Maisha ni magumu, lakini watu wamekuwa wanazidisha ugumu wa maisha kiasi kwamba wanaona hayawezekani tena.

Moja ya njia ambazo watu wamekuwa wanazidisha ugumu wa maisha yao wenyewe, ni kukwepa majukumu yao wenyewe.

Mwanasaikolojia mmoja amewahi kusema kwamba, hakuna magonjwa ya akili, bali kuna watu ambao wanajaribu kutoroka matatizo yao. Yaani kinachofanya mtu anaonekana ana ugonjwa wa akili, ni kwa sababu kuna matatizo au changamoto anazojaribu kuzitoroka.

Moja ya njia ambazo watu wamekuwa wakitumia kukwepa na kutoroka changamoto zao ni kulalamika na kulaumu wengine.

Pale jambo baya linapotokea, au mtu anapopata matokeo tofauti na alivyotegemea, anatafuta watu wa kuwalaumu au kuwalalamikia.

Na cha kushangaza ni kwamba huwa hakosekani mtu au kitu cha kulaumu, kwenye jambo lolote lile. Yaani hata kama umechukua kisu na ukajikata wewe mwenyewe, ukaumia, bado utapata watu wa kulaumu na kulalamikia kwa hatua hiyo uliyochukua.

Wapo watu na vitu ambavyo vimezoea kulaumiwa na kulalamikiwa pale mambo yanapokwenda tofauti na mtu anavyotegemea.

Wa kwanza ni serikali, kila serikali huwa inalaumiwa kwa kila kitu, kila kitu.

Wa pili ni wazazi, utamkuta mtu ana miaka 30, maisha yake ni magumu halafu anasema kama wazazi wake wangefanya kitu fulani basi angekuwa bora zaidi, na hakikosekani kitu cha kulaumu kwa wazazi.

Vitu kama mazingira, hali ya hewa na hata uchumi, huwa vina nafasi ya kulaumiwa kwenye jambo lolote lile. Mtu biashara yake haiendi vizuri, kwa sababu haisimamii vizuri, anaendesha kwa mazoea na sababu atakayokupa ni uchumi mbaya.

Maisha Hayajawahi

Rafiki yangu, mimi nimekuwa nakuambia kitu kimoja, jambo la hovyo kabisa unaloweza kufanya na muda mfupi uliopewa hapa duniani, ni kulaumu au kulalamikia watu wengine kwa jambo lolote lile.

Ni jambo la hovyo kwa sababu halina manufaa yoyote, linakupa ulevi wa muda tu, kuona kwamba mwingine kakukosea, lakini mwisho wa siku, maisha yako yanaendelea kuwa magumu.

Hivyo ambacho nimekuwa nakushirikisha ni kuchukua hatua. Kama kuna kitu kimetokea ambacho hukipendi au hukutegemea, basi angalia kama ipo hatua ya kuchukua na ichukue, kama hakuna hatua ya kuchukua basi achana nacho.

Pamoja na kueleweka kirahisi kwa somo hili la kutokulaumu wengine, bado unaweza kujihalalishia kwamba kuna wakati hakuna namna bali kulaumu wengine. Na mimi nakuambia siyo kweli, nyakati zote hakuna manufaa kuwalaumu wengine, labda kama unafurahia ulevi wa muda mfupi unaopata kwa kulaumu wengine.

Hapa nakupa mifano mitano ya maeneo ambayo unaweza kuona ni halali kulaumu wengine, wakati hupaswi kufanya hivyo.

  1. Kwenye mahusiano.

Umeingia kwenye mahusiano na mtu, ambaye ulimwamini sana, akauahidi mengi na ukampa moyo wako wote, ukijua umempata mtu wa maisha yako. Lakini baadaye anakuja kukusaliti, anakuja kuvunja ahadi zake na anakunyanyasa na kukuumiza. Mmeingia kwenye ndoa na amebadilika, anakusumbua hakuna mfano, unaona kama amekuwa mtu mwingine kabisa na alivyokuwa awali.

Hapa unaweza kuona una kila sababu ya kumlaumu mwenzako, kwa sababu amekwenda kinyume na alivyoahidi. Lakini nikuambie tu rafiki, huna cha kulaumu, kwa sababu kama ungekuwa makini na ukamchunguza vizuri, kuna viashiria alikuwa navyo tangu mwanzo ambavyo vilikuwa vinakuonesha huyu mtu atakuja kuwa tatizo. Lakini huenda uliviona na ukavipuuza, ukijiambia hakuna shida, atabadilika tu, au nitambadili. Sasa ulipo unavuna ulichopanda, huna wa kumlaumu bali wewe mwenyewe.

Umebeba fedha zako mfukoni, kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli zako mbalimbali, akatokea mtu akakuibia, iwe kwa nguvu au kwa kutokujua. Mtu huyo si anastahili lawama?

Hapana, wewe umekuwa mzembe, unashindwaje kulinda fedha zako mpaka mwingine anaweza kujua unazo na akakuibia, wakati mwingine kuwa makini.

SOMA; Ushauri Wa Bure Unaokuzunguka Ambao Bado Hujaanza Kuutumia.

  1. Ubia kwenye biashara.

Umeingia kwenye ubia wa kibiashara na watu wengine. Mlikubaliana vizuri mwanzoni, kila mtu akapewa wajibu na majukumu yake. Wewe unatekeleza yako lakini mwingine au wengine hawayatekelezi, wanafanya maamuzi ya hivyo, biashara inakufa. Si wanastahili kulaumiwa?

Ndiyo, wanastahili kulaumiwa kama walikushikia bastola kwamba lazima ushirikiane nao la sivyo wanakuua, kama hawakufanya hivyo, ulifanya uzembe kuingia ubia na watu ambao hukuwajua vizuri.

  1. Nchi imeingia kwenye vita na watu wanakufa.

Kuna vitu ni rahisi kulaumu na kulalamikia, mfano nchi inaamua kuingia kwenye vita, na watu wasio na hatia wanauawa na kuumia, uchumi unaharibika. Ni rahisi kulaumu viongozi waliofikisha nchi katika hali kama hiyo.

Lakini unapaswa kukumbuka kwamba, viongozi hawakujiweka pale, bali wamepewa mamlaka na wananchi, wewe ukiwa mmoja wao na wanatekeleza kile ambacho wametumwa kuwakilisha. Hivyo kama serikali imeua, na wewe umeshiriki kuua. Na hata kama utasema hujachagua serikali hiyo, basi utuambie umefanya nini kuhakikisha serikali hiyo haiendelei kuwepo, kinyume na hapo unakuwa mshiriki kwenye kila linalofanywa na serikali, maana unakuwa umeipa mamlaka.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; TAO TE CHING (Falsafa Ya Uchina Ya Kukuwezesha Kuwa Na Maisha Bora Na Yenye Mafanikio).

  1. Kupata ajali.

Unatembea barabarani, eneo la waenda kwa miguu, mara linatokea gari na kukugonga na unaumia, si anastahili kulaumiwa mwenye gari? Au umepanda kwenye usafiri wa umma, na dereva anaendesha kwa mwendo kasi, mnapata ajali, je dereva si wa kulaumiwa?

Ndiyo atalaumiwa kama unataka tu kujifurahisha, lakini umekosa umakini kujikuta kwenye eneo la ajali, hata kama ajali imekufuata ulipo kisheria. Hivi kwanza umepata ajali hiyo ukiwa unafanya kile ambacho ulipanga kufanya? Au kuna vitu ulikuwa umeahirisha, unaenda na mipango ambayo hata haipo na kujikuta kwenye ajali?

Sijui kama umenielewa vizuri hapo, lakini nifupishe ka kukuambia tu, kama umejikuta kwenye ajali, iwe umesababisha wewe au wamesababisha wengine, wewe pia ni chanzo.

Rafiki, hii inaweza kuwa falsafa ngumu sana kwako kuelewa, hasa kama umeshazoea kulaumu kila mtu kwa kila kitu. Lakini unapokaa chini na kutafakari kwa kina, utajiona jinsi ambavyo wewe ni msababishi wa kila kinachoendelea kwenye maisha yako.

Fikra zinazotawala akili yako, mazingira unayojiruhusu kuwepo na mambo unayovumilia au kutokuyachukulia hatua, yanageuka kuwa chanzo cha matatizo na changamoto nyingi unazopitia. Ukiongeza umakini wako kwa kila unachofanya, utapunguza matatizo yasiyo na umuhimu na kuacha kabisa kulaumu wengine.

Lengo siyo kulaumu wengine, lengo siyo kujilaumu wewe mwenyewe, bali lengo ni kujifunza na kuchukua hatua ili kuhakikisha chochote kilichotokea kwenye maisha yako hakijirudii tena na kuleta madhara makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

MIMI NI MSHINDI