Mabadiliko yoyote kwenye maisha siyo rahisi, hata kama mabadiliko hayo hayagharimu fedha.

Yanakuwa mabadiliko magumu kwa sababu kwa sehemu kubwa, yanatutaka tubadili kabisa ile imani ambayo tumeshajijengea kwenye maisha yetu.

Ipo hivi rafiki, kuna vitu vingi ambavyo unaamini ndiyo ukweli na ndivyo maisha yanavyopaswa kuwa, lakini siyo imani sahihi.

Sasa unapotaka kufanikiwa, kazi ya kwanza ni kubomoa zile imani ambazo umejijengea kwa miaka mingi. Na hapa ndipo ugumu wa mabadiliko unapoanzia, kwa sababu kubadili imani ambayo umeishi nayo miaka mingi, ina maana kubadili kabisa maisha yako.

Maisha ambayo kila mmoja wetu anayaishi, yamejengeka kwenye zile imani ambazo tunazo. Unaamka asubuhi na kuanza kusikiliza habari, kwa sababu umeshajiaminisha kwamba usipoanza siku na habari, utapitwa. Labda kuna hatari imetokea na wewe hutaijua kama hujasikiliza habari asubuhi.

SOMA; UKURASA WA 691; Imani Inayowatenganisha Watu Na Utajiri…

Sasa unapotaka kubadili hilo la kusikiliza habari asubuhi, inakuwa kazi kwa sababu unapojaribu, ile imani ambayo ulishajijengea inatikiswa, na hapa unaona kama maisha yako yanatikiswa.

Wapo watu wanaamini kabisa ya kwamba kwenye haya maisha huwezi kufanikiwa bila ya kukopa. Huwezi kuanza biashara bila mkopo, huwezi kujenga nyumba bila mkopo na kama unataka gari, basi lazima ukope. Leo hii ukimwambia mtu huyu hilo siyo sahihi, inakuwa vigumu kwake kuelewa kwa sababu unatikisa imani nzima ambayo maisha yake yametengenezwa. Unafikiri kwa nini watu wanakuwa kwenye madeni miaka nenda miaka rudi hata kama yanawaumiza? Imani ambayo mtu amejijengea kuhusu madeni.

Hivyo rafiki, mabadiliko yoyote unayotaka kufanya kwenye maisha yako, anza na imani uliyonayo. Unapofikiria kubadili chochote kwenye maisha yako, anza kujiuliza unaamini nini kwenye hicho ambacho umekuwa unafanya. Kisha anza kujenga imani ya tofauti, ambayo sasa itakuruhusu ufanye kwa utofauti bila ya kuona kama maisha yako yote yanaporomoka.

Rahisisha mabadiliko kwenye maisha yako kwa kuanza na kile unachoamini, kubali mambo mengi unayoamini kwenye maisha siyo sahihi na unahitaji kujenga imani mpya ili kubadili hatua unazochukua na kuweza kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog