Accept the things to which fate binds you, and love the people with whom fate brings you together, but do so with all your heart. – Marcus Aurelius

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa sana kwenye siku yetu hii.

Asubuhi ya leo tutafakari POKEA VITU, WAPENDE WATU.
Asili huwa inatuweka kwenye mazingira tofauti tofauti katika kipindi chote cha maisha yetu.
Huwa tunajikuta kwenye mazingira ambayo huenda hatuyapendi sana, tukiwa na vitu ambavyo hatuvikubali, huku tumezungukwa na watu ambao hatuendani nao.

Kitu ambacho wengi wamekuwa wanafanya ni kukataa yale mazingira ambayo asili imewaweka. Kukataa vile vitu ambavyo hawavikubali na kuwachukia wale watu ambao hawaendani nao.

Lakini kufanya hivyo kumekuwa hakuwapi faida wala mabadiliko yoyote, badala yake inafanya mambo kuzidi kuwa magumu zaidi, kwa sababu mtu anaendelea kuwa kwenye mazingira hayo kwa muda mrefu.
Na kadiri mtu anavyopigana kuondoka kwenye mazingira hayo, ndivyo anazidi kukaa kwenye mazingira hayo.

Hatua sahihi kuchukua ni kupokea na kukubali yale mazingira ambayo asili imetuweka na kuwapenda wale watu ambao asili imetuletea. Tunafanya hivi tukijua kwamba mambo hayo hayatakaa milele, kila kitu kinabadilika ha hivyo mazingira ambayo mtu upo yatabadilika pia.

Unapopokea kile asili inakupa, na kupenda watu ambao umekutanishwa nao na asili, kwanza maisha yanakuwa rahisi, hakuna msongo na mtu unaweza kufanya makubwa. Pili mambo yanabadilika haraka na kujikuta upo kwenye mazingira mazuri zaidi, ukiwa na watu bora zaidi ambao unaendana nao.

Pokea kila ambacho asili inakupa, na wapende wale wote ambao asili imekukutanisha nao. Ni muda mfupi utautumia kwenye mazingira mbalimbali, ufanye kuwa muda bora kabisa kwako.

Siku yako leo ikawe njema na ya kufanya kwa ubora zaidi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha