Unaianza siku kwa mipango yako au mipango inajitokeza ndani ya siku na unaifanyia kazi?

Kila siku unaianza kwa ajenda zako binafsi au unapokea ajenda za wengine na kuzifanyia kazi?

Unadhibiti muda wako wa siku au muda unaenda tu na hujui unapotelea wapi?

Mtu Pekee

Tunapanga makubwa, tunakuwa na ndoto na maono makubwa ya maisha yetu, lakini tunasahau kitu kimoja, kwamba yale makubwa ambayo tunayaona mbele, yanatengenezwa kwa siku moja moja.

Kwamba ukiishi siku ya leo kwa mafanikio, unasogea karibu na ndoto yako. Lakini kama utaipoteza siku ya leo, unakwenda mbali zaidi na ndoto yako.

SOMA; TABIA ZA MAFANIKIO; Kujenga Tabia Ya NIDHAMU BINAFSI.

Siku moja ni kiungo muhimu sana cha mafanikio yako. Unachofanya kila siku kimechangia kukufikisha hapo ulipo sasa. Hivyo kama unataka kufika mbali zaidi ya hapo ulipo, hatua ya kwanza ni kuangalia jinsi kila siku yako inavyokwenda.

Ogopa kuishi kila siku yako kwa mazoea, kufanya leo kama ulivyofanya jana, kuona hakuna jipya, mambo ni yale yale.

Epuka sana usumbufu ambao umekuzunguka kila kona, usumbufu ambao unaiba muda wako na kupoteza nguvu zako. Usumbufu unaokudanganya uone mambo ni muhimu na yanakupita, kumbe hata siyo.

Linda siku yako sana, ukiruhusu ipotee, ukiruhusu wengine waichezee, unakuwa umechagua kukosa wewe mwenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog