Masaa 168 ndiyo masaa ambayo kila mmoja wetu anapewa kwa wiki. Lakini wengi wamekuwa wanapoteza masaa haya wasijue yanaenda wapi. Wanachoshangaa ni wiki imeisha lakini hakuna kikubwa wamefanya.

Kwa mfano mtu anayefanya kazi masaa 10 kwa siku, na siku sita za wiki, kwa juma anakuwa amefanya kazi masaa 60 pekee. Hapo anabaki na masaa zaidi ya 100 ambayo siyo ya kazi moja kwa moja. Ukitoa hata muda wa kulala, labda masaa 8 kwa siku, yanakuwa masaa 56, bado mtu ana masaa zaidi ya 50 kwa wiki, ambayo hajui yanaenda wapi.

Huwa ninashangaa sana pale mtu anaposema hana muda wa kufanya kitu fulani, lakini unamkuta mtu huyo huyo anaangalia TV, anasoma magazeti, yupo kwenye mitandao ya kijamii. Unajiuliza kama kweli mtu huyo anajua anachofanya na maisha yake.

masaa 168

Karibu rafiki kwenye tano za juma, mkusanyiko wa mambo matano muhimu ninayokushirikisha ili uweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako. Nimeanza na msisitizo kwenye muda kwa sababu naamini wiki ndiyo kipimo kizuri sana cha matumizi ya muda wetu. Hivyo kama utahesabu kila saa ya wiki yako uone umeitumiaje, itakuwa rahisi kuona wapi muda wako unapotelea.

Karibu kwenye tano za juma, yasome mambo haya matano, yatafakari kwa kina, angalia namna gani unaweza kuyatumia kwenye maisha yako na hakikisha unafanya kitu ili maisha yako yawe bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUJIUZA VIZURI.

Kila mtu kuna kitu anauza kwenye maisha yake, lakini kabla mtu hajauza chochote, anajiuza yeye kwanza. Na ninaposema kujiuza simaanishi kuuza mwili kama wengi wanavyofikiria, bali kuuza utu na haiba yako, ambavyo mtu inabidi akubaliane navyo kabla hajanunua unachouza.

Umewahi kwenda eneo ambalo kuna wafanyabiashara wawili, wote wanauza kitu cha aina moja, kwa bei moja na huduma zao zinafanana, lakini ukakuta mmoja ana wateja wengi na wengine wanasubiri, wakati mwingine hana mteja hata mmoja?

Waswahili wakiona hivyo wanasema yule mwenye wateja wengi anatumia kizizi au njia fulani za ushirikina. Lakini huo siyo ukweli, ukweli ni kwamba, yule ambaye ana wateja wengi, anaweza kujiuza vizuri kuliko mwenye wateja wachache. Wateja wanajisikia vizuri kununua kwake kuliko kununua kwa wengine.

Napoleon Hill, ambaye tunaweza kumwita baba wa hamasa na mafanikio, aliyeandika kitabu ambacho kimekuwa msingi wa mafanikio ya wengi, THINK AND GROW RICH, alikuwa pia akifundisha kuhusu uuzaji. Na moja ya vitabu vyake ni SELLING YOU, ambapo anafundisha jinsi ya kujiuza wewe mwenyewe kwanza kabla hujauza chochote unachotaka kuuza.

Katika kitabu hichi, Napoleon pamoja na mhariri wa kitabu hicho, wanatupa misingi muhimu sana ya kuzingatia katika kuuza ili kuweza kufanikiwa.

Na kabla hujasema kwamba wewe huuzi, soma sentensi niliyoanza nayo hapo juu, kila mtu anauza. Iwe unauza bidhaa au huduma kama upo kwenye biashara, kama umeajiriwa, unauza muda wako na ujuzi wako kwa aliyekuajiri. Hata katika uongozi, unauza sera zako na maono yako.

Maisha ni kuuza, vingine vyote tunavyofanya ni kusaidia mauzo.

Hivyo kabla hujauza chochote unachouza, lazima ujiuze wewe kwanza. Na katika kujiuza wewe kwanza, Hill anatuambia tufanye yafuatayo;

 1. Kukubali kwamba unauza, na kujua nini hasa unauza.
 2. Kutengeneza haiba ambayo watu watainunua, yaani kukubalika na wengine.
 3. Kutumia vizuri akili yako ya ndani ambayo ina uwezo mkubwa wa kukupa chochote unachotaka.
 4. Kujua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako na kuweka juhudi kukipata.
 5. Kutengeneza ushirikiano mzuri na wengine, ili kunufaika na kile kilichopo ndani yao.
 6. Kuwa na tabia nzuri, inayowafanya watu wakuamini na kukutegemea.
 7. Kuwa na hamasa na kuweza kujithibiti wewe mwenyewe.
 8. Kuweza kutengeneza taswira kwenye akili yako na kuishi taswira hiyo.
 9. Kuwa mwanzishaji na kiongozi kwenye chochote unachofanya.
 10. Kuwa mvumilivu na king’ang’anizi.
 11. Kuuza kile ambacho unauza.

Kama unavyoona mambo hayo 12 hayaangalii kama una elimu kubwa au ndogo, umetoka mazingira mabaya au mazuri na kama una hela au huna. Ni kitu cha kuamua ndani yako, kisha kuchukua hatua. Na siyo kwenye kuuza pekee, bali kwenye kila kitu unachofanya kwenye maisha yako.

#2 MAKALA YA WIKI; MANENO MANNE YA KUSEMA ILI KUFANIKIWA.

Mafanikio kwenye maisha yetu ni kitu ambacho tunatengeneza sisi wenyewe, na tunatengeneza kwa mambo madogo madogo tunayofanya kila siku. Kama ilivyo kwenye kupanda mlima, hutaamka na kujikuta upo kileleni, bali kila hatua moja unayopiga inakusogeza kileleni.

Hivyo ndivyo mambo madogo madogo unayofanya kila siku yanavyokusogeza kwenye mafanikio yako. Na moja ya mambo hayo ni maneno unayotumia kila siku.

Kwenye makala ya wiki hii nilikushirikisha maneno manne muhimu ya kuyasema kila siku ili kuweza kufanikiwa. Ni maneno rahisi na unayoweza kuyatumia kila wakati. Kama hukusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa; Maneno Manne (04) Unayopaswa Kutumia Ili Kutengeneza Mahusiano Bora Na Kufikia Mafanikio Makubwa. (https://amkamtanzania.com/2018/05/25/maneno-manne-04-unayopaswa-kutumia-ili-kutengeneza-mahusiano-bora-na-kufikia-mafanikio-makubwa/)

Nyongeza; juma lililopita nilishirikisha kuhusu mimi kujiondoa kwenye mitandao yote ya kijamii niliyokuwa natumia. Wapo walioniandikia wakitaka kujua wanawezaje na wao kujitoa, nilitoa maelezo ya jinsi unavyoweza kujitoa kwa urahisi, makala iko hapa; Hii Ndiyo Njia Rahisi Ya Kujiondoa Kwenye Mitandao Yote Ya Kijamii Unayotumia. (https://amkamtanzania.com/2018/05/23/hii-ndiyo-njia-rahisi-ya-kujiondoa-kwenye-mitandao-yote-ya-kijamii-unayotumia/)

#3 TUONGEE PESA; CHA KUFANYA KABLA HUJAWEKEZA FEDHA YOYOTE.

Linapokuja swala la fedha, kila mtu huwakwa tamaa pale anaposhawishiwa kwamba anaweza KUPATA FEDHA NYINGI, KWA HARAKA NA BILA YA KUFANYA KAZI. Na matapeli wote wanajua hilo, ndiyo maana ukiangalia utapeli mwingi ambao wengi wanaingizwa, utakuta unahusisha mtu kupata fedha nyingi bila ya kufanya kazi yoyote.

Sasa siku za karibuni kumekuwa na fursa nyingi sana za kuwekeza, ambazo zinawaonesha watu uwezo wa kupata faida kubwa kwa kuweka fedha zao, bila ya wao kufanya kazi kubwa. Na fursa hizi zinatumia teknolojia mpya zinazozaliwa kila siku. Sasa kitu kingine ni kwamba, watu wanapenda vitu vipya, hasa wakiambiwa bado wengi hawajajua, hivyo watakuwa wa kwanza kunufaika.

Katika fursa nyingi watu wanazopewa za kupata fedha nyingi, zipo ambazo ni za kweli, na zipo ambazo ni za utapeli. Lakini kwa wingi na urahisi wa kusambaza taarifa tulionao sasa, ni vigumu sana mtu kujua ipi ya kweli na ipi siyo ya kweli. Kila mtu anaweza kusema chochote kwa sasa, na kila mtu anaweza kutetea chochote kwa mifano ambayo anaweza kuitoa popote.

Sasa ili kukuepusha wewe na utapeli au fursa zisizo za kweli, nakushirikisha kitu kimoja muhimu cha kufanya kabla hujawekeza fedha yako popote. Maana hicho ndiyo kitakachokusaidia.

Kitu ninachotaka ufanye, ni KUWEKEZA NDANI YAKO KWANZA, kabla hujaweka hata senti yako moja popote, wekeza ndani yako kwanza. Jifunze sana, kuwa bora kwanza wewe mwenyewe kabla hujataka kuwekeza sehemu yoyote. Kwa sababu ukishajifunza, ukishakuwa bora, unaweza kufanya maamuzi sahihi ya wapi pa kuwekeza.

Angalizo kuhusu kujifunza, unapaswa kujifunza hasa, na siyo kupitia habari. Kwa hiyo basi, mtu akija kukuambia nina fursa fulani, halafu yeye akawa ndiyo anakufundisha kuhusu fursa hiyo, hapo hujajifunza, umepewa taarifa. Kazi kwako ni kwenda kujifunza sasa, kujifunza hasa na siyo kwa yule aliyekuambia kuhusu fursa, wala kwa wanaofanya, bali kujifunza kupitia misingi ya fursa hiyo.

Usiwe na haraka na wala usiwe na papara, mtu akikuambia fursa hii inakupita, usipoteze muda utakuja kujutia, hapo ndiyo unapaswa kuachana nayo mara moja, wala hata usijifunze. Maana vitu vizuri, vitu halisi huwa haviishi.

Mwisho kabisa, naomba nikusihi hili rafiki yangu, usikazane kukimbiza fursa za kupata fedha za haraka bila ya kazi, bali kazana kuwa mtu mzuri, kuwa mtu bora. Kwa sababu ukishakuwa mtu mzuri, ukishakuwa mtu bora, fedha zitakuja zenyewe. Haijalishi zitakuja kwa njia gani, lakini jua zitakuja. Hivyo kuliko kupoteza muda kukimbizana na fursa usizozielewa, wekeza muda huo kuwa bora.

Kwa mfano, badala ya kukimbizana na cryptocurrency au forex gani itakulipa haraka, kazana kuwa bora kwenye kile unachofanya. Halafu watu watakulipa kulingana na ubora wako, iwe watakulipa kupitia crypocurrency, au njia nyingine, haijalishi, wewe utalipwa kwa ubora wako.

Nisisitize tena rafiki, kazana kuwa bora kwenye chochote unachofanya, na utapata fedha. Usipoteze muda wako kukimbizana na fursa unazoambiwa utapata fedha bila ya kuweka kazi. Chagua kipi unachojali kufanya, chagua kipi uko tayari kuteseka nacho, kisha ingia kwenye mateso, kwa sababu maisha ni mateso na hakuna namna ya kuepuka hilo. Ukiteseka na unachopenda, unachojali, maisha yanakuwa na maana kubwa kwako na kwa wengine pia.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; PERSONAL COACHING.

Wachezaji wote wenye mafanikio makubwa duniani, wanajua na kutumia siri moja muhimu sana. Siri hiyo ni kuwa na mtu wa kuwasimamia. Hata kama wana mafanikio makubwa kiasi gani, wanajua tabia yetu sisi binadamu ni kutengeneza mazoea. Na ndiyo maana wengi huanza kwa hamasa, wanafanikiwa, lakini baadaye wanaanguka, kwa sababu wanatengeneza mazoea na hawapigi hatua tena.

Siri hii ya wachezaji imeanza kutumiwa na watu wanaofanikiwa sana kwenye kazi na biashara zao. Watu wanaofanikiwa, wanajua kuwa na mtu wa kuwasimamia ni muhimu, ili waweze kujituma kwa kiwango cha juu sana, bila ya kujionea huruma au kujidanganya kwamba wamefanya makubwa.

Rafiki yangu, unahitaji kutumia siri hii pia kama unataka kufanikiwa kwa viwango vya juu. Kama unataka kufanya zaidi ya ulivyozoea kufanya, unahitaji kuwa na mtu wa kukusimamia, unahitaji kuwa na kocha.

Na hapo ndipo mimi ninapoingia kwenye maisha yako, kama kocha wako. Kupitia makala ninazokuandikia kila siku, yapo unayojifunza na kupiga hatua. Lakini kama unataka kupiga hatua zaidi, basi unahitaji kunipa nafasi ya kuwa kocha wako moja kwa moja kwa kipindi cha mwezi mmoja tu.

Kwenye programu ya PERSONAL COACHING huwa nafanya kazi na mtu moja kwa moja, kwa kumsimamia kwenye mambo anayotaka kufanya kwa viwango vya juu. Program hii ni kwa kipindi cha mwezi mmoja, ambapo mtu utaweza kufanya makubwa kuliko kipindi kingine cha maisha yako.

Kama unahitaji kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako, basi nakupa nafasi ya kupata COACHING kutoka kwangu. Nafasi za coaching kwa mwezi wa tano zipo, hivyo kama ungependa kupata nafasi hizi, niandikie ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 ujumbe uwe na maneno PERSONAL COACHING.

Karibu sana tufanye kazi pamoja kwa mafanikio makubwa zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; WAACHIE WENGINE HAYO.

“Let others lead small lives, but not you. Let others argue over small things, but not you. Let others cry over small hurts, but not you. Let others leave their future in someone else’s hands, but not you.” – Jim Rohn

Waache wengine waishi maisha madogo, lakini usiwe wewe.

Waache wengine wabishane mambo madogo, lakini usiwe wewe.

Waache wengine walilie maumivu madogo, lakini usiwe wewe.

Waache wengine waweke mustakabali wa maisha yao kwenye mikono ya wengine, lakini usiwe wewe.

Jim Rohn anatufundisha kitu kikubwa sana hapa kuhusu maisha yenye maana, yanapaswa kuwa maisha unayoyamiliki na yasiyozuiliwa na chochote kidogo.

Waachie wengine maisha ya kawaida, kazana kuishi maisha bora, maisha yanayoacha alama kwa kila anayekutana na wewe.

Leo, pangilia masaa 168 yanayokuja kwenye juma la 22 la mwaka huu 2018, halafu unapoanza juma, fuatilia kila saa umefanya nini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji