Kuna vitu ambavyo watu tumekuwa tunafanya, ambavyo vimeshakuwa tabia kwetu, lakini havitupi matokeo ambayo tumekuwa tunayategemea. Lakini kwa kuwa vitu hivyo vimeshakuwa tabia, inakuwa vigumu kwetu kuacha kuvifanya na kwa kuwa tunaendelea kufanya, tunaendelea kupata matokeo yale yale.

Iko hivi rafiki, kipato utakachopata kesho, hakitakuwa tofauti na kile ulichopata jana na unachopata leo, kama unaendelea kufanya kile ambacho umekuwa unafanya. Haihitaji shahada kujua hilo, lakini sasa mbona watu wanaendelea kufanya?

Mambo ya Kawaida

Kwa sababu hatua ngumu kabisa kwenye maisha, ni kuacha kufanya kile ambacho tayari mtu umeshazoea kufanya. Kwanza ugumu unaanzia kwako binafsi, kwa sababu kwa kuacha kufanya kile ulichozoea kufanya unajiona kama siyo wewe. Na ugumu unakuwa mkubwa zaidi kutoka kwa wale wanaokuzunguka, wale waliokwisha zoea kwamba huwa unafanya nao kile unachotaka kuacha.

SOMA; UKURASA WA 1103; Tatizo Lako Halihitaji Kutumia Chochote…

Katika hali kama hii, kujaribu kuacha tabia kistaarabu na kwa kujionea huruma, inakuwa njia ya kushindwa. Kujaribu kuacha kidogo kidogo inakuchukua muda na huenda usiweze kuacha kabisa.

Hapo sasa ndiyo unahitaji kuacha tabia mbaya kishujaa na kikatili, kwa njia hii unajiambia wewe mwenyewe na dunia nzima kwamba hutafanya tena kile ulichozoea kufanya. Unasema hutafanya tena na hata ukijipa au ukipewa sababu nzuri kiasi gani kwamba siyo vibaya kufanya kidogo, hufanyi.

Unafanya maamuzi kwamba hutafanya tena, na hiyo inakuwa imetoka, hufanyi tena kweli.

Hili ni zoezi gumu, lakini ambalo linawezekana na lina manufaa makubwa kwako. Na ili likamilike vizuri, unahitaji kuwa na kitu mbadala cha kufanya, kuchukua nafasi ya kile ambacho umeshazoea kufanya. Ukiacha tabia fulani lakini ukawa na uwazi kwenye nafasi ya tabia hiyo, ni rahisi kuirudia. Lakini kwenye nafasi ya tabia hiyo ukaweka kitu kingine, kitakuondoa haraka kwenye mazoea ambayo ulikuwa umeshayajenga.

Pale unaposhawishika kufanya kile ulichozoea kufanya, unafanya kile kipya ambacho umechagua kufanya. Hivyo unapunguza ule msuguano wa nifanye au nisifanye, msuguano ambao huwa haumwachi yeyote salama.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog