Fedha ni fedha, ni kipande cha karatasi, au chuma, au tarakimu kwenye kompyuta ambayo imepewa thamani na wote tukakubaliana nayo. Nje ya hapo, fedha haina hisia yoyote ile.
Lakini sasa, mtu akiokota, kupewa au kushinda zawadi ya fedha, ataitumia hovyo kuliko fedha ambayo ameitafuta kwa nguvu na jasho!
Mtu akiwa hana fedha anakuwa na mawazo mazuri kweli, lakini akipata fedha mawazo yote mazuri yanapotea, anazitumia mpaka zinaisha na zikishaisha ndiyo anakumbuka mawazo aliyokuwa nayo.

Mtu akiwa na fedha, kila mtu anajua kwamba ana fedha, na akiwa hana fedha basi kila mtu anajua hana fedha. Je hizi fedha zina harufu au alama gani?
Utagundua kwenye mambo yote hayo, namna watu wanavyochukulia fedha wanatofautiana, lakini kwa wengi ni kwa njia ya hisia ambapo itakuwa rahisi kuona kwamba fedha zina hisia.
Lakini ukweli ni kwamba, fedha hazina hisia, ni kipande cha karatasi, chuma au tarakimu, zaidi ya hapo, sisi wenyewe ndiyo tunazipa hisia.
SOMA; Tabia Moja Inayowaingiza Watu Wengi Kwenye Madeni Ya Kifedha, Na Namna Ya Kuiepuka.
Ukitaka kuwa na nidhamu ya fedha, ukitaka kupiga hatua kwenye maisha, ni lazima udhibiti hisia zako juu ya fedha.
Hatua ya kwanza kupiga ni kuipa fedha heshima yake kama fedha, kwamba kila fedha ni muhimu, iwe umeokota, umepewa au umeshinda, ikishakuwa fedha basi ni muhimu na itumike kwa mipango mizuri ambayo umekuwa nayo.
Kingine ni kudhibiti tabia zako wakati unapokuwa na fedha, usikimbilie kununua kitu kwa sababu umekiona au kwa sababu una fedha, kama hujawahi kupata wazo la kununua kitu hicho ukiwa huna fedha, basi usinunue ukiwa na fedha, ni hisia zako zinakusukuma na siyo uhitaji.
Kazana kuondoa kila aina ya hisia unayoweka kwenye fedha na fedha itatulia kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog