbalimbali. Lakini hilo ni changamoto kwangu, kwa sababu muda ni mfupi na mambo ya kufanya ni mengi. Hivyo sehemu pekee ambayo mtu unaweza kunipata moja kwa moja, ukaniuliza chochote na nikakujibu, au ukanishirikisha changamoto zako na nikakupa ushauri wa moja kwa moja ni kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Ukishakuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA unakuwa na nafasi kubwa hata ya kuweza kupata huduma nyingine ninazotoa kama COACHING PROGRAM na hata kuhudhuria semina mbalimbali ninazotoa.

Hivyo kama umekuwa unanufaika na mafunzo ninayotoa, ila bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, huu ndiyo wakati wako kuchukua hatua hiyo.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kujiunga tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap namba 0717396253.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; UKWELI HAUJAWAHI KUMUUMIZA YEYOTE.

“If anyone can refute me—show me I’m making a mistake or looking at things from the wrong perspective—I’ll gladly change. It’s the truth I’m after, and the truth never harmed anyone.” – Marcus Aurelius

Marcus Aurelius, aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa Ustoa, ana maneno mazuri kwetu kuhusu ukweli. Wengi wetu huwa hatupendi kuambiwa ukweli, hasa pale ambapo ukweli unatufanya tuonekane tumekosea au tupo upande tofauti. Lakini Marcus anatuambia kama ukweli unakufanya kuwa sahihi, basi unapaswa kuukubali na kubadilika. Kwa sababu, ukweli haujawahi kumuumiza yeyote.

Hivyo mtu anapokuambia kitu, na ndani yako ukafikiri na kuona ni sahihi, usitake kuonekana kwamba na wewe upo sahihi, badala yake badilika.

Nakutakia kila la kheri kwenye juma #11 tunalokwenda kuanza, nenda kautafute ukweli, nenda katafute fedha na siyo sababu na nenda kaishi kila dakika ya maisha yako bila ya kuahirisha chochote. Usisahau pia ya kwamba, ndoto yoyote kubwa uliyonayo, inahitaji kujitoa, inahitaji kuweka juhudi na inahitaji muda, tena siyo muda mdogo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0