Kufanya unachopenda ndiyo njia ya uhakika ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha. Siyo tu kifedha, bali hata ile hali ya kuridhika na unachofanya.
Lakini sasa, wapo wanaofanya kile wanachopenda, lakini hawajapiga hatua kubwa kwenye maisha yao, wako pale pale ambapo wamekuwepo miaka yote.
Kwa sababu hii basi, wengi wamekuwa wakiona kufanya unachopenda siyo njia ya mafanikio, bali bahati na nafasi nyingine ndiyo zinaleta mafanikio.

Lipo tatizo kubwa ambalo nimekuwa naliona kwenye kufanya unachopenda, na tatizo hili ni watu kufikiri kwamba kwa kuwa wanafanya wanachopenda, basi hakuna kuteseka, mambo yatakuwa rahisi na hakutakuwa na vikwazo au changamoto.
Ukweli ni kwamba, kufanya unachopenda, hakuondoi yale mengine yote yanayoendana na kazi au maisha ya kawaida.
Mambo yatakuwa magumu, utahitaji kujitoa kwa kiwango cha juu sana, utahitaji kujisukuma zaidi ya ulivyozoea, na utahitaji kuwa mvumilivu kwa sababu siyo kila kitu kitakuja kwa wakati unaotaka wewe.
Fanya unachopenda lakini usitegemee mambo yawe rahisi, usitegemee kukutana na mteremko, usitegemee kila kitu kitakuja kwa wakati ambao wewe unataka.
Usiingie kwenye tatizo la kufikiri kwamba kufanya unachopenda itakuwa rahisi, chochote kinachokuwa rahisi jua hakina mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Kweli kabisa unachosema, kufanya unachopenda sio kwamba utakuwa umeepukana na ugumu/changamoto. Zipo changamoto ngumu utakutana nazo ila utapaswa kutokata tamaa, bali utapaswa kuendelea kuweka bidii zaidi.
LikeLike