Rafiki yangu mpendwa,

Fedha ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukiongelea awezavyo. Lakini pia ndiyo kitu ambacho watu wengi sana hawana elimu ya kutosha.

Yaani utakuta mtu ana elimu kubwa sana kwenye mambo magumu kama sayansi na historia, lakini inapokuja kwenye fedha, hana tofauti na mtu ambaye hakuenda darasani kabisa.

Hii ni kwa sababu hakujawahi kuwa na mtaala maalumu kuhusu fedha kwenye elimu rasmi ambayo wengi tumeipata. Na ndani ya familia, kuongelea fedha ni kitu kibaya, wengi hawathubutu hata kukaa na kujadili fedha, itaonekana ni watu wenye tamaa na wasiojali.

Hivyo elimu pekee ambayo watu wanayo kuhusu fedha, ni mazoea ambayo wamejifunza kutoka kwa wale wanaowazunguka.

Utawezaje kuelezea hali ambayo utaikuta inafanana kifedha kwa watu wa aina fulani. Mfano ukienda kwa waajiriwa, utakuta wote inapofika mwisho wa mwezi, hawana fedha, wakipokea mshahara haudumu muda mrefu na baada ya hapo wataishi kwa kukopa. Sehemu kubwa ya waajiriwa utawakuta wana mikopo kwenye taasisi za kifedha, na ukiwauliza kwa nini walichukua mikopo ile wala hawana sababu za msingi. Na hata ukiangalia sababu ya kuchukua mkopo na matumizi ya mkopo utakuta haviendani.

FEDHA KWA BLOG

Kwa kuwa elimu ya fedha ni mtihani kwenye jamii zetu, hapa kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA nimekuwa nakushirikisha elimu hii bila ya kujali hisia zako juu ya fedha. Na kama unataka kuchimba kwa undani zaidi kuhusu ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, basi karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwenye makala ya leo, nakwenda kukushirikisha kanuni tatu muhimu kuhusu fedha, ambazo kama utaweza kuziishi kila siku basi utaondokana na matatizo mengi sana ya kifedha. Jifunze kanuni hizi na chukua hatua, utaondokana na changamoto nyingi za kifedha ambazo unajitengenezea wewe mwenyewe.

Kanuni ya kwanza; watu wanakulipa kulingana na thamani unayozalisha.

Watu hawakulipi kwa sababu wanakuonea huruma,

Watu hawakulipi kwa sababu unastahili kulipwa,

Watu hawakulipi kwa sababu kuna vitu unajua,

Na wala watu hawakulipi kwa sababu elimu yako ni kubwa.

Watu wanakulipa kwa sababu ya thamani unayozalisha.

Hii ina maana kwamba kama malipo unayopata sasa ni madogo, basi thamani unayozalisha ni ndogo. Hivyo ukitaka kuongeza kiasi unacholipwa, unahitaji kuanza kuongeza thamani unayozalisha.

Popote ulipo, angalia ni kitu gani unazalisha kwa wengine, angalia ni thamani ipo unaitoa, angalia ni changamoto zipi unatatua. Kisha weka juhudi kuzalisha zaidi na kwa hakika kipato chako kitaongezeka zaidi.

SOMA; Ninaposema Usilalamike Wala Kulaumu Yeyote, Namaanisha Hivi (Mifano Mitano Ya Maeneo Uliyozoea Kulalamika Ambayo Hayakusaidii Chochote).

Kanuni ya pili; kadiri unavyoongeza kipato chako, ndivyo unavyoweza kutoa thamani kubwa zaidi.

Tumeona kwamba unalipwa kulingana na thamani unayozalisha. Lakini pia thamani unayozalisha itategemea na kiasi unacholipwa. Hii ina maana kwamba kadiri kipato chako kinavyokua, ndivyo unavyoweza kutoa thamani kubwa zaidi.

Hivyo unapaswa kuongeza thamani, ili kipato kiongezeke na uweze kuongeza thamani zaidi na zaidi.

Wengi huwafanya kosa kubwa, pale kipato kinapoongezeka wanazoea na kupunguza thamani, kwa sababu fedha wanazokuwa wamepata zinakuwa kama usumbufu kwao na kuwaondoa kwenye kile walichokuwa wanafanya kwa ubora.

Kadiri kipato kinavyoongezeka ndivyo unavyopaswa kuongeza thamani zaidi. Maana kipato zaidi kinakupa uhuru zaidi na kinakuwezesha kununua muda zaidi na utaalamu zaidi wa wengine.

Kanuni ya tatu; fedha ni kiashiria kwamba unafanya kitu sahihi.

Kama unafanya kitu sahihi na unakifanya kwa ubora wa kipekee, unapaswa kukipwa vizuri. Hivyo kadiri kipato chako kinavyokuwa kikubwa ni kiashiria kwamba unafanya vitu sahihi kwako na kwa wengine pia.

Na hapa siongelei wale ambao wanaweza kulaghai na kupata fedha nyingi haraka, hao hawatadumu nazo, watazirudisha zote kwa namna moja au nyingine. Kipato kinachokua na kudumu ni kile inachotengenezwa kwa njia sahihi.

Kama unatatua tatizo la watu, unawapa kile wanachohitaji, ambacho ni bora kabisa kwao, lazima ulipwe fedha. Na kama unafanya kilicho sahihi na hulipwi vizuri, kuna tatizo jingine utakuwa nalo.

Jikumbushe na kuishi kanuni hizo tatu kuhusu fedha kila siku na utaweza kuongeza sana thamani unayotoa, kitu ambacho kitapelekea kipato chako kuongezeka. Na ongezeko la kipato chako litakuwezesha kuongeza zaidi thamani yako. Yaani ni moto unaojichochea mwenyewe, ambapo wewe unauanzisha kwa kutoa thamani kubwa na kufanya kilicho sahihi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha