Katika mipango yetu ya maisha, kuna vitu ambavyo tumekuwa tunafanya ambavyo vinaturudisha nyuma au vinatuzuia kufika kule ambapo tunataka kufika.

Na hivyo katika kuhakikisha tunaondokana na mambo hayo, tunapanga kutokufanya vitu fulani. Lakini kinachotokea ni kwamba, tunajikuta bado tunafanya, na hivyo kuona kama tumeshindwa kuondokana na mambo hayo yanayoturudisha nyuma.

Unachopaswa kujua ni kwamba, mpango wowote wa kutokufanya kitu ni mpango wa kushindwa. Ukishajiambia sitafanya hichi na ukaishia hapo, unaacha nafasi ya nafsi yako kuendelea kufikiria kitu hicho. Hivyo hata kama hutakifanya, bado utatumia muda mwingi kukifikiria na kujikuta bado unacho kitu hicho.

Huwezi Kuona

Unachopaswa kupanga ni utafanya nini kwenye nafasi ya kile ambacho hutaki kufanya. Badala ya kupanga tu kwamba hutafanya kitu fulani, panga pia kwamba utafanya nini kama mbadala wa kitu hicho. Hapo jipe kitu cha kufanya, kitu ambacho ni muhimu, kitu ambacho kinakupa hamasa na msukumo wa hali ya juu.

SOMA; UKURASA WA 1048; Fikiri, Kuwa, Zalisha…

Hivyo mazingira yanapokuchochea kufanya kile ambacho hutaki kufanya, huishii kushindana na nafsi yako iwapo ufanye au usifanye, badala yake unafanya ule mbadala uliojipangia kufanya.

Kwa njia hii hakuna kitakachokusumbua, kwa sababu utakuwa na mbadala wa kitu cha kufanya wakati wote na badala ya akili yako kupambana na kipi usifanye, itakuwa inafikiria kipi cha kufanya.

Mara zote ifanye akili yako kukaa upande chanya, kukaa upande wa kuona kipi cha kufanya chenye manufaa na siyo kuona kipi cha kuacha ambacho hakina manufaa. Usipange kipi hufanyi na kuishia hapo, bali panga kipi utafanya kama mbadala wake.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog