Machi 20 kila mwaka ni siku ya furaha duniani. Katika kipindi hicho shirika la umoja wa mataifa linalojihusisha na maendeleo endelevu huwa linatoa ripoti ya hali ya furaha duniani. Katika ripoti hiyo, wanazipanga nchi kulingana na kiwango cha furaha cha wananchi wake.

Katika orodha ya mwaka 2018, nchi ya Finland ndiyo imekuwa ya kwanza kwa wananchi wake kuwa na furaha zaidi. Kwa nchi yetu Tanzania, tumeshika nafasi ya tatu kutoka mwisho. Katika nchi 156 ambazo zimejumuishwa kwenye ripoti hiyo, sisi tumeshika nafasi ya 153.

Kwa kifupi ni kusema kwamba, kwa ujumla wetu kama nchi hatuna furaha, hatuyafurahii maisha na tupo tupo tu. Watu wengi wametoa maoni yao kuhusu ripoti hii na hali yetu ya furaha. Wapo ambao wanasema siyo kweli na kutoa sababu zao nzuri tu, pia wapo ambao wanasema ni kweli na kueleza sababu nzuri.

Sasa mimi sitakuwa kwenye kundi lolote kati ya hayo mawili. Bali nitakuwa kwenye kundi tofauti ambalo litatuwezesha kupiga hatua. Wanasema tafiti hupingwa kwa tafiti, hivyo mtu akija na ripoti yake ya tafiti ambayo huikubali, inabidi na wewe ufanye utafiti wako kuja na kile ambacho unafikiri ni sahihi.

Mimi ninachokwenda kukushirikisha leo ni sababu 10 kwa nini unapaswa kuwa na furaha hapo ulipo sasa, bila ya kujali una nini au uko wapi.

furaha3

Tunapokosea kwenye furaha.

Tatizo kubwa linalokuja kwenye furaha ni kwamba huwa tunategemea itoke nje. Hivyo tunakazana kutaka kuwaridhisha wengine, tunakazana kupata vitu au kufikia hali fulani tukiamini baada ya kuwa na vitu hivyo tutakuwa na furaha. Lakini tunaweza kuvipata na bado tusiwe na furaha.

Pia changamoto ya kutegemea furaha ya nje ni kwamba, kadiri mtu unavyopata kile unachofikiri kitakupa furaha, ndivyo unavyogundua kwamba unahitaji kupata zaidi na zaidi.

Watu wamekuwa wakifikiria kwamba wakiwa na mafanikio basi watakuwa na furaha. Hivyo wanakazana kupata mafanikio, lakini kadiri wanavyofanikiwa ndivyo wanavyoona kwamba furaha siyo zao la mafanikio. Bali kilicho sahihi ni kwamba ukiwa na furaha ndiyo unafanikiwa. Yaani furaha inatangulia kabla ya mafanikio.

Sasa nikupe zile sababu kumi kwa nini unapaswa kuwa na furaha popote ulipo, bila ya kujali ripoti zinasemaje.

  1. Upo hai.

Kuna watu ambao walikuwa na mipango mikubwa sana ya kuitekeleza siku ya leo, lakini jana waliaga dunia. Wapo watu ambao walikuwa na fedha na kila kitu cha kuwawezesha kuendelea kuwa hai, lakini vyote hivyo havikusaidia, walikufa.

Wapo watu ambao wanazaliwa na kufa hapo hapo, wengine wanaishi miaka michache na kufa, wengine wanaishi mpaka uzeeni ndiyo wanakufa.

Lakini wewe upo hai leo, upo hai sasa, kwa nini usiwe na furaha? Kama umewahi kufikiria kwamba maisha yako hayana maana, tembelea makaburi ya Umma na soma maelezo yaliyoandikwa kwenye makaburi ya wengi, utaona kwa nini maisha yako yana maana kubwa sana na unapaswa kuwa na furaha wakati wote.

  1. Afya yako ni njema kiasi cha kukutosha kuchukua hatua.

Kama unaweza kusoma hapa nilipoandika, basi unapaswa kuwa na furaha kwa sababu afya yako ni njema kiasi cha kukuwezesha kuchukua hatua. Hata kama huna mikono wala miguu, kama akili yako iko sawa, na lazima itakuwa sawa kama unasoma hapa, basi una kila unachohitaji ili kuwa na maisha bora.

Hata kama unajisikia kuumwa kwa kiasi fulani, lakini hujalala chini kabisa, bado afya yako ni njema kiasi cha kukuwezesha kuchukua hatua.

Kama unafikiri kwa namna yoyote ile afya yako siyo njema, jaribu kutembelea hospitali kwenye eneo la wagonjwa mahututi na utaona jinsi ambavyo unachukulia kwa kawaida kitu ambacho wengine wangekipata kwa dakika chache wangefurahi mno.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Craving Mind (Jinsi Tunavyonasa Kwenye Uraibu Na Jinsi Ya Kuvunja Tabia Mbaya.)

  1. Una watu wanaokupenda, jinsi ulivyo.

Nina hakika huishi mwenyewe, una ndugu, jamaa na marafiki, ambao wanakupenda wewe kama ulivyo na ndiyo maana mnaendelea kuwa na mahusiano.

Kuwa na watu ambao wanakupenda wewe kama wewe na siyo wewe kwa sababu una nini au uko wapi, ni kitu ambacho unapaswa kukifurahia sana. Kwa sababu maana ya maisha yetu inatoka kwa wengine, na sisi tupo kwa ajili ya wengine pia.

Hata kama maisha ni magumu kiasi gani, hutakosa watu ambao wanakupenda wewe kama wewe, wajue watu hao na wapende pia.

  1. Unaishi zama bora kabisa kuwahi kutokea duniani.

Kama unasoma hapa, basi una uwezo wa kupata vitu ambavyo miaka 500 iliyopita, raisi au mfalme wa nchi hakuwa na uwezo wa kuvipata. Siyo kwa sababu hakuwa na uwezo wa kulipia kupata, bali havikuwepo kabisa.

Kwa mfano kwa miaka mingi, magonjwa yamekuwa yanawaua watu wengi na hakukuwa na matibabu sahihi. Lakini kwa kipindi cha miaka 100 iliyopita, ugunduzi wa dawa mbalimbali umeweza kurefusha maisha ya wengi.

Kama ungezaliwa miaka 500 iliyopita, labda ungekufa utotoni, au usingeweza kuishi maisha marefu, kwa sababu hali haikuwa bora kama sasa.

  1. Unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya.

Miaka kumi iliyopita, kama ulitaka kuwa msanii, ni mpaka watu fulani wakukubali ndiyo warekodi nyimbo zako, na hata baada ya kurekodi, ilibidi kituo cha redio kikukubali ndiyo nyimbo yako ipigwe. Lakini sasa hivi, kama unataka kuwa msanii, unaweza kurekodi nyimbo yako na kuisambaza mwenyewe kupitia mitandao ya kijamii.

Miaka 10 iliyopita, kama ulitaka kuwa mwandishi, ilibidi watu fulani wakukubali ndiyo wachape kitabu chako. Lakini sasa hivi unaweza kuandika kitabu chako mwenyewe, ukakichapa na kukisambaza kwa njia mbalimbali kupitia mtandao wa intaneti.

Mtandao wa inaneti umerudisha nguvu na mamlaka kwa kila mmoja wetu, hivyo kila mtu sasa anaweza kufanya chochote anachotaka kufanya bila kusubiri mpaka watu fulani wakubali au kuidhinisha. Hili ni jambo la kufurahia sana.

  1. Unaweza kusema hapana kwa usichopenda.

Kuna watu ambao hupendi kukaa nao kwa namna wanavyofanya mambo yao? Una uwezo wa kusema hapana na ukakaa na wale unaowapenda.

Kuna kazi unafanya ambayo huipendi na haiendani na uwezo au vipaji vyako? Una uwezo wa kusema hapana na ukatengeneza kazi inayoendana na vile ulivyo.

Nguvu ya kusema hapana kwenye chochote ambacho hupendi ni nguvu kubwa ambayo ukiitumia vizuri itakusaidia sana,

SOMA; USHAURI; Hatua Za Kuchukua Pale Marafiki Au Watu Wa Karibu Wanakukatisha Tamaa Kwenye Wazo Lako La Biashara.

  1. Wewe siyo mti, una uwezo wa kuondoka popote ulipo.

Mti una kiwango kidogo cha uhuru, kama hali ya pale ulipo siyo nzuri, hauwezi kuondoka hapo na kwenda kwingine. Lakini wewe, una uwezo wa kuondoka popote ulipo, una uwezo wa kubadili mazingira yoyote uliyopo au kuondoka kwenye mazingira hayo kabisa.

Iwe ni aina ya maisha unayoishi, kazi unayofanya, biashara unayofanya, mahusiano uliyonayo, au chochote, kama mambo hayaendi kama unavyotaka, una uwezo wa kubadili chochote unachotaka kubadili.

  1. Kila kitu kinapita.

Ipo tiba moja ya kila kitu kinachotokea au kuendelea kwenye maisha. Tiba hiyo ni muda. Kila kitu kinapita, hakuna chochote kinachodumu milele, hata wewe mwenyewe.

Hivyo unapojikuta kwenye mazingira ambayo ni magumu, unapoona mambo hayaendi, jua kabisa hakuna kinachodumu, kila kitu kinapita. Hata mambo yawe magumu kiasi gani, hayatadumu milele.

  1. Hakuna yeyote anayefanana na wewe kwa kila kitu.

Wewe ni wa kipekee hapa duniani, upo wewe tu kwa jinsi ulivyo. Hakuna mtu mwingine yeyote ambaye ana uwezo, vipaji, na hata tabia na uzoefu ulionao wewe.

Hii ina maana kwamba kuna kitu au vitu ambavyo ni wewe tu unaweza kuvifanya hapa duniani, hakuna mwingine mwenye uwezo wa kufanya. Tumia upekee wako vizuri kuweza kupiga hatua kimaisha.

  1. Changamoto ni sehemu ya maisha.

Kama huna furaha kwa sababu unapitia changamoto fulani kwenye maisha yako, basi jua unajitesa wewe mwenyewe. Changamoto ni sehemu ya maisha na kama unataka maisha ambayo hayana changamoto kabisa, basi jua hakuna maisha ya aina hiyo.

Changamoto ulizonazo sasa, ukizitatua utakutana na changamoto nyingine, na ukitatua hizo zinakuja nyingine. Hautafika wakati na ukajikuta huna changamoto kabisa. Hivyo usiahirishe furaha yako mpaka pale ambapo hutakuwa na changamoto, utauwa umejikwamisha mwenyewe.

Kama tulivyoona kwenye mambo hayo kumi, hakuna hata jambo moja linalotegemea nafasi yako, fedha ulizonazo au hata mali gani unamiliki. Mambo yote hayo kumi yanaanzia ndani yako, na unaweza kuyatumia ukiwa popote pale. Kama tu upo hai, na akili yako ipo sawa, basi dunia ni yako na unapaswa kuwa na furaha kubwa sana kwa sababu una kila aina ya fursa ya kufanya chochote unachotaka kufanya.

Usisubiri mpaka mtu wa nje akuambie kama una furaha au la, hayo ni maamuzi yako binafsi na yafanye kwa usahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog