Watu huwa tunafikiria makubwa, tuna ndoto kubwa sana kwenye maisha yetu, ndoto za kuibadili dunia na kuifanya kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi.
Lakini pamoja na ndoto kubwa sana tunazokuwa nazo, kuna mambo madogo mno yanakuwa yanatushinda.
Kuna vitu vidogo kama kudhibiti hasira zako mwenyewe. Wengi huwa hatufikirii vitu kama hivyo, lakini ni muhimu sana na hakuna tunachoweza kufanya kwenye maisha yetu kama kitu kidogo namna hiyo kinatushinda.
Kama hatuwezi kudhibiti hasira zetu wenyewe, kama hatuwezi kuzuia hisia tulizonazo zisiingilie kile tunachofanya, ni vigumu sana kwetu kuweza kufanya chochote kikubwa kwenye maisha yetu.

Kuna vitu vingine vidogo sana kama nidhamu ya muda na nidhamu ya fedha. Kama huwezi kupanga kufanya kitu muda fulani na ukakifanya kweli, safari yako kwenye jambo lolote itakuwa ngumu. Kama huwezi kuwahi mahali, kama huwezi kufika ndani ya muda unaopaswa kufika mahali fulani, upo kwenye upande mgumu wa kufikia mafanikio yoyote unayofikiria.
Kuweza kukaa na fedha kidogo na ukaituliza ni kitu kingine kidogo ambacho ni muhimu sana kwa mafanikio yako. Kama ukiwa na fedha kidogo huwezi kutulia mpaka uitumie, jua pia ukiwa na nyingi, ndiyo mambo yatakuwa mabaya zaidi.
SOMA; UKURASA WA 697; Jua Udhaifu Wako Kifedha Na Udhibiti…
Kusema ukweli hasa kwenye mambo madogo ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio yako. Kama huwezi kusema ukweli hasa kwenye mambo madogo unajiweka kwenye wakati mgumu wa kufanikiwa.
Rafiki, ni vizuri sana kuwa na ndoto na mipango mikubwa kwenye maisha yako. Lakini kama vitu vidogo vidogo kama tulivyojadili hapa vinakushinda, ndoto kubwa ulizonazo ni za kujifurahisha tu, hutaweza kuzifikia. Anza kufanyia kazi mambo madogo madogo yanayokusumbua na utashangaa jinsi gani yale makubwa yatakwenda vizuri kabisa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,