Rafiki yangu mpendwa,

Kwa mwandishi, hakuna kitu kinaumiza kama kutumia nguvu na maarifa yako kuandika kitabu au makala nzuri halafu pasiwe na watu wa kusoma kazi yako. Inaumiza na kuchosha sana pale ambapo watu hawaweki uzito kwenye kazi zako kama ambavyo wewe mwandishi unaweza uzito katika kuandaa kazi hizo.

Na kama hiyo haitoshi, wapo wengine ambao watachukua juhudi za makusudi kupinga au kukosoa kazi ambayo umeifanya wewe mwandishi. Na hili linazidi kufanya uandishi kuwa mgumu na unaokatisha tamaa.

Hii ndiyo hali niliyokuwa nayo wakati naanza kazi hii ya uandishi wa makala za kumpa mtu maarifa ya kujikomboa na kuwa na maisha bora miaka 6 iliyopita. Kipindi hicho hapakuwa na wasomaji wengi wa kazi zangu kama walivyo sasa. Na hata wale wachache waliosema, hawakupokea kazi hizi kwa uzito ambao nilitegemea.

Wengi walikuwa na maoni mbalimbali, ikiwepo msisitizo kwamba Watanzania siyo wasomaji wa makala za mafunzo, wanapenda blogu za umbeya na mambo yanayosisimua. Pia wengi walisema watanzania wengi hawana muda wa kusoma makala ndefu, hivyo ukiandika makala ndefu unajisumbua, hawatasoma.

ngazi za mafanikio

Hali hii iliniweka njia panda, na kujiuliza kama kazi hii ya uandishi wa makala za maarifa na hamasa ya kufanikiwa zaidi inaweza kuwa na msaada kwa yeyote.

Baada ya kutafakari kwa kina niliamua kitu kimoja, nitaendelea kuandika na nitamwandikia mtu mmoja tu. Mtu huyo ni mimi mwenyewe. Hivyo nikawa naangalia ni changamoto gani napitia kwenye maisha yangu kila siku, nazitafutia ufumbuzi kisha naandika makala.

Niliacha kuangalia niandike kumfurahisha nani na nikaanza kuangalia niandike kujifunza nini. Haikuchukua muda sana mpango huu ukawa na matokeo bora sana kwa wengi kuliko nilivyotegemea. Wengi wakaanza kuniandikia jinsi ambavyo makala ninazoandika zinagusa maisha yao, zinawatoa kwenye changamoto na zinawawezesha kupiga hatua sana.

Na hapa ndipo nilianza kupata msukumo mkubwa zaidi, msukumo wa kuandika vitabu, msukumo wa kuandaa semina za mitandaoni, msukumo wa kuanzisha huduma za mafunzo zaidi kama KISIMA CHA MAARIFA na msukumo wa kuwa na semina za kukutana moja kwa moja.

Msukumo ambao nimeendelea kuutumia mpaka leo kwenye kazi hii ya uandishi umezidi kuwa mkubwa kadiri siku zinavyokwenda. Kwanza msukumo unaanzia ndani yangu kwa kuwa nimejiwekea uandishi kuwa sehemu ya maisha yangu, kwamba nitaandika kila siku mpaka siku ambayo nitaondoka hapa duniani, na mtu wa kwanza kumwandikia nitakuwa mimi mwenyewe.

Pili msukumo huu unaongezeka zaidi kwa nje kadiri watu wengi wanavyoniandikia na kunipa shuhuda mbalimbali jinsi ambavyo kazi zangu zimebadili maisha yao, na hapa naona jinsi ambavyo nina jukumu kubwa la kuendelea kutoa kazi bora zaidi.

vitabu vya elfu 10

Jinsi ninavyovuka hali ya kukata tamaa.

Kitu kikubwa nilichojifunza kwenye uandishi ni kwamba watu huwa wanakuchukulia wewe mwandishi kwa utofauti mkubwa sana. Mfano watu wengi ambao hawajawahi kukutana na mimi ana kwa ana huwa wanachukulia ni bonge la mtu, mtu mzima sana na ambaye kwa kumwona kwa nje tu basi unajua ana hekima na busara za kutosha. Lakini ninapokutana na watu hao kwa mara ya kwanza, huwa hawaamini kama mimi ndiye ninayetoa kazi hizi, kwa umri na mwonekano wangu wa nje, wanakuwa hawategemei kama ningeweza kufanya yote haya.

Kitu kingine ambacho watu huwa wananichukulia tofauti ni kwenye kukata tamaa. Wengi hufikiri kwa sababu naandika makala na vitabu vya maarifa sahihi na hamasa basi muda wote nakuwa na hamasa ya kufanya kila ninachopanga kufanya.

Lakini huo siyo ukweli, inapokuja kwenye hamasa na kukata tamaa, sina tofauti na binadamu mwingine yeyote. Kuna wakati hamasa inanitoka kabisa, kuna wakati napata ushawishi wa kuacha baadhi ya vitu ninavyofanya.

Lakini ipo njia moja ambayo imekuwa inanipa msukumo zaidi wa kuendelea na kutokukata tamaa.

Njia hiyo ni kusoma maoni mbalimbali ya watu ambao wamenufaika na kazi zangu. Hivyo ninapokwa sina hamasa ya kufanya kitu fulani, au ninapojiambia niache kufanya kitu fulani, naangalia ni watu gani wataathirika sana, na hapo napata msukumo wa kufanya zaidi.

Hivyo huwa naweka maoni na shuhuda zote ambazo watu wamekuwa wananiandikia, jinsi ambavyo kazi zangu zimebadili maisha yao, na huwa nasoma maoni na shuhuda hizo mara kwa mara, hasa pale ninapokuwa nimeishiwa hamasa au kutaka kukata tamaa. Na hili limekuwa linanipa hamasa kubwa sana ya kuendelea.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Hamasa Inayodumu Muda Wote Na Kurudisha Hamasa Iliyopotea.

Mfano wa maoni na shuhuda zinazonipa msukumo zaidi.

Juma lililopita niliandika makala fupi sana kuhusu umuhimu wa kuwashukuru watu kwa yale ambayo wameyafanya kwenye maisha yetu. Na niliandika makala ile kwa kwenda kinyume kabisa na taratibu ambazo nimekuwa natumia kiuandishi. Mfano kichwa cha habari hakikuwa na ahadi yoyote ya kumvutia msomaji kusoma, kilikuwa cha kawaida kabisa; SEMA ASANTE.

SOMA; Sema Asante.

Lakini watu wengi wamesoma makala ile, na kuielewa na hapo hapo kutoa shukrani zao kwangu kwa kazi hizi ninazoendelea kufanya kila siku.

Nimepokea shukrani nyingi mno, hapa nimeambatanisha chache kama mfano, uweze kuona mwenyewe jinsi ambavyo ninatengeneza msukumo wa kuniwezesha kupiga hatua zaidi.

Mifano ya shuhuda na maoni ya wasomaji ambao wamenipa shukrani kwa kazi ninayofanya;

Asant Dr makirita hakika umekuwa mwalimu bora wa maisha yangu ulipo popote mungu akulinde na mabaya yote uzidi kutuelimisha nina imani wewe ni hazina ya TAIFA – Vitalis Issa.

Asante sana Kocha, Maarifa haya ninayopata kwako sijawahi kuyapata kwa mtiririko kama hivi tangu kuzaliwa kwangu ‘over fifty years’. ASANTE SANA – Eng. Enelisa Andengulile Mbwile

Mimi binafsi umekuwa msaada mkubwa katika maisha yangu. Baada ya kukutana na makala zako nipo nilipoona faida ya kutumia simu janja ,kila nikichukua simu ni kutafuta makala zako, nasema tena Ahsante mno. Sehemu ambayo ulikuja kukonga moyo wangu ni kwenye chambuzi za Vitabu, hapo ulinimaliza kabisa, hapo kuna madini ya hatari sana  hiyo ni sehemu ambayo kiukweli imenibadilisha mtazamo wangu sana, na hata jinsi ya kufikiri sasa kumebadilika sana. Ni mengi sana lakini natoa machache hayo. Ahsante sana naamini siku moja utakuja kulipwa zaidi ya hiki unacholipwa sasa. – Onesmo Potino.

Asante sana kocha kwa kunisaidia kuwa mtu wa tofauti na nilivyokuwa nimekuwa mtu bora sana na unaendelea kunisaidia kila siku kuwa bora zaidi. Asante sana kocha wangu. – Oscar Feruzi

Nachukua nafasi hii kusema ASANTE kwako kocha Dr. Amani Makirita Kwa kazi zako za ukocha na uandishi wako na huduma nyingine unatoa. Hakika nimekuwa sehemu ya watu wanaonufaika na huduma zako. Bila ya mafunzo yako maisha yangu yasingekuwa na matokeo ninayoendelea kupata. Nasema ASANTE. – Tumaini Jonas

Asante sana  Kocha kwa yote unayotushirikisha, Asante kwa USHAURI, MAJIBU KWA MASWALA MBALIMBALI, NAKALA ZA AFYA (e.g.Bulletproof diet), TAFAKARI ZA ASUBUHI, NAKALA YA WIKI, UCHAMBUZI WA VITABU, USOMAJI WA VITABU NA ZAWADI YA VITABU, DAKIKA MOJA, COACHING, GAME CHANGERS, N.K. ASANTE SANA – Asubuhi Kasunga

Asante kocha kwa kuwa pamoja kwa kipindi chote hakika nimejifunza mengi na maisha yangu yamebadilika pia asante wanamafanikio wote kwa kuwa pamoja nawapenda sana – Mustapha Kunyaula

Asante Kocha kwa yote makuu usokoma kututendea Watanzania – Raymond Mgeni

Asante sana kocha kwa kila jambo kwangu na kwa watanzania kwa ujumla. Tangu nimekufahamu nimekua wa tofauti sana. Naongea tofauti,  nawaza tofauti, najifunza,   nachukua hatua naanguka nasimama yote ni kwa ajili ya maarifa kutoka kwako na kisima cha maarifa kwa ujumla wake na wewe kutuhimiza kusoma. Ni mengi sana siwezi maliza Mungu akulinde na Kukubariki sana! – Saruni Telele.

Ahsante sana kocha kwa tafakari nzuri sana. Ahsante kwa somo la matumizi ya neno Ahsante. Ahsante sana kwa elimu ya msingi ya fedha kwani somo hili huwa nalirudia kusoma maana ndo ulionitoa kwenye madeni na kuniwezesha kuwa na akiba na kuanza kufanya biashara, Ahsante kocha. – Moses Mahenge.

Asante sana kocha kwa makala nzuri ya kunielimisha, asante sana kwa hapo uliponitoa na sasa nilipo na safari ya mafanikio niliyonayo. – Beatus Rwitana

Rafiki, hii ni sehemu ndogo sana ya maoni na shuhuda nyingi sana ambazo nimekuwa napokea kutoka kwenu kila siku. Kama umeniandikia na hujaona ushuhuda wako hapo siyo kwamba sijaupokea au sijauthamini, bali ni muhimu sana kwako.

Sasa rafiki yangu, pata picha naamka asubuhi, halafu siku hiyo sijisikii kuandika kabisa, halafu napitia maoni kama hayo, nakutana na maneno ambayo mtu ameniandikia jinsi kazi zangu zimebadili maisha yake, nitaachaje kuendelea kuandika? Kwa sababu nisipoandika, maana yake ninawadhulumu wengi ambao wangeweza kunufaika na maarifa niliyonayo. Na hivyo ndivyo ninavyopata msukumo wa kuendelea na kazi hii kila siku, kujipa hamasa zaidi na kutokukata tamaa.

SOMA; SHUHUDA; Watu Hawa Walikuwa Na Wasiwasi Wa Kujiunga Na KISIMA CHA MAARIFA Kama Wewe, Lakini Baada Ya Kujiunga Wanajutia Kuchelewa Kujiunga. Soma Na Uchukue Hatua Leo.

Naomba ushuhuda wako jinsi kazi zangu zimebadili maisha yako.

Rafiki yangu mpendwa, kesho tarehe 28/05 ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu. Nimekuwa natumia siku za kuelekea kwenye siku hiyo kuyatafakari maisha yangu na kila ninachofanya, kuangalia maeneo ya kuboresha zaidi na kuweka sawa vipaumbele vyangu.

Kumekuwa na maazimio ambayo najiwekea kwenye kila mwaka mpya wa maisha yangu, na kwa mwaka ninaokwenda kuanza kesho, nitakushirikisha maazimio makubwa sana ambayo nitahitaji sana msaada wako kuyafikia.

Lakini kabla hujayapata maazimio hayo nitakayokushirikisha kesho, nina ombi moja kwako.

Ninaomba uniandikie ushuhuda wa jinsi ambavyo kazi zangu zimebadili maisha yako. Kwa kifupi nieleze ulipokuwa kabla ya kukutana na kazi zangu na ulipo sasa baada ya kukutana na kazi zangu. Siyo lazima yawe mafanikio makubwa, kitu chochote chanya ulichofanya kwenye maisha yako basi nishirikishe.

Nahitaji sana maoni na ushuhuda wako kwenye maazimio ambayo nakwenda kufanyia kazi kwenye mwaka wangu mpya wa maisha. Hivyo chukua dakika zako chache kunishirikisha jinsi kazi zangu zimebadili maisha yako.

Unaweza kutuma ushuhuda wako kwa njia ya email au njia ya wasap. Kwa email tuma kwenda email amakirita@gmail.com na kwa wasap tuma ujumbe kwenda namba 0717396253.

Nategemea kusikia mambo mazuri kutoka kwenu marafiki zangu, mambo ambayo yatanisukuma zaidi kwenye maazimio makubwa ninayokwenda kufanyia kazi kwenye mwaka mpya wa maisha yangu.

Nimalize kwa kusema asanteni sana marafiki zangu, nyinyi ndiyo mnafanya kazi yangu ya uandishi iwe na maana kubwa zaidi. Na siku zote nitaweka kipaumbele kwenye hili na niwaahidi sitawaangusha kwa namna yoyote ile. Nitaendelea kujisukuma katika kutafuta na kuwashirikisha maarifa bora zaidi ya kutuwezesha kupiga hatua zaidi. Karibuni sana tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA, KISIMA CHA MAARIFA na channel ya TANO ZA JUMA ambapo nawashirikisha chambuzi za kina za vitabu.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

vitabu vya elfu 5