Kwenye mchezo wa riadha, kinachomtofautisha mshindi wa kwanza na mshindi wa mbili inaweza kuwa sekunde chache sana, lakini mshindi wa kwanza atapata zawadi kubwa sana ukilinganisha na mshindi wa pili. Tofauti ya sekunde chache kwenye ukimbiaji, inaleta tofauti mara mbili ya matokeo kwenye zawadi. Lakini ukiangalia, mshindi wa kwanza hajakimbia mara mbili ya alivyokimbia mshindi wa pili, bali ni tofauti ndogo.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa kila tunachofanya kwenye maisha, wanaofanikiwa hawapo bora sana ukilinganisha na wasiofanikiwa. Bali kuna tofauti ndogo ndogo sana wanazo, ambazo ukizikusanya pamoja unaona tofauti kubwa baina ya watu hao.

Hivyo unapofikiria kufanikiwa, acha kufikiri utahitaji kuwa bora mara mbili zaidi ya wengine ili kupata matokeo makubwa. Badala yake jua unahitaji kupiga hatua ndogo ya ziada ukilinganisha na hatua wanazopiga wengine. Unahitaji kwenda mbele zaidi ya wanapoishia wengine, hata kama siyo mbali sana.

SOMA; UKURASA WA 243; Baada Ya Kufanya Kazi Iliyo Bora Sana.

Na kipimo kizuri cha kutumia ni asilimia 1 ya ziada ukilinganisha na wengine. Badili kitu kwa asilimia moja ya ziada ukilinganisha na wengine.

Japokuwa pia vipo vitu ambavyo unaweza kufanya kwa hatua kubwa ukilinganisha na wengine, mfano kufanya kazi mara mbili ya wanavyofanya wengine, au kujifunza mara mbili ya wanavyojifunza wengine.

Chochote ambacho unaweza kufanya zaidi ya wanavyofanya wengine, fanya hivyo, kitakuwa na msaada mkubwa kwako. Na siyo lazima iwe mara mbili ya wanavyofanya wengine, au kwa utofauti mkubwa sana, unachohitaji ni hatua ya ziada, kwa asilimia moja tu ukilinganisha na wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog