Matajiri Wawekezaji wa programu ya NGUVU YA BUKU, tumechagua kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja kwa sababu ya urahisi wake na kutupa sisi fursa ya kuendelea na shughuli zetu nyingine.
Kwa nchini Tanzania, kuna aina mbalimbali za mifuko ya pamoja ya uwekezaji. Tumechagua kuwekeza kupitia mifuko ya UTT AMIS (Unit Trust Of Tanzania, Asset Management and Investor Services).
Tumechagua mifuko hii kwa sababu mbalimbali, ikiwepo;
1. Ukongwe wa mifuko hiyo, ambapo imekuwepo kwa karibu miaka 20 sasa (Tangu mwaka 2003).
2. Kufanya vizuri kwa mifuko licha ya kuyumba kwa uchumi ambapo kumekuwa kunatokea.
3. Urahisi wa kuingia na kuendelea kuwekeza kwa viwango vidogo vidogo.
4. Urahisi wa mchakato mzima wa kujiunga, kuwekeza na hata kutoa. Unaweza kufanya hayo yote ukiwa na simu yako tu.
5. Ukuaji mzuri wa thamani ukilinganisha na njia nyingine za kuweka fedha kama akiba ya muda mrefu au hatifungani za muda mfupi.

Jinsi UTT AMIS inavyofanya kazi.
Kwa mfumo wa Mifuko ya uwekezaji wa pamoja ambao tumejifunza, mfuko unakusanya fedha za wawekezaji, kisha unawekeza halafu faida inayopatikana inarudi kwa wawekezaji.
Swali ni faida inapatikanaje na wewe mwekezaji unafaidikaje? Hili ndiyo wengi wamekuwa hawalielewi, hapa nakwenda kukueleza kwa lugha rahisi na mifano ili upate uelewa wa msingi kama mwekezaji.
Kwanza kabisa, uwekezaji unaofanya kwenye UTT unahesabiwa kwa vipande. Hivi vipande siyo vitu unavyopewa uwe navyo, bali ni ukokotozi wa uwekezaji wako kulingana na thamani ya mfuko.
Hiyo ni njia rahisi ya kuweza kupima thamani ya ukuaji wa uwekezaji wako, ukizingatia kwamba uwekezaji ni wa nyakati zote hivyo faida itategemea na thamani wakati unawekeza na ongezeko.
Tuchukue mfano unataka kuwekeza kwenye mfuko wa Umoja na wakati wa kuwekeza kipande kinakuwa na thamani ya Tsh 1,000/=. Kama utawekeza Tsh 10,000/= maana yake utakuwa umepata vipande 10.
UTT inaenda kuwekeza mtaji wako uliowekeza kwenye maeneo mbalimbali, kama itapata faida, inairudisha na kuigawa sawa kwa vipande vyote. Hivyo kama baada ya muda thamani ya kipande imekuwa Tsh 1,100/=, wewe mwenye vipande 10, sasa hivi thamani yake inakuwa Tsh 11,000/=.
Hapo unaona iliwekeza elfu 10, lakini baadaye uwekezaji huo huo umekuwa elfu 11. Ina maana unapokuja kuuza vipande vyako unaviuza kwa thamani ya vipande kwenye wakati huo na siyo kwa ile thamani iliyokuwepo wakati unanunua.
Kwa upande wa pili pia ni sawa, kama mfuko utapata hasara na thamani ya vipande kushuka, thamani ya uwekezaji wako inashuka pia.
Kwa kuwa uwekezaji utakuwa unafanya mara kwa mara, kila wakati unapowekeza, thamani ya vipande inakuwa tofauti. Hivyo vipande unavyopata vinategemea na thamani yake wakati unawekeza.
Mifuko iliyo chini ya UTT AMIS.
UTT AMIS ina mifuko 6 ambayo iko chini ya usimamizi wake, kila mfuko ukiwa na malengo yake na sera yake ya uwekezaji.
Mifuko hiyo ni kama ifuatavyo;
1. Mfuko wa Umoja
2. Mfuko wa Wekeza Maisha
3. Mfuko wa Watoto
4. Mfuko wa Kujikimu
5. Mfuko wa Ukwasi
6. Mfuko wa Hati Fungani
Kwenye masomo yanayofuata tutajifunza mfuko mmoja mmoja, malengo yake, sera yake ya uwekezaji na faida kwa wawekezaji.
Faida nyingine za kuwekeza na UTT AMIS.
Kuna faida zingine kubwa ambazo mtu anaweza kupata kwa Kuwekeza katika mifuko inayosimamiwa na UTT AMIS;
1. Uwekezaji Mseto
Kutawanya uwekezaji hupunguza hatari ya uwekezaji na kuongeza mapato. Hakuna kikomo kwa idadi ya wawekezaji ambao wanaweza kumiliki vipande kwenye mfuko wetu wowote. Kuwepo kwa wawekezaji wengi zaidi katika mfuko ndivyo rasilimali zaidi na faida inavyopatikana kwa uwekezaji mseto katika mfuko.
2. Weledi
UTT AMIS ndiyo wasimamizi wa mifuko yote sita. Ni wasimamizi wa viwango vya juu vya kimataifa wenye rekodi ya mapato mazuri katika soko hapa nchini. Ikumbukwe, wasimamizi bora wa mifuko husaidia kuongeza kipato cha mwekezaji.
3. Usalama
Mifuko ya uwekezaji wa pamoja inaratibiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na inadhibitiwa na sheria ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja yenye lengo la kumlinda mwekezaji. Kanuni hizi zinahusiana na shughuli za kampuni za Usimamizi/Uwendeshaji wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
4. Unafuu
Mifuko ya uwekezaji wa pamoja inakupa unafuu wa kununua hisa za makampuni yanayofanya vizuri. Mwekezaji ana uwezo wa kupata hisa zote ambazo mfuko umewekeza kwa ununuzi mmoja.
5. Urahisi Na Vigezo Vya Uwekezaji
Unaweza kuwekeza kwa muda mrefu au mfupi. Hakuna kipindi mahsusi/maalum cha uwekezaji kilichowekwa. Vipande vya mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni rahisi kununua na ni rahisi kuuza. Mwekezaji anaweza kubadilisha mgawanyo wa mali kulingana na hali ilivyo mwekezaji anaweza kubadilisha uwekezaji kutoka uwekezaji wa msingi wa hisa (hisa) hadi dhamana ya mapato ya moja kwa moja (Hatifungani za muda mfupi na hati fungani za muda mrefu) au mchanganyiko wa aina yoyote utakohitajika. Hili linategemea na waraka wa toleo wa mfuko.
6. Ukwasi
Mwekezaji anaweza kuwekeza kwa muda mrefu au mfupi kulingana na sifa za mfuko. Mwekezaji anauwezo wa kuamua wakati anaotaka kuuza vipande pia kupata pesa za mauzo ya vipande kwa muda mfupi. Kwa kuwa uwekezaji ni zoezi la muda mrefu, wawekezaji wanashauriwa kuwa na mtazamo wa muda mrefu ili kunufaika zaidi na uwekezaji.
Mjadala wa somo.
Kwa yale uliyojifunza kwenye somo hili, shirikisha majibu ya maswali yafuatayo kwenye maoni hapo chini.
1. Lini ilikuwa mara ya kwanza kwako kusikia kuhusu UTT AMIS? Uliposikia ulielewaje? Je uliamini au kutokuwa na imani?
2. Kwa sasa unaelewaje kuhusu UTT AMIS tofauti na wakati unasikia kwa mara ya kwanza?
3. Eleza jinsi ambavyo faida ya uwekezaji (ukuaji wa thamani) kwenye UTT inapatikana na wewe kama mwekezaji kunufaika.
Shirikisha majibu yako kwenye mjadala kama sehemu ya kujifunza na kuendelea kuwa mwekezaji bora na kujenga utajiri kama lilivyo lengo letu.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.