“Worthless people live only to eat and drink; people of worth eat and drink only to live.” -Socrates
Hongera mwamamafanikio kwa siku hii nzuri ya leo.
Hii ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuishi msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambavyo vinatuwezesha kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUISHI ILI ULE…
Kama kinachokunyima usingizi usiku ni utakula nini kesho, basi bado hujaanza kuishi.
Hii ni kwa sababu hata funza na minyoo wanasukumwa na kitu hicho kimoja, wanakula nini.
Hivyo kama na wewe kinachokusumbua ni unakula nini, unajitofautishaje na viumbe hao wengine?
Ndani ya vichwa vyetu tuna kiungo ambacho kina uwezo na nguvu kubwa sana ambayo kama tukiitumia tunaweza kufanya makubwa sana.
Lakini wengi wanachagua kutumia nguvu hiyo kwa ajili ya kula tu.
Hii ni sawa na mtu kununua kompyuta ili kuitumia kusikiliza mziki pekee.
Uwezo mkubwa uliopo ndani ya kompyuta hiyo haupati matumizi.
Sisemi usile, lakini ninachosema, usikubali chakula kiwe ndiyo kitu kinakusukuma kwenye maisha yako. Kuna na ndoto kubwa zinazokusukuma, zinazokunyima usingizi, zinazokufanya ujitoe kwa kiwango cha juu sana.
Ukishakuwa na ndoto za aina hii, hata kula kunakuwa ni usumbufu kwako, unajikuta inabidi ule ili uishi na siyo kuishi ili ule.
Tumia uwezo ulio ndani yako kwa ukamilifu wake, na hilo litakuwezesha kujitofautisha na viumbe wengine.www.kisimachamaarifa.co.tz / kocha
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha