We become wiser by adversity; prosperity destroys our appreciation of the right. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo mwaka huu 2018 unakwenda kuwa bora na wa kipekee sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MAFANIKIO KIDOGO NI SUMU YA MAFANIKIO MAKUBWA.
Wapo watu wengi ambao huwa wanaanzia chini, wanakuwa na hamasa ya kufanikiwa, wanachukua hatua na wanaanza kupata mafanikio, ila baada ya hapo hawakui tena na badala yake wanaanguka kabisa.
Watu hawa wanakuwa wamepata mafanikio kidogo ambayo yanageuka kuwa sumu kubwa kwao.
Mafanikio kidogo yanakuwa sumu kwa sababu;
👉🏼Mtu anaanza kujiona tayari anajua kila kitu hivyo hakuna kipya cha kujifunza.
👉🏼Mtu anaanza kujiona yeye ndiye anayejua kila kitu hivyo hawezi kujifunza kwa yeyote.
👉🏼Mtu anakuwa na hofu ya kupoteza kile kidogo alichopata hivyo hachukui hatua za hatari.
👉🏼Mtu anaanza kusikiliza kauli za wengi na walioshindwa, kwamba tayari ana mafanikio hivyo asijisumbue sana.
👉🏼Mtu anakosa ndoto ya uhakika ya mafanikio, hana picha ya mafanikio makubwa zaidi ya pale alipofika.
Ili kuwa na mafanikio yanayokua na kudumu, haya ni mafanikio ambayo yanaendelea kukua kila siku, unahitaji;
👉🏼Kuwa na ndoto kubwa sana ya mafanikio, kuona kwa hakika ukiwa mbali mno, na ukizidi kuwa bora kila siku.
👉🏼Kuendelea kuweka juhudi kubwa kama vile ndiyo siku yako ya kwanza, au kama vile kuna mtu anakesha usiku na mchana kubomoa mafanikio yako, na ukweli ni kwamba wapo wengi.
👉🏼Kuendelea kuchukua hatua zinazoonekana ni za hatari.
👉🏼Kuendelea kujifunza kila siku, kila siku na kila wakati.
👉🏼Kuacha kuisikiliza jamii na kundi kubwa la watu kwa wanachosema kuhusu mafanikio, maana kwa sehemu kubwa wanachosema siyo sahihi.
Rafiki, fanikiwa na endelea kufanikiwa zaidi, usiruhusu mafanikio kidogo kuwa sumu kwako.
Uwe na siku njema leo, siku ya mafanikio zaidi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha