Linapokuja swala la fedha, hakuna tofauti sana na jeshi. Wewe ndiye unakuwa jenerali wa jeshi na fedha ulizonazo ndiyo wanajeshi wako.

Sasa ili kushinda vita yoyote ile, lazima jenerali wa jeshi awe na mbinu za kumwezesha kujenga jeshi lake vizuri. Lazima pia awe na nidhamu ya hali ya juu katika kujenga jeshi lake.

Jua

Kwenye jeshi la fedha, unapowekeza fedha maana yake unakuza jeshi lako zaidi, unakuwa na wanajeshi wengi na hivyo kuwa na nguvu ya kushinda vita. Fedha unayowekeza inazalisha fedha zaidi, hivyo unakuwa na wanajeshi wengi zaidi.

Unapotumia fedha maana yake unapoteza wanajeshi wako, unapunguza nguvu ya jeshi lako, unalifanya jeshi kuwa dhaifu na lisiloweza kupambana na maadui mbalimbali.

SOMA; DARASA LA JUMAPILI; UWEKEZAJI KWENYE SOKO LA HISA

Unapokopa fedha sasa, hapo unatumia jeshi lako kujenga jeshi la wengine. Maana yake unawapa wengine fedha zaidi ya zile walizokupa, hivyo siyo tu unapoteza jeshi, bali unajenga jeshi la wengine, wewe unakuwa dhaifu huku wengine wakiwa imara zaidi.

Hivyo kama unataka kuwa jenerali mzuri, kama unataka kuwa na wanajeshi wa kupambana na changamoto za maisha, kazi yako kubwa ni kuongeza wanajeshi wako kupitia kuongeza kipato na kuwekeza. Dhibiti matumizi yako na epuka kukopa kama utalazimika kulipa wewe mwenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog