Kitu ambacho nimejifunza kwenye maisha ni kwamba, binadamu huwa tunazaliwa tukiwa na maandalizi ya kutosha kupambana na changamoto za dunia. Mtoto mchanga aliyezaliwa leo, akisikia sauti kali atashtuka, akiona kitu kinakuja mdomoni kwake ataanza kunyonya, akiona kama anaanguka anajishika kwenye kitu. Kumbuka huyu ni mtoto wa siku moja, ambaye hajafundishwa chochote kuhusu maisha, bali amekuja kwenye hii dunia akiwa na maandalizi ya kutosha, kuhakikisha anapona na kukua.

Lakini sasa, mazingira ambayo tumekuwa tunakutana nayo hapa duniani yamekuwa yanatutengenezea vitu vya tofauti. Yanatuaminisha kwenye vitu ambavyo siyo sahihi, na kutufanya tusahau kwamba ndani yetu tuna kitu kikubwa cha kutuwezesha kupiga hatua kwenye haya maisha.
Sehemu kubwa ya mazingira inayowaharibu wengi ni mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu umekuwa unaanzia kwenye msingi kwamba, mtoto hajui chochote na hana uwezo wowote na hivyo ni kazi ya mfumo wa elimu kumtengeneza. Na hivyo hapa anafuta kila ambacho kilikuwa ndani ya mtu na kujenga vitu vipya, ambavyo haziwezi kuwa sawa kwa kila mtu.
Ni sawa na kuchukua kompyuta zote duniani na kusema lazima zitumie programu ya aina moja, hivyo kufuta programu nyingine zote na kuweka moja tu. Kama umewahi kutumia kompyuta, unajua kabisa kuna kompyuta zitakubali na nyingine nyingi zitakataa au hazitaendana na programu ile. Lakini hilo halimaanishi kwamba kompyuta hizo ni mbovu, bali inamaanisha zipo tofauti na zinahitaji programu sahihi.
SOMA; UKURASA WA 1053; Kadiri Uimara Unavyokuwa Mkubwa, Ndivyo Udhaifu Unakuwa Mkubwa Pia….
Hivyo hata kwenye maisha yako, popote ambapo umewahi kushindwa, haimaanishi kwamba wewe hufai, bali inamaanisha kwamba ukikuwa hujajua kipi sahihi kwako. Hivyo kama utaweka juhudi na kujua kipi hasa ni sahihi kwako, na ukakifanya kwa namna hiyo ambayo ni sahihi, utafanikiwa.
Hata kama shuleni walikuambia wewe ni wa kushindwa, kwa sababu hukufaulu mitihani, haimaanishi kwamba wewe hufai, badala yake mfumo wa elimu uliokuwa unalazimishwa uende nao haukukufaa wewe.
Huenda pia umewahi kuwa kwenye kazi ambayo kila mtu anafanikiwa na kupiga hatua, ila wewe ndiyo hujielewi hata unafanya nini. Kila siku unakutana na changamoto na unaonekana kama ni mzembe na hujui unachofanya. Haimaanishi kwamba wewe hufai kabisa, bali inamaanisha kazi unayokazana kwenda nayo, siyo ya aina yako. ukiweza kupata ile kazi inayoendana na wewe, utaweza kupiga hatua kubwa sana.
Hivyo rafiki yangu, kama hukufa ulipokuwa mtoto, wakati ambapo ulikuwa huwezi kuongea lakini uliweza kutoa ujumbe kwamba una njaa, unamuwa au tu hujisikii vizuri, basi una uwezo wa kutosha wa kufanikiwa kwenye maisha yako. Asikuambie yeyote kwamba umeshindwa na huwezi tena. Tafuta kile kinachoendana na wewe na weka juhudi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog