Rafiki yangu mpendwa,

Leo napenda tukumbushane kanuni za ustaarabu, kitu ambacho kinapungua kwa kasi na kinaathiri sana mahusiano yetu na watu wengine.

Tumekuwa watu wa kusema sana, na maneno yetu ndiyo yamekuwa yanatuingiza kwenye matatizo na changamoto mbalimbali.

Kama kuna hatua moja kubwa unayoweza kuchukua na ikasaidia sana kuyaboresha maisha yako basi ni kudhibiti usemaji wako na kuchagua maneno yako kwa umakini.

Kuna maneno machache sana ambayo ukiyatumia vizuri yatakusaidia sana kwenye maisha yako, yataimarisha mahusiano yako na kukuwezesha kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Baadhi ya maneno hayo ni ASANTE, SAMAHANI, TAFADHALI na KARIBU.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kujifunza kuhusu neno ASANTE, kwenye makala zijazo tutajifunza kuhusu maneno mengine yenye ushawishi kwenye maisha yetu.

say-thank-you

ASANTE.

Asante ni neno la kuwashukuru watu wengine kwa kile ambacho wamefanya kwa ajili yetu.

Ni neno la kujali na kuwaheshimu wengine kwa kile walichofanya kwa ajili yetu.

Neno asante huwa linaleta faraja kwa yule anayelisikia, hasa linapotolewa kwa uhalisia.

Neno asante linawasukuma watu kujituma zaidi, hasa pale wanapotegemea kulipata baada ya kukamilisha kitu fulani.

Ni neno lenye ushawishi mkubwa, ambalo tunapaswa kulitumia sana kwenye maisha yetu.

Neno asante huwa halichoshi, hata mtu alisikie mara ngapi, bado linampa hamasa zaidi kama limetumika kwa usahihi.

SOMA; Maneno Manne (04) Unayopaswa Kutumia Ili Kutengeneza Mahusiano Bora Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

SEMA ASANTE.

Watu wengi wamekuwa na fursa za kutumia neno asante lakini wanazipoteza. Wengine wanapata fursa hizo, wanatumia neno hilo, lakini wanaharibu asante hiyo wanapoanza kutoa maelezo ya ziada.

Hapa chini nimeorodhesha baadhi ya nafasi unazopaswa kuzitumia kusema asante, na pia nimetahadharisha nyakati ambazo unapaswa kuepuka kuongeza neno jingine mbele ya neno asante.

Fursa za kutumia neno asante.

Mtu amekuambia nakupenda, sema asante.

Mtu amekuambia umependeza, sema asante, epuka kuelezea kwamba ni kawaida kwako, inaharibu asante yako.

Mtu amekusaidia kufanya kitu fulani kwenye maisha yako, sema asante.

Mtu amekusaidia kutoka mahali ulipokwama, sema asante.

Mtu amekupa ushauri kwenye jambo lolote unalofanyia kazi kwenye maisha yako, sema asante.

Mtu amekukosoa kwa jambo ulilosema au kufanya, sema asante na epuka kutaka kuonesha kwamba ukosoaji wake siyo sahihi.

Mtu amekupa ushauri ambao hukubaliani nao, sema asante na epuka kubishana naye kwamba ushari wake haufai.

Mtu amekujibu vibaya na kuibua hasira ndani yako, sema asante na epuka kutaka kumjibu zaidi kwa hasira ulizonazo.

Mtu amekutukana au kukupa maneno makali na mabaya, sema asante na usiongeze neno jingine baada ya hapo.

Mtu amewahi kukusaidia huko nyuma lakini hukupata nafasi ya kumshukuru kwa msaada wako, sema asante.

Na wakati wowote mtu anafanya au kusema kitu chochote kwa ajili yako, jibu sahihi kwako kutoa ni asante.

Kama ambavyo umeona hapo juu, unaweza kutumia neno asante kwenye kila eneo la maisha yako, kwa kifupi kila mtu unayekutana naye kwenye maisha yako, una nafasi ya kusema asante kwake, kama utakuwa msikivu na mfuatiliaji wa kile wengine wanafanya au kusema.

Neno asante pia litakuepusha na matatizo makubwa zaidi, mfano mtu anayekujibu vibaya, kukutukana au kukupa maneno makali, unaposema neno asante unammaliza nguvu kabisa. Mtu kama huyo alitegemea ujibu kwa matusi ili ugomvi uendelee, lakini kwa kujibu asante, unakuwa umemaliza ugomvi na utamfanya aumie sana ndani yake. Kwa kifupi hakuna adhabu kubwa unayoweza kumpa mtu anayekusumbua kama kumwambia asante.

Hatua ya kuchukua.

Kuna watu wengi kwenye maisha yako ambao wamewahi kukufanyia mambo mazuri lakini hukupata nafasi ya kuwapa neno asante. Inaweza kuwa ni wazazi wako, walimu wako, mwenza wako, watoto wako na hata mtu mwingine yeyote.

Chukua nafasi ya leo na tafakari watu wote ambao wamewahi kuyagusa sana maisha yako kwa namba moja au nyingine na kisha waambie asante. Unaweza kuwaambia ana kwa ana, unaweza kuwaambia kwa simu, unaweza kuwatumia ujumbe au njia nyingine unayoweza kutumia kuwafikishia ujumbe huo.

Usione aibu wala kujiuliza mwingine atajisikiaje kusikia asante kutoka kwako, fanya hivyo na utawafanya wengine kujisikia vizuri sana. Na kwa kusema asante, utajikuta unafungua fursa nyingi zaidi kwenye maisha yako. Ukiwaambia watu 20 asante leo, kuna wachache ambao watafanya kitu cha kukunufaisha zaidi.

Hivyo huna cha kupoteza kwa kutumia neno asante kwa watu waliokufanyia mazuri huko nyuma na kwa kila anayekufanyia jambo lolote siku zote za maisha yako.

Tumia neno hili kwa kila nafasi unayoipata na litaboresha sana maisha yako.

Nafasi yangu ya kusema asante.

Napenda kuchukua nafasi hii kusema ASANTE kwako msomaji ambaye unasoma kazi zangu. Bila ya wewe uandishi na mafunzo yangu yasingekuwa na maana yoyote. Kazi ninazofanya zinaleta maana kwa sababu wewe msomaji, unajifunza na kuchukua hatua kwenye maisha yako na unapata matokeo mazuri. Nasema ASANTE.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge