Chochote unachotaka kwenye maisha yako, utakipata kutoka kwa wengine. Licha ya kwamba mafanikio yako yanahitaji juhudi zako binafsi, lakini huwezi kufanya kila kitu wewe mwenyewe. Unawahitaji watu wengi sana wa kushirikiana na wewe ili uweze kufanikiwa kwenye maisha.
Kama unafanya biashara unahitaji kuwa na wateja wa kununua kile unachouza, unahitaji kuwa na watu wa kukuuzia yale unayohitaji kwenye biashara yako. Muhimu zaidi unahitaji watu wa kushirikiana nao kwenye biashara hiyo kama washirika wa biashara au wasaidizi wako.
Kwenye maisha ya kila siku pia unahitaji kuwa na mahusiano mazuri na wale wanaokuzunguka, ukianza na familia yako kisha kwenda kwenye jamii inayokuzunguka.
Mafanikio yatakuwa na maana gani kwako kama hakuna watu wanaokupenda na kukujali, watu waliopo kwa ajili yako?
Yote haya yanatuonesha ni kwa jinsi gani mahusiano ni eneo muhimu sana la maisha na mafanikio yetu.
Lakini sisi ni binadamu, na ubinadamu una changamoto nyingi, kwa sababu hatukuzaliwa na kitabu cha maelekezo, ya nini unapaswa kufanya na kutokufanya kwenye maisha. Mengi tunayofanya ni kwa sababu tumeona wengine wakifanya, na kwa sehemu kubwa vitu vingi tunafanya kwa kujaribu na siyo kwa kujua na kuwa na uhakika.
Katika kujaribu kwetu, tumekuwa tunawakwaza na hata kuwakosea wengine, kitu ambacho kinaleta doa kwenye mahusiano yetu. Kama doa hilo halitafanyiwa kazi mapema, linapelekea ubora wa mahusiano kushuka na hata kupelekea mahusiano kuvunjika kabisa.
Ili kuimarisha mahusiano yetu, ili kuondoa madoa madogo madogo tunayoweka kwenye mahusiano yetu na wenzetu, yapo maneno manne muhimu sana ya kutumia.
Kwa kutumia maneno haya manne, tutaimarisha mahusiano yetu na wengine na hata kupelekea kufanikiwa kwa viwango vikubwa.
Yafuatayo ni maneno manne muhimu ya kutumia ili kuboresha mahusiano yetu na wengine;
NENO LA KWANZA; NAKUPENDA.
Hakuna neno ambalo watu wanapenda kusikia kama neno NAKUPENDA. Ni neno ambalo linashika hisia za watu, na linapotumika kwa kumaanisha, linatengeneza mahusiano bora sana.
Watu wengi wanawapenda watu, lakini wamekuwa wanaogopa kuwaambia wazi kwa kuona wakiwaambia basi huenda watu hao watawasumbua. Kama unataka mahusiano bora na wengine, kama unataka mafanikio, wapende watu na waambie unawapenda. Waambie wateja wako unawapenda, waambie wazazi wako unawapenda, waambie watoto wako unawapenda, mwambie mwenza wako unampenda.
Unapotumia neno nakupenda, hakikisha unamaanisha kweli, kwa sababu huwezi kudanganya ukabaki salama. Neno nakupenda liendane na matendo. Kama unawaambia wateja wako unawapenda, basi lazima uwauzie kile ambacho kina msaada kwao kweli, uweke mahitaji yao mbele kuliko faida unayotafuta.
SOMA; Sababu Kumi (10) Kwa Nini Unapaswa Kuwa Na Furaha Sasa Hivi, Bila Ya Kujali Upo Wapi Au Una Nini.
NENO LA PILI; SAMAHANI.
Neno la pili muhimu kutumia ni neno SAMAHANI au NIMEKOSA. Sisi ni binadamu, na ubinadamu ni kukosea. Watu hawatakuwa na shida na wewe kwa sababu umekosea, bali wanakuwa na shida na wewe pale unapokosea lakini hutaki kukubali kwamba umekosea.
Ukiwa tayari kukubali makosa yako, watu wanakuelewa, kwa sababu kila mtu kwenye maisha yake anakosea, na wengine wamefanya makosa makubwa kuliko uliyofanya wewe. Hivyo unapofanya makosa, unapokosea, sema SAMAHANI au NIMEKOSEA, watu wataona unajali na hilo litaimarisha mahusiano yenu.
NENO LA TATU; NISAMEHE.
Kukosea na kukubali ni jambo moja, kuomba kusamehewa ni jambo muhimu zaidi. Kuna makosa machache sana ambayo watu hawawezi kuyasamehe kabisa, lakini makosa mengi ambayo unayafanya kwenye maisha yako ya kila siku, watu wapo tayari kukusamehe, kama tu utakuwa tayari kuomba msamaha.
Pale unapokosea, pale unapowaangusha wengine, kubali kosa na omba kusamehewa. Omba ukimaanisha kweli, na jifunze ili usirudie kufanya kosa hilo moja kwa wakati mwingine. Msamaha unaoomba uwe halisi, na uoneshe umejifunza na unabadilika.
SOMA; Mshukuru Sana Yeyote Ambaye Amewahi Kukunyanyasa, Bila Yeye Huenda Usingepiga Hatua.
NENO LA NNE; ASANTE.
Neno hili limekuwa la mwisho katika orodha yetu ya maneno manne, lakini haimaanishi ni la mwisho kwa umuhimu. ASANTE ni neno muhimu sana sana sana. Isipite siku hujatumia neno hilo kwa yeyote anayekuzunguka. Yapo mambo mengi ambayo wale wanaokuzunguka wanafanya kwa ajili yako kila siku, makubwa na madogo, usiache kusema asante kwa watu hao.
Unapowaambia watu asante wanafarijika kwa kuona umetambua mchango wao kwenye maisha yako, na wanapopata nafasi nyingine ya kufanya kitu kwa ajili yako, wanahamasika kufanya, hata kama hakiwanufaishi kabisa. Sema asante na maanisha kweli.
Hayo ndiyo maneno manne muhimu sana rafiki yangu, yatumie mara kwa mara na pale inapohitajika, yatumie kwa kumaanisha na siyo kulaghai, na unapoyatumia, hakikisha ni kwenye wakati sahihi ili yaweze kutengeneza mahusiano yako na wengine.
Nimalizie kwa kuyatumia maneno mawili kati ya haya manne kwako rafiki yangu,
NAKUPENDA sana wewe rafiki yangu, ambaye umekuwa unasoma makala ninazoandika na maarifa mengine ninayotoa. Ni mapenzi yangu kwako ndiyo yananifanya niendelee kuandika kila siku. NAKUPENDA.
ASANTE sana rafiki yangu kwa namna ambavyo umekuwa sehemu ya maisha yako, bila ya wewe kuwa msomaji, uandishi wangu usingekuwa na maana kubwa kwa yeyote. Asante pia kwa sababu kupitia wewe kazi zangu zimewafikia wengi, kwa kuwashirikisha kazi hizo moja kwa moja au kuwaalika wajiunge na huduma ninazotoa, nasema ASANTE SANA.
Kama kwa namna yoyote ile, kupitia uandishi wako au chochote ninachofanya, nimewahi kukuangusha, kuumiza hisia zako au kukukosea, nasema SAMAHANI na nikuombe sana UNISAMEHE.
Ni hayo machache muhimu kwako rafiki yangu, nina imani utayatumia maneno hayo manne katika kuimarisha mahusiano yako ili kuweza kufanikiwa zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.
Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa; www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha
Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha
Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog