We become wiser by adversity; prosperity destroys our appreciation of the right. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari CHANGAMOTO ZINAJENGA BUSARA…
Changamoto tunazopitia kwenye maisha, ndiyo zinatufanya tufikiri zaidi, ndiyo zinatufanya tutafute maarifa zaidi na ndiyo zinatufanya tujaribu mambo mengi zaidi.
Ni katika kufanya hayo ndiyo tunajifunza zaidi, na kuwa na busara zaidi.
Hata unapokaa na kuwahadithia watu ulipotoka mpaka ulipo sasa, kikubwa utakachokuwa unawaeleza ni changamoto ulizokutana nazo na jinsi ulivyozivuka.
Mafanikio mara nyingine huleta uvivu, huleta mazoea na ndiyo maana haya upige hatua kiasi gani, changamoto haziondoki kabisa, ila tu zinabadilika.
Unapotatua changamoto unazokutana nazo, unajijengea uzoefu na pia unapiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
Pia unakuwa na ushauri na mwongozo mzuri kwa yeyote anayepitia hali kama uliyopitia wewe.
Hivyo tusiziogope wala kuzikimbia changamoto,
Badala yake tuzikaribishe, tukijua ndiyo chanzo cha busara, ndiyo zinazofanya tufanikiwe zaidi.
Uwe na siku njema, usikimbie changamoto za leo, bali zifanyie kazi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha