Juma namba 12 linamalizika na mwaka 2018 unazidi kuyoyoma. Kama kuna mambo uliyopanga kufanya mwaka huu 2018 ni vyema uwe tayari umeshaanza, usiendelee kusubiri mpaka ukamilishe kila kitu, la sivyo mwaka utaisha ukiwa hujaanza.

Karibu tena kwenye #TANO ZA JUMA ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu niliyojifunza na kukutana nayo kwa juma zima, ambayo kwa kujifunza unaweza kuchukua hatua na maisha yako yakawa bora zaidi.

vitabu softcopy

Katika juma hili la 12 linaloisha, nimekutayarishia mambo haya matano muhimu sana ya kujifunza.

#1 KITABU NILICHOSOMA; HOW YOUR CHILD LEARN BEST.

Lipo kosa moja kubwa sana ambalo wazazi na walimu tumekuwa tunafanya kwa watoto wetu. Tumekuwa tunawafanya watoto wote kama vile wanafanana, yaani wana akili ya aina moja na njia moja pekee ya kujifunza inawafaa.

Kwa njia hii tumekuwa tunatengeneza makundi ya watoto wenye akili kwa sababu wanafaulu vizuri mitihani na watoto wasio na akili au wenye uelewa hafifu kwa sababu wanafeli mitihani.

Lakini tafiti za kisayansi na zinazotumia kifaa kinachoweza kuona ubongo unavyofanya kazi, zinatuonesha kwamba akili za watu zinatofautiana na njia iliyozoeleka kufundisha kwenye mfumo wa elimu siyo njia pekee.

Zipo aina nane za akili na njia kuu tatu za kujifunza. Kama wazazi na walimu tutajua aina ya akili ambayo watoto wetu wanayo, na tukajua njia bora kwao kujifunza, itawaandaa watoto wetu kuwa washindi kwa namna yao binafsi. Hakutakuwa na mtoto wa kushindwa au kufeli, kwa sababu anachofundishwa kinakuwa kinaendana na yeye.

Zifuatazo ni aina nane za akili, kwa maelezo rahisi kueleweka;

Aina ya kwanza; akili ya lugha, hii ni akili ambayo inahamasika kwa njia ya sauti na maneno. Akili hii hufanya kazi vizuri kwenye mambo yaliyopangiliwa na ni nzuri kwenye kukariri.

Aina ya pili; akili ya mantiki na hesabu, hii ni akili ambayo inaweza kufikiri mambo kwa kina na kuyachambua pia.

Aina ya tatu; akili ya muziki, hii ni akili inayofanya kazi vizuri kwa njia ya sauti, na kuweka kumbukumbu vizuri kupitia kusikia.

Aina ya nne; akili ya uoni, hii ni akili inayofanya kazi vizuri kwa kuona vitu, picha na hata kutengeneza taswira ya kitu. Akili hii inaweka kumbukumbu vizuri kwa kuona kitu.

Aina ya tano; akili ya mwili na kushika, hii ni akili ambayo inahusisha vitu vinavyoshikika. Mtu anaweka kumbukumbu vizuri kwa kushika na kujihusisha moja kwa moja na kitu.

Aina ya sita; akili ya mahusiano na wengine, hii ni akili ambayo inamwezesha mtu kujua hisia za wengine, mahitaji yao na jinsi ya kujenga mahusiano bora na wengine.

Aina ya saba; akili ya mahusiano binafsi, hii ni akili ambayo inamwezesha mtu kujijua yeye mwenyewe, kujua hisia zake, kujua uwezo wake na hata kujiamini.

Aina ya nane; akili ya asili, hii ni akili inayoelewa mazingira ya asili na vitu vyake kama miti na wanyama.

Ukiangalia akili hizo nane, kila mtu anazo kwa kiasi fulani, lakini kuna ile ambayo inatawala zaidi kwa mtu fulani. Akili inayopimwa kwenye mfumo wa elimu ni ya lugha na mantiki na hesabu. Hivyo wale watoto wote ambao hawapo vizuri kwenye aina hizo za akili, wataambiwa hawana akili wakati kumbe wanaweza kuwa wazuri sana kwenye mahusiano binafsi na mahusiano na wengine, au wakawa vizuri kwenye vitu vya kufanya, muziki na hata mambo ya asili.

Aina tatu za kujifunza.

Zipo aina kuu tatu za kujifunza;

Aina ya kwanza ni kusikia na mpangilio, hii ni aina ambayo mtu anakaa na kusikiliza kile anachofundishwa kisha kukariri na kukariri.

Aina ya pili ni kuona na taswira, hii ni aina ambayo mtu anajifunza kwa kuona kitu au kujenga taswira ya kitu anachoambiwa.

Aina ya tatu; kushika na kufanya, hii ni aina ambayo mtu anajifunza kwa kushika na kufanya, na hapo anaelewa vizuri kupitia kile alichofanya.

Na hapo pia, utaona mfumo wa elimu unatumia njia moja tu, ya kusikia, ambapo mwalimu anafundisha na watoto wanatakiwa kusikiliza kwa makini, kujisomea, kukariri na kufaulu mtihani. Njia hii inawafaa wale wenye akili za lugha na hesabu. Ila wenye akili nyingine wanahitaji kuona, kushika na kufanya.

Hivyo ili kuwasaidia watoto waweze kujua na kutumia uwezo mkubwa ulipo ndani yao, tunapaswa kujua aina ya akili ambayo ina nguvu zaidi kwao, na kujua njia ipi bora kwao kujifunza.

Hili ni jukumu la kila mzazi kwa sababu mfumo wa elimu hauna muda na rasilimali za kuweza kumpa kila mtoto kile kinachomfaa, unachofanya ni kuchukua njia moja inayowafaa wengi hata kama inawatenga wengine.

#2 MAKALA YA WIKI; SABABU KUMI KWA NINI UNAPASWA KUWA NA FURAHA.

Dunia tunayoishi sasa inashangaza sana, ni moja ya nyakati bora kabisa kuwa hai, lakini ndiyo wakati ambao wengi mno wamevurugwa. Tunayafanya maisha kuwa magumu kuliko yanavyopaswa kuwa. Na cha kushangaza zaidi, tunasubiri mpaka mtu mwingine atuambie kama una furaha au la. Au tunasubiri mpaka watu wengine watupe furaha, au kusubiri mpaka tupate kitu fulani ndiyo tuwe na furaha.

Yote hayo yamechangia watu wengi kuwa na maisha ya hovyo, yasiyo na furaha na ya kujitesa. Wakati kila mtu ana vitu vingi ambavyo akiweza kuviona na kuvifanyia kazi, anapaswa kuwa na furaha kubwa kwenye maisha yake.

Kwenye makala ya wiki hii, nimekupa sababu 10 kwa nini unapaswa kuwa na furaha, bila ya kujali upo wapi au una nini. Fungua hapa kusoma makala hii na uanze kuwa na furaha sasa; Sababu Kumi (10) Kwa Nini Unapaswa Kuwa Na Furaha Sasa Hivi, Bila Ya Kujali Upo Wapi Au Una Nini. (https://amkamtanzania.com/2018/03/23/sababu-kumi-10-kwa-nini-unapaswa-kuwa-na-furaha-sasa-hivi-bila-ya-kujali-upo-wapi-au-una-nini/)

#3 NILICHOKIONA JUMA HILI; #DELETEFACEBOOK.

Juma hili zimeibuka taarifa kwamba mtandao mkubwa kabisa wa kijamii, Facebook umekuwa ukitumia vibaya taarifa za watumiaji wa mtandao huo. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa ni kwamba mwaka 2014 mtandao huu uliruhusu taasisi ya Cambridge Analyitica kukusanya taarifa za watumiaji wa mtandao wa facebook kwa nia ya kujifunza. Lakini baadaye taasisi hiyo iliweza kupata data za zaidi ya watumiaji milioni 50 wa mtandao huo wanaoishi nchini Marekani.

Kibaya zaidi ni kwamba taasisi hiyo iliuza taarifa hizi kwa timu ya kampeni za uraisi uliofanyika mwaka 2016 nchini Marekani. Inaonekana taarifa hizo zilisaidia timu ya kampeni ya Raisi Donald Trump kuweza kuwatumia taarifa fulani watumiaji wa mtandao huu ambazo zilishawishi yeye ashinde.

Kumekuwa na malalamiko ya wengi kuhusu mtandao huu na namna unavyozidi kukua na kuwa hatari. Kwa mfano katika kipindi hicho hicho cha uchaguzi, ilionekana habari za uongo zilikuwa nyingi na zilisambaa kwa kasi sana kupitia mtandao huu.

Pia mtandao huu hauna bidhaa yoyote bali watumiaji wake. Hivyo njia ya kutengeneza kipato kwa mtandao huu wa kijamii, ni kuuza taarifa za watumiaji wake kwa watangazaji mbalimbali. Kwa mfano kama kuna kitu chako unachotaka kutangaza, ukitumia facebook inaweza kukuchagulia wale unaowalenga tu ndiyo waone tangazo lako. Mfano unaweza kuchagua tangazo lako liwafikie wanawake, wenye umri kati ya miaka 25 mpaka 35, wanaoishi Dar na wenye kupenda biashara na ujasiriamali, facebook itakupa watu hao na utawafikia.

Unachopaswa kuelewa kama mtumiaji wa mitandao ya kijamii ni kwamba hakuna usalama kwenye mitandao hii. Mtu yeyote anaweza kujua chochote kuhusu wewe na kutumia taarifa ulizoweka kufanya kile anachotaka. Hivyo kuwa makini ni aina gani ya taarifa unatoa kupitia mitandao hii, na kama hakuna manufaa unayopata kwenye mitandao hii, unaishia tu kuangalia nani kafanya nini, unaweza kuungana na kampeni ya #DeleteFacebook na ukapata muda wa kufanya mambo muhimu kwenye maisha yako.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; COACHING PROGRAM.

Kila mwezi huwa natoa nafasi ya kufanya kazi na mtu mmoja mmoja kupitia coaching program. Katika program hii ninamsaidia mtu kupiga hatua ambayo amekuwa anatamani kupiga lakini anashindwa kujisimamia au kujipa nidhamu ya kufanya.

Iwe ni mtu anayetaka kuanza kuandika, kufanya biashara, kukuza biashara, kuboresha mahusiano na hata kujifunza tabia yoyote mpya, tunafanya kazi pamoja.

Mfumo ninaotumia ni kuweka malengo na mipango kwa pamoja, kukupa kifaa cha kupima hatua unazochukua kila siku, kila siku unatuma hatua unazopiga na kila wiki tunakuwa na mazungumzo ya kuangalia wiki imeendaje na hatua za kuchukua kwa wiki inayofuata.

Kwa mwezi wa nne unaokwenda kuanza zimebaki nafasi nne za coaching program, hivyo kama unataka kupata nafasi hiyo tuwasiliane kwa wasap namba 0717 396 253.

Angalizo; ada ya coaching program ni tsh laki moja kwa mwezi, na unahitaji kujua nini unataka ndiyo tufanye program hiyo. kama bado hujaamua nini unataka kwenye maisha yako, program hii haitakuwa na msaada kwako.

Karibu sana kuwahi nafasi hizi za kipekee za kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; USITAKE USHICHOKUWA NACHO.

“No person has the power to have everything they want, but it is in their power not to want what they don’t have, and to cheerfully put to good use what they do have.” – Seneca

Seneca, aliyekuwa mwanafalsafa wa ustoa anatuambia kwamba hakuna mwenye nguvu ya kupata kila anachotaka, lakini kila mtu ana nguvu ya kutokutaka kile ambacho hana, na kuchagua kutumia vizuri kile ambacho anacho.

Hebu tafakari hili kwa makini rafiki, acha kufikiria huna nini, na angalia kila ulichonacho na ukitumie vizuri. Acha kufikiria huna mtaji wa kuanza biashara na angalia nguvu, muda, utaalamu na uzoefu ulionao ambao unaweza kuutumia kuongeza thamani kwa wengine.

Acha kuangalia kile ambacho huna, na angalia ulichonacho na unawezaje kukitumia kupata kile unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji