Watu wanapenda ukuu kwenye maisha, kwenye kazi zao, kwenye taaluma zao, kwenye biashara zao na mengine wanayofanya.
Lakini ni wachache ambao wamekuwa wakifikia ukuu kwenye yale wanayofanya. Na kadiri siku zinavyokwenda, kwa zama hizi tunazoishi, ndivyo wachache wanaweza kufikia ukuu.
Hii ni kwa sababu, mambo ambayo watu wanafanya, yanapingana kabisa na kanuni ya ukuu, yaani wanafanya mambo ambayo matokeo yake hayawezi kuwa ukuu kabisa.
Na hii ni kwa sababu watu wengi hawajui kanuni ya ukuu, au wanaijua lakini hawajui namna ya kuiishi, au wanaijua, wanajua jinsi ya kuiishi lakini wanaipuuza.

Haijalishi upo kwenye kundi lipi, kama hutaijua na kuiishi kanuni ya ukuu, hutafikia ukuu.
Kabla hatujaendelea kwanza tuwekane sawa kwenye ukuu. Ukuu tunaozungumzia hapa siyo ule wa kuwa bwana na kuwatumikisha wengine, siyo wa kutawala wengine au kuwanyanyasa wengine.
Ukuu tunaozungumzia hapa ni kufika viwango vya juu kabisa kwenye kile ambacho mtu unafanya. Unakuwa umefikia mafanikio ya kiwango cha juu kabisa, na unakuwa umefanikiwa nje na ndani, siyo tu kuonekana nje kwamba umepiga hatua, bali ndani yako unaona umepiga hatua na hilo linakuridhisha.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Uliza Kwanza, Ukamilifu Wa Kanuni Ya Dhahabu Ya Maisha Ya Mafanikio.
Sasa kwa kuwa tupo sawa kwenye ukuu, hebu sasa turudi kwenye kanuni ya ukuu.
Ni kanuni rahisi inayohusisha vitu viwili, kanuni hii ni kama ifuatavyo;
MAPENZI + UNG’ANG’ANIZI = UKUU.
Ni hivyo tu, mapenzi, ukijumlisha na ung’ang’anizi basi unapata ukuu, hapo ni kwa jambo lolote lile.
Kwanza unahitaji kupenda sana kile ambacho unafanya, kipende hasa, kitoke ndani ya moyo wako, uwe tayari kusukuma zaidi ya wengine, uwe tayari kujitoa kweli kweli. Kadiri unavyokuwa na mapenzi juu ya kitu, ndivyo pia inavyokuzuia wewe kuchoka haraka. Wakati wengine wanaangalia saa ngapi muda unaisha waondoke, wewe unatamani hata muda usiishe, uendelee tu kufanya. Mapenzi yanakufanya uweke kila unachopaswa kuweka kwenye kile unachofanya, ili uweze kupata matokeo bora.
Lakini wote tunajua hii ni dunia, sisi tunapanga yetu na dunia inapanga yake, hivyo licha ya kujitoa, haimaanishi kwamba tutapata kila tunachotaka, tena kwa wakati ambao tunataka. Na hapa ndipo sehemu ya pili ya ukuu inapoingia. Lazima uwe KING’ANG’ANIZI kweli, lazima uwe mgumu kukata tamaa na kuacha, lazima uitishe dunia na wengine wote, kwa namna unavyong’ang’ana na kukataa kurudi nyuma.
Hakuna ukuu unaokuja kirahisi, lakini zama tunazoishi sasa, kila siku tunajidanganya zipo njia rahisi za ukuu, na hizo zimekuwa zinatupotezea muda tusipate matokeo tunayotaka kupata.
Penda unachofanya, ng’ang’ana hasa na ukuu utakuwa wako, haitakuwa leo wala kesho, lakini jua ukuu utakuwa wako. Hivyo usiache mpaka umefikia ukuu, na ukifikia ukuu, mchezo ndiyo kwanza unakuwa umeanza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog