Ustaarabu ni moja ya maneno ambayo yamekuwa yanatumika vibaya na kuwa kikwazo kwa watu wengi kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Kama neno, ustaarabu halina shida yoyote, maana ni kufanya mambo kwa namna sahihi na yenye tija. Lakini kwenye matumizi, neno ustaarabu limebadilishwa kabisa maana yake.
Kwenye jamii, ustaarabu inachukuliwa ni kufanya kile ambacho kinawafurahisha wengine, hata kama hakina manufaa kwa anayefanya. Pale mtu anapofanya kitu sahihi, ambacho kina manufaa kwake lakini hakiwafurahishi wengine anaonekana siyo mstaarabu.

Kwa sababu watu wanapenda kukubalika na wengine, basi huwa wanafuata dhana hiyo potofu ya kutaka kuonekana ustaarabu. Hivyo huwa wanahangaika na mambo yasiyokuwa na tija kabisa kwao, kwa lengo la kuwafurahisha wengine.
Kwa bahati mbaya sana, kuwafurahisha wengine haijawahi kuwa njia sahihi ya kufanikiwa kwenye maisha. Kwa sababu hata ufanye nini, huwezi kuwafurahisha watu wote. Na hata kwa baadhi ya wale unaowafurahisha, bado watakuweka kwenye gereza fulani la wewe kuendelea kufanya mambo yanayowafurahisha wao hata kama kwako hayana manufaa.
Ustaarabu pekee kwenye maisha ni wewe kupata kile unachotaka. Hivyo wajibu wako namba moja kwenye maisha ni kuhakikisha unapata kile unachotaka kwa kutumia njia zote zilizo sahihi. Huhitaji kuwafurahisha watu, unachohitaji ni kupata kile unachotaka.
Kwa sababu haijalishi wengine wanakukubali kiasi gani, kama hujapata kile hasa unachotaka, wewe siyo mstaarabu. Unakuwa siyo mstaarabu kwa sababu ndani yako unakuwa na hali ya kutokuridhika. Kwa nje unaweza kuonekana kuwa na furaha, lakini kwa ndani yako unakuwa na majuto kwa sababu hujapata kile unachotaka na ambacho unajua kipo kabisa ndani ya uwezo wako.
Kwenye biashara, ustaarabu ni kuweza kujenga biashara inayojiendesha yenyewe kwa mafanikio bila ya kutegemea uwepo wako wa moja kwa moja. Ili kufikia hilo lazima utafanya mambo mengi ambayo hayatawafurahisha walio wengi. Kuna wabia unaoshirikiana nao ambao utapaswa kuachana nao. Kuna wafanyakazi utakaowaajiri ambao utapaswa kuwafukuza kazi. Kuna wengi watataka kunufaika isivyo sahihi kupitia wewe na utahitaji kuwakatalia. Hayo yote yatawafanya baadhi ya watu wasifurahishwe na mafanikio utakayokuwa umeyapata. Lakini hilo halijalishi, kwa sababu kama umepata unachotaka, ukiwa hujavunja sheria yoyote, hilo ndiyo muhimu zaidi.
Kwenye mauzo, ustaarabu ni kukamilisha mauzo kwa kuwafanya wateja wakubali kununua. Hilo litakutaka wewe uwe na wateja wengi sana na ambao unawafuatilia kwa karibu. Kitendo cha wewe kuwa na wateja wengi hakitawafurahisha wengine. Na kitendo cha kuwafuatilia wateja kwa wingi na msimamo bila kuacha, kitawaudhi baadhi ya hao wateja unaowafuatilia.
Wauzaji wasio na mafanikio, huwa hawawafuatilii wateja wao na kuwasisitiza kununua. Huwa wanadhani kwa kufanya hivyo wataonekana wastaarabu. Wanaona wakiwafuatilia wateja sana watakuwa wanawasumbua na kuonekana siyo wastaarabu. Lakini hawauzi, je hapo kuna ustaarabu gani? Utasemaje wewe ni muuzaji mstaarabu wakati huuzi? Kuwa muuzaji halafu usiuze, kwanza hupaswi kujiita muuzaji na pili, unakosa ustaarabu, kujiita kitu ambacho hukifanyi.
Hivyo ustaarabu pekee kwa muuzaji ni kuuza. Na ili kukamilisha hilo anapaswa kufanya kila kinachoweza kuwashawishi wateja kununua, ambacho siyo kinyume na sheria. Kama kwa muuzaji kulia inaweza kumshawishi mteja, anatakiwa alie. Huwa tunasema mauzo ni maigizo, hivyo unapaswa kuwa tayari kuigiza chochote kinachohitajika kuigizwa ili mteja ashawishike kununua kile unachouza.
Acha kujidanganya na dhana potofu ya ustaarabu wa kuwafurahisha wengine. Ustaarabu pekee kwako ni kupata kile unachotaka, bila ya kuvunja sheria. Kama hujapata unachotaka, haijalishi wengine wanakukubali kiasi gani, wewe siyo mstaarabu. Jiite vingine vyovyote unavyotaka, lakini usijiite mstaarabu. Maana unakuwa ni mtu uliyeshindwa na kwenye kushindwa hakuna ustaarabu.
Pambana kwa kila namna kupata unachotaka. Wengi hawatapenda mapambano unayoyaendesha na ushindi utakaoupata, lakini watakuheshimu. Na heshima ni nzuri na muhimu kuliko kupendwa. Kuwa mstaarabu kwa kuhakikisha unapata kile hasa unachotaka. Mengine hayatakuwa na umuhimu kama hujapata unachotaka.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza dhana hii kwa kina, karibu ujifunze hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.