It is not death that a man should fear, but he should fear never beginning to live. – Marcus Aurelius
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio kwa mwaka huu 2018.
Asubuhi ya leo tutafakari USIOGOPE KIFO, OGOPA KUTOKUISHI…
Kwa kuwa kifo ni fumbo, ambapo hakuna anayejua atakitana nacho lini, kimekuwa hofu kwa wengi.
Wengi hutumia muda wao ambao ni adimu na wa thamani kuhofia kifo.
Lakini kwa hakika kifo hakipaswi kuogopwa wala kuhofia, maana haijalishi unahofu na kuogopa kiasi gani, hilo haliondoi kifo kwenye maisha yako.
Kitu ambacho mtu unapaswa kuogopa ni kutokuanza kuishi.
Wapo watu ambao wapo hapa duniani, lakini hawaishi maisha yao.
Kila siku wapo kwenye maandalizi ya kuanza kuishi, lakini hawaaanzi.
Kila siku wanasema nikimaliza hichi, nikifikia hatua fulani, basi nitaanza maisha yangu.
Ubaya unakuja kwamba wanapomaliza walichokuwa wanasema, au wanapofikia hatua waliyokuwa wanasubiri, wanajikuta kuna vitu vingine zaidi vya kufanya.
Wengine ni wale wanaoishi maisha ya maigizo, kutaka kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, kutaka kuonekana kwa nje hata kama haitoki ndani. Hawa ndiyo wanaahirisha maisha yao ha kukimbizana na maisha ya wengine.
Unachopaswa kuogopa ni kutokuishi maisha yako,
Hivyo kila siku badala ya kujiuliza kifo chako kitakuwaje, hebu jiulize je umeshaanza kuishi maisha yako?
Swali hilo ndiyo sahihi na litakuonesha wapi ulipokwama na hatua zipi za kuchukua.
Hangaika na kile unachoweza kuathiri, kifo huwezi, bali maisha yako unayaweza.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha