Hivi unajua kwamba kila mtu anapaswa kupata kiasi chochote cha fedha anachotaka kupata?

Hivi unajua kwamba dunia ina fedha nyingi kiasi cha kumwezesha kila mtu kuwa tajiri?

Hivi unajua kwamba kiasi cha fedha duniani kimekuwa kinaongezeka kila mwaka na matajiri wamekuwa wanazidi kuwa wengi?

Unaweza kuwa unayajua haya, lakini kwa ndani unajiambia fedha siyo muhimu, au hatuwezi kuwa wote matajiri, au masikini hawatakosekana.

Na kwa kauli kama hizo, wengi wanaishia kubaki masikini, huku wachache wakiendelea kuwa na fedha nyingi.

Na hata wale ambao wanasema fedha siyo muhimu, ndiyo ambao usiku hawalali, wakifikiria kesho itakwendaje, wakifikiria kesho watakula nini.

Kuna kauli nyingi ambazo tumekaririshwa kuhusu fedha, ambazo zimekuwa zinatuzuia kupata fedha nyingi. Kauli kama hizo nilizokushirikisha hapo juu, zipo kwa kila mtu.

88c15-4326597376_a74a527ef3_z

Na wapo watu wanaochukulia kama ni tabia mbaya mtu anapozungumzia mambo ya fedha, lakini tunajua namna ambavyo maisha ya sasa hayawezi kwenda bila ya fedha.

Lakini pia lipo kundi la watu ambao wanafanya kazi kweli, wanajituma hasa, wanaamka asubuhi na kuchelewa kulala, wanafanya kazi kwa masaa ya ziada, lakini hawaondoki kwenye umasikini, fedha wanazopata ni za kula na hivyo wanaendelea kufanyia kazi matumbo yao na familia zao.

Ipo kauli moja ambayo watu hawa wanaojituma sana, kwa hakika si wavivu, wanapenda kuitumia, ambayo inawazuia wasipate zile fedha wanazostahili kupata. Yaani fedha wanazopata, haziendani na kazi wanayofanya, elimu waliyonayo na hata uzoefu ambao tayari wanao.

Kauli hii imekuwa kikwazo kwa wengi, lakini hakuna mtu yeyote amewahi kuwaambia watu kauli hii ni mbaya. Kwa sababu mtu anakua akisikia wazazi wake wakitumia kauli hiyo, akiwa shuleni anafundishwa kwa kauli hiyo na hata anapoenda kwenye kazi au biashara, kauli pekee inayotumika ni hiyo.

Kauli hiyo ambayo imekuwa inakutenganisha wewe na fedha zako ni hii; NAENDA KUTAFUTA FEDHA. Unaweza kuona jinsi ilivyo kauli rahisi, kauli ya kawaida, kauli isiyoonekana kuwa na madhara yoyote kwa nje, lakini kwa ndani, kwenye akili na fikra ni kauli sumu mno. Na hapa nitakuonesha kwa nini pia nitakupa kauli mbadala ya kutumia kuanzia sasa.

Kauli ya NAENDA KUTAFUTA FEDHA, au NATAFUTA FEDHA, ni kauli sumu na inayowafanya wengi wasipate fedha.

Hii ni kwa sababu, kitu pekee ambacho kinatafutwa ni kitu kilichopotea, au kitu ambacho ni adimu na kigumu kupatikana. Sasa kama umepoteza fedha, unaweza kuzitafuta, lakini pale unapozungumzia kipato chako, kutumia kauli ya kutafuta, unajizuia kupata fedha. Kwa sababu hakuna fedha umepoteza, sasa unatafuta nini?

Huwezi kutafuta ambacho hujapoteza, hivyo kujiambia unatafuta fedha, unajidanganya, kwa sababu hakuna fedha ambazo umepoteza. Ukiwa na mtazamo wa kutafuta fedha, unajua kabisa kwamba kinachotafutwa kinaweza kisipatikane, hivyo kama hutapata, utajiambia ndiyo maana tunatafuta, haipatikani na utakubali haraka.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Harmonic Wealth (Siri Ya Kuvuta Maisha Unayoyataka).

Kwa upande wa pili wa kutafuta, unatafuta kile ambacho ni adimu au kigumu kupatikana. Hivyo kama unatafuta fedha, maana yake unajiambia fedha ni adimu na ngumu kupatikana. Hili pia ni kikwazo kwa sababu ukishajiambia fedha ni adimu, huwezi kuipata ya kutosha, utaipata kwa kiwango kile kile ambacho unaamini kinapatikana. Na hata utakapokosa, utajiambia hata hivyo ni adimu, nitaendelea kutafuta tena.

Ukiamini fedha ni ngumu kupatikana na ndiyo maana unahitaji kuitafuta sana, utaridhika haraka pale unapokwama na kuona kwamba ni ngumu, na kuendelea kutafuta kwa njia nyingine. Simaanishi kwamba fedha inapatikana kirahisi tu, lakini unapokuwa na mtazamo kwamba ni ngumu kuipata, hayo ndiyo matokeo ambayo utayapata.

Kauli ya KUTAFUTA FEDHA imewafanya wengi kufanya mambo ya hivyo kabisa kufikiri yatawapatia fedha.

Wanaotafuta fedha ndiyo utawakuta wakicheza kamari na michezo ya kubahatisha, wakiamini wataipata fedha, na huwa hawaipati, au wakiipata kidogo wanairudisha tena huko huko.

Wanaotafuta fedha ndiyo wanaofikiria kama wazazi wao wangekuwa matajiri na wakarithi mali basi maisha yao yangekuwa mazuri na siyo magumu. Kwa sababu wanafikiri kupata fedha kwa njia ya urithi.

Wanaotafuta fedha ndiyo wanaotapeli, wanaoiba, wanaodhulumu, wanaopokea rushwa na hata kufanya mambo maovu ili tu waipate fedha, na wanaipata lakini inaishia kuwatesa maisha yao yote.

Wanaotafuta fedha ni wale ambao wamekata tamaa na maisha, ambao wakisikia wengine wanaongelea utajiri wanachukia, wakiwaona matajiri wanawaona kama watu wabaya, na kinachowaweka hapa duniani ni watakula nini kesho.

Hao ndiyo watu WANAOTAFUTA FEDHA, nina hakika wewe rafiki yangu hutaki kuwa sehemu ya watu hawa, na ndiyo maana mpaka sasa unaendelea kusoma hapa. Na kama nilivyokuahidi, nitakupa kauli mbadala ya kutumia, ambayo itakuwezesha wewe kupata zile fedha unazostahili kupata.

Kauli sahihi kwako kutumia kifedha ili upate kiasi cha fedha unachostahili kupata.

Tumeshaona ya kwamba kauli NATAFUTA FEDHA ni kauli sumu, kauli inayowatenganisha wengi na fedha zao.

Swali ambalo utakuwa unajiuliza mpaka sasa ni je kauli ipi sahihi ya kutumia badala ya NATAFUTA FEDHA? Mbona kutafuta fedha ni kitu ambacho kimezoeleka na tunatumia kauli hiyo kila siku?

Jibu lipo rafiki yangu, ipo kauli ambayo kwa kuanza kuitumia na kuiishi, nusu ya changamoto zako kifedha zinapotea kabisa. Kauli hii inakuondoa kwenye uhaba wa fedha na kukufikisha kwenye utele wa fedha, ambao unakupa hamasa ya kupiga hatua zaidi.

Kauli sahihi kwako kutumia kifedha ni NAKUSANYA FEDHA. Usiseme unaenda kutafuta fedha, sema unaenda KUKUSANYA FEDHA. Kwa sababu fedha zimetapakaa duniani, wajibu wako ni kuzikusanya tu.

Sasa usije ukanielewa vibaya, ukasema nakuambia fedha ni rahisi kupata, unachotaka ni kukusanya tu.

Ninachokuambia, ninachotaka uelewe na kuanza kukiishi utakapomaliza kusoma makala hii ni hichi; fedha unazohitaji wewe zipo kwa watu wengine. Watu wengine ndiyo wenye fedha zako wewe, sasa unachohitaji wewe ni kuzikusanya kutoka kwao, kuwashawishi wao wakupe fedha ambazo wao wanazo.

SOMA; Kama Umewahi Kucheza Kamari Au Bahati Nasibu Nina Maneno Makali Kwako, Yasome Na Yatakusaidia.

Na njia pekee ya kufanya hivi, ni kuwapa kile ambacho wanakitaka hasa, kuwapa kitu ambacho kinaongeza thamani kwenye maisha yako, kuwapa kitu ambacho kinatatua changamoto zao, kuwapa kitu ambacho wamekuwa wanakitafuta mno na wanapokiona wanafurahi na kuwa tayari kukigharamia.

Hiyo ndiyo namna ambayo unakusanya fedha, kwa njia hii hukazani kutafuta fedha, fedha haiwi kitu kigumu kupata, fedha haiwi adimu, bali fedha inakuwepo na kazi yako ni kuja na njia ya kuikusanya.

Anza sasa kukusanya fedha zako, ambazo kwa sasa zipo kwenye mikono ya wengine. Anza sasa kufikiria kila aina ya thamani unayoweza kutoa, kila aina ya matatizo unayoweza kutatua, kila aina ya uhitaji unaoweza kuwatimizia wengine. Ukiweza haya, hutakuwa na haja ya kufikiria unapata wapi fedha, fedha zitakuwa zinatiririka kuja kwako.

Kusanya fedha ambazo zimezagaa kila mahali, unapoona watu wanalalamika, ona fedha zimezagaa, unapoona watu wana matatizo, ona fedha zimezagaa, unapoona watu wanatamani maisha yao yawe bora zaidi, ona fedha zimezagaa.

Wakati wengine wanaona ugumu, wanaona changamoto, wanaona mambo hayaendi, wewe ona fedha zimezagaa, kisha njoo na njia ya kukusanya kila aina ya fedha iliyozagaa pale ulipo.

Naomba uniamini kwenye hili, hata kama imani inakataa kuja, lichukue tu kwa siku moja, nenda kwa mtazamo huu kwamba fedha imezagaa na kazi yako ni kuikusanya. Kisha angalia kipi unachoweza kufanya kuongeza thamani kwa wengine na wao wawe tayari kukulipa wewe.

Nakuambia uniamini kwenye hili kwa sababu ndiyo imani pekee ambayo nimekuwa natumia kwenye maisha yangu na ninapata fedha. Sifikirii uhaba, bali nafikiria kukusanya fedha. Na ninajua nitakusanya mabilioni ya fedha kupitia kuongeza thamani kwa wengine, kutatua matatizo yao na kuwasaidia kutimiza mahitaji yao.

Je upo tayari kwa angalau siku moja tu kuondoka kwenye mtazamo wa KUTAFUTA FEDHA na ukajaribu mtazamo wa KUKUSANYA FEDHA? Hebu ishi siku moja kwa mtazamo huu wa KUKUSANYA FEDHA kisha nipe mrejesho wa yapi uliyojifunza.

Au kama huko nyuma ulikuwa unaishi kwa mtazamo wa kutafuta fedha lakini sasa umekuwa na mtazamo wa kukusanya fedha, pia nishirikishe matokeo gani umekuwa unayapata. Njia ya kunishirikisha ni kutuma email kwenda maarifa@kisimachamaarifa.co.tz

KWA NINI SIYO TAJIRI

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog