“To accuse others for one’s own misfortunes is a sign of want of education. To accuse oneself shows that one’s education has begun. To accuse neither oneself nor others shows that one’s education is complete” – Epictetus

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii bora sana ya leo.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio kwa mwaka huu 2018, ambao unatuwezesha kupiga hatua zaidi.

Asubuhi ya leo tutafakari UKIFIKA KIWANGO HICHI, ELIMU YAKO IMEKAMILIKA…

Ni rahisi sana kuwalaumu wengine pale ambapo hutaki kubeba majukumu yako.
Hivyo unajidanganya wengine ndio wanaohusika, wengine ndio wamesababisha wewe umeingia kwenye matatizo ambayo unayo, na wakati mwingine kuona wengine ndiyo wameshindwa kukutoa pale ulipo.

Ni rahisi kujilaumu wewe mwenyewe pale ambapo hutaki kuuangalia ukweli kama ulivyo. Pale ambapo hutaki kukubaliana na ukweli wa mambo, unatafuta njia ya mkato ambayo ni kujilaumu mwenyewe.
Kujilaumu mwenyewe ni bora kuliko kuwalaumu wengine kwa sababu angalau unakubali majukuku yako, lakini kwa kuwa hutaki kuuangalia ukweli, inakuwa kikwazo kwako.

Hatua ya juu kabisa, na hatua ambayo ukishafikia basi kwa kila linalotokea unawajibika nalo na kujifunza pia ni hatua ya kutomlaumu yeyote.
Hata kama kitu kikubwa kiasi gani kimetokea, unakipokea kama kilivyotokea na kukubali kwamba kimetokea bila ya kutafuta wa kulaumu.

Lolote linalotokea kwenye maisha yako, kubali kwamba limeshatokea, chukua jukumu la kubeba wajibu huo na jifunze ili wakati mwingine lisitokee kama hilo.
Hii ndiyo njia bora kabisa ya kuhakikisha unakuwa bora zaidi kila siku.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha