Malalamiko na lawama ni vitu viwili ambavyo huwa vinapatikana kwa watu wote ambao wameshindwa. Wengi hudhani kwamba wanalalamika na kulaumu kwa sababu wameshindwa. Lakini ukweli ni kinyume kabisa na hilo, watu wanakuwa wameshindwa kwa sababu wanalalamika na kulaumu.

Rudia hiyo sentensi taratibu ili ikuingie vizuri na ukachukue hatua za tofauti kwenye maisha yako kuanzia leo. UNASHINDWA KWENYE MAISHA KWA SABABU YA KULALAMIKA NA KULAUMU. Ukieleza hiyo sentensi na kuifanyia kazi, kamwe huwezi kushindwa.

Na hilo ni jambo ninakuambia siyo kukufurahisha, bali kwa sababu ushahidi upo dhahiri kabisa, ambao hata wewe mwenyewe unaujua. Hivi unafikiri kati yako wewe unayesoma hapa sasa hivi, na mtu ambaye amefariki dunia siku ya leo, nani ana nafasi ya kubadili maisha yake? Jibu ni wewe, kwa sababu bado upo hai, wakati huyo mwingine ameshafariki.

Tuendelee, kati yako wewe, ukiwa na afya njema kabisa na una uwezo wa kufanya shughuli zako na mwingine ambaye anaumwa yupo hoi hospitalini, nani anayeweza kutumia muda wake wa leo kufanya mambo makubwa na ya tofauti? Sihitaji kukuambia jibu, kwa sababu unalijua tayari.

Kama utakuwa unafuatilia kwa umakini, mpaka sasa utakuwa umeshaanza kufunguka ni nini ninachotaka kukuambia. Ni kweli unaweza kuwa na mengi ambayo unayalalamikia na kulaumu, lakini je umekuwa unaangalia upande wa pili?

Je umekuwa unaangalia mambo au vitu ulivyonavyo, ambavyo kuna watu wengine wangeshukuru sana kama wangekuwa navyo? Wakati wewe unalalamika kwa vitu ulivyokosa, kuna ambao wangetamani sana kuwa na vile ambavyo unavyo.

Swali ni je wewe unatumiaje vitu ulivyonavyo, ambavyo kuna wengine hawana na kama wangevipata wangefanya makubwa sana? Hapa ndiyo ninarudi kwenye kauli niliyofungua nayo, kwamba unashindwa kwa sababu ya kulalamika na kulaumu.

Ninachomaanisha ni kwamba, kwa kulalamikia na kulaumu vile ulivyokosa, unashindwa kutumia vizuri vile ambavyo tayari unavyo. Hilo linapelekea wewe kutokupata matokeo mazuri kitu kinachofanya usifanikiwe. Hiyo ina maana kwamba kama ukiacha kulalamika na kulaumu na ukachagua kutumia kile ambacho tayari unacho, utaweza kufanya makubwa zaidi ya yale unayofanya sasa.

Swali ni je unawezaje kuachana na hali ya kulalamika na kulaumu ili uweze kutumia vile ambavyo tayari unavyo. Na hapo ndipo penye zoezi muhimu sana unalopaswa kufanya kila unapotaka kulalamika au kulaumu. Zoezi hilo ni kuwa mtu wa shukrani.

Kuwa mtu wa shukrani ni kushukuru kwa vitu ambavyo unavyo na vimekuwa na manufaa kwako. Pale unaposhukuru kuhusu kitu, unakuwa umekithamini na hivyo kuweza kukitumia vizuri na kwa manufaa.

Huwa kuna usemi kushukuru ni kuomba tena, yaani pale unaposhukuru, unakuwa tayari kupokea tena hicho ambacho umeshukuru kuwa nacho. Hebu fikiria hapo rafiki yangu, yaani unaweza kuendelea kupata mambo mazuri uliyonayo, kwa kufanya kitu kimoja tu, kushukuru. Nani anayeshindwa kushukuru? Inaweza isiwe tabia uliyozoea, lakini ni ambayo unaweza kuijenga.

Kwa sababu kila kitu kwenye maisha yetu ni tabia, na kwa sababu njia ya kubadili tabia mbaya ni kuibadilisha na tabia nzuri, hapa tunaenda kujifunza jinsi ya kuacha kulalamika na kulaumu. Unachopaswa kufanya ni kushukuru pale unapotaka kulalamika au kulaumu.

Hili ndiyo zoezi ambalo nataka uondoke nalo na kwenda kulifanya kila siku. Pale unapopata msukumo wa kulalamika au kulaumu kwa chochote kile, jikamate hapo hapo na shukuru. Chagua vitu ambavyo unashukuru kuwa navyo, vitu ambavyo tayari unavyo ila kuna wengine hawana.

SOMA; Ninaposema Usilalamike Wala Kulaumu Yeyote, Namaanisha Hivi (Mifano Mitano Ya Maeneo Uliyozoea Kulalamika Ambayo Hayakusaidii Chochote).

Hata kama kwa sasa hutumii vitu hivyo vizuri, anza kwa kushukuru kile kitendo tu cha kuwa navyo, kwa sababu wapo wengi ambao wangetamani kuwa navyo, ila wanashindwa kuvipata. Kwa wewe kuwa navyo, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kunufaika navyo kama utaanza kuvitumia vizuri.

Kwa yote uliyonayo ambayo unayalalamikia na kuyalaumu kama kikwazo kwako kufanikiwa, orodhesha pia mazuri uliyonayo ambayo wengine hawana. Kisha jiulize ni kwa namna gani unaweza kuyatumia hayo mazuri ili kuleta matokeo ya tofauti na unayopata sasa.

Uwezo wa kufanya makubwa na kufanikiwa tayari upo ndani yako, tabia yako ya kulalamika na kulaumu imepelekea ushindwe kutumia uwezo huo. Anza sasa kushukuru badala ya kulalamika na kulaumu na utaweza kuleta matokeo makubwa na ya tofauti kwenye maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.