Tumezoea kusikia utapiamlo wa mwili, ambao huwa unasababishwa na kukosa virutubisho muhimu kwenye chakula, au kupata kwa wingi aina fulani ya virutubisho. Kwa mfano kama mtu atakosa protini kwenye chakula chake, hasa watoto, anapata kwashiakoo, huu ni utapiamlo. Lakini pia kama mtu atakula wanga (sukari) kwa wingi, mwili wake utapata uzito uliopitiliza, huo nao ni utapiamlo.

Lisha Akili

Sasa utapiamlo upo pia kwenye akili, lakini hapa haihuishi chakula, bali inahusisha maarifa na taarifa. Kama akili yako haipati maarifa sahihi, inakuwa na utapiamlo, inashindwa kufikiri kwa kina na kuishia kufanya mambo kwa mazoea. Uwezo mkubwa wa akili hiyo unakuwa hauna mchango kwa mtu kuweza kupiga hatua.

SOMA; UKURASA WA 954; Ubobezi Huu Hautakusaidia Lolote….

Pia akili inapopata taarifa zisizo sahihi kwa wingi, mfano kupata kila aina ya habari, kusoma vitu hasi na visivyo na mchango, inapata utapiamlo. Taarifa hizo zisizo muhimu zinaweza kuonekana ni nzuri lakini kadiri muda unavyokwenda zinaharibu akili yako, zinabadili mtazamo wako na hata kuondoa hamasa yako.

Kama ambavyo tunailinda miili yetu dhidi ya utapiamlo, hasa ule utapiamlo wa uzito kupitiliza, ndivyo tunavyopaswa kuzilinda akili zetu dhidi ya utapiamlo wa taarifa, hasa zile habari hasi na zisizo na maana.

Chambua kwa makini kila unachoruhusu kiingie kwenye akili yako, na ona kina manufaa gani kwa sasa na hata baadaye. Kama hakuna manufaa mazuri, achana nacho mara moja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog