Uchumi wa mapinduzi ya viwanda ulijengwa kwenye msingi wa viwanda kutengeneza vitu vya kawaida kwa watu wa kawaida. Ni rahisi kufanya hivyo, na ina faida zaidi. Lakini changamoto kubwa ni moja, ni vigumu kujitofautisha na wengine, ambao nao wanatengeneza vitu vya kawaida kwa watu wa kawaida.

Uchumi wa mapinduzi ya taarifa, umerithi hili pia, kutoa taarifa na maarifa ya kawaida kwa watu wa kawaida. Kitu ambacho ni rahisi, lakini pia kigumu kwa sababu kila mtu anaweza kufanya hivyo. Kila mtu sasa anatoa taarifa na maarifa ya kawaida kwa watu wa kawaida, kitu ambacho kimegeuka kuwa kelele.

Mtu Pekee

Mitandao ya kujamii imeongeza mafuta ya taa kwenye hilo la vitu vya kawaida kwa watu wa kawaida. Kwa sababu mitandao hii inategemea wingi, na kwa kuwa watu nao wanataka wingi, wingi wa marafiki, wingi wa ‘likes’, wingi wa ‘comments’ basi kelele zimekuwa maradufu.

SOMA; UKURASA WA 850; Chanzo Cha Kujiona Hufai…

Njia pekee ya kuondoka kwenye kelele hizi, ni kuacha mchezo huo wa kufanya vitu vya kawaida kwa watu wa kawaida. Hao ni watu ambao huwezi kuwapata, kwa sababu ni watu ambao wamevurugwa na kelele nyingi zinazowalenga.

Cha kufanya chagua watu wenye uhitaji, watu wanaotafuta suluhisho fulani unaloweza kutoa, siyo watu wa kawaida ambao wapo wapo tu, bali watu wenye shida na wanatafuta suluhisho la shida zao.

Watu hao sasa, wape thamani, watatulie matatizo yao, wape njia za kuondokana na changamoto zao na watakuwa tayari kukulipa kile unachotaka kulipwa.

Hawatakuwa watu wengi, lakini watakuwa watu wenye thamani, watu wenye kujali kile unachofanya, na watu unaoweza kuhesabu kwamba wapo kwa ajili yako.

Je unataka wengi na wa kawaida, wasio na manufaa, au wachache, wa kipekee na wenye faida? Kuenda kwa wachache wenye manufaa, unahitaji uende kinyume na tamaa ya kibinadamu ya kutaka wingi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog