Rafiki yangu mpendwa,

Jinsi wengine wanavyotuchukulia ina maana kubwa sana kwenye maisha yetu na mafanikio tunayoyatafuta kwenye maisha.

Chochote ambacho unakitaka kwenye maisha yako, utakipata  kutoka kwa wengine. Hivyo jinsi ambavyo wengine wanakuwa na sifa nzuri juu yako, ndivyo wanavyokuwa tayari zaidi kukupa kile unachotaka.

Mahusiano yetu na wengine ni eneo muhimu sana tunalopaswa kufanyia kazi kwenye safari yetu ya maisha ya mafanikio. Bila ya mahusiano haya, itakuwa vigumu kwetu kufanikiwa, na hata tukifanikiwa bila ya mahusiano haya, mafanikio hayo hayawezi kudumu kwa muda mrefu.

Tabia zetu wenyewe ndiyo kitu pekee ambacho tuna nguvu ya kuzibadili, sifa zetu kwa wengine ni vile wengine wanatuchukulia kulingana na tabia zetu.

Hivyo hatuwezi kuwaambia watu watuchukulieje, wala hatuwezi kuwalazimisha watuchukulie kwa sifa fulani. Ila sisi wenyewe tunaweza kujijengea tabia ambazo zitawafanya wengine wajenge sifa nzuri kwako.

Hivyo rafiki, kama watu wana sifa mbaya juu yako, jua ni kwa sababu ya tabia zako na siyo kingine. Na njia pekee ya kuwafanya watu hao wawe na sifa nzuri juu yako ni kubadili tabia zako.

Maisha Bora

Kwenye makala ya leo tunakwenda kujifunza tabia mbili za kujijengea ambazo zitakujengea sifa nzuri kwa wengine na kukuwezesha kufanikiwa sana.

Tabia ya kwanza; sema ukweli mara zote.

Hakuna uongo mdogo, hakuna uongo mweupe, uongo ni uongo na ukidanganya mara moja utaendelea kudanganya tena na tena na tena. Hivi ndivyo uongo unaofikiri ni mdogo unavyoweza kuharibu kabisa sifa yako mbele ya wengine.

Mara zote sema ukweli, hata kama siyo mzuri kusikia, lakini ukweli huwa haujifichi kwa muda mrefu. Ukweli ni mgumu na ukweli ni mkali, lakini ukiuficha au kuukwepa unajipa ahueni ya muda tu, baadaye ukweli utajulikana na utakuwa wazi.

Ukweli pekee ndiyo unaoweza kukupa sifa nzuri kwa wengine, siyo wote watakupenda kwa kusema ukweli, lakini nakuhakikishia, hakuna atakayekudharau kwa sababu unasema ukweli. Hata wanaokuchukia kwa kusema kwako ukweli, watakuheshimu, na watakuheshimu sana. Na popote wanapokuona watasema huyu mtu huwa anasema ukweli.

Kusema ukweli kunaweza kukunyima mazuri ambayo ungeweza kuyapata haraka, lakini kutakuwezesha kupata makubwa zaidi kwa baadaye.

Ukweli ndiyo utakuweka huru na ukweli ndiyo utakujengea sifa imara kwa wengine. Danganya mara moja na utadanganya tena na muda siyo mrefu unajikuta kwenye uongo mkubwa kiasi kwamba hujui hata unawezaje kuendeleza uongo huo.

Na mara zote uongo unapoanza kuanguka, huanguka na kila kitu kilichojengwa kwenye uongo huo.

SOMA; UKWELI KUHUSU AJIRA; Mambo Kumi(10) Ya Kweli Ambayo Waajiriwa Hawapendi Kuyasikia.

Tabia ya pili; kufanya.

Kila mtu anaweza kuongea na wengi sana wanaongea, wengi wanaahidi, wengi wanapanga na kusema watafanya makubwa. Lakini inapofika kwenye kufanya, ni wachache sana wanaokaa chini na kufanya. Na katika hao wachache wanaofanya kweli, wengi wanaishia njiani wanapokutana na vikwazo.

Hivyo katika wengi ambao wanatamani kufanya, na wachache wanaoanza kufanya ni wachache mno ambao wanazalisha matokeo kweli kwenye ufanyaji.

Hivyo ukiwa mtu wa kufanya, ukiwa mtu wa kutoa matokeo, watu watakuheshimu, na sifa yako kwa wengine itakuwa nzuri.

Kila mtu anapenda mtu anayefanya, mtu anayetoa matokeo. Hakuna anayependa wasemaji na watoaji wa sababu. Hivyo kama unataka sifa nzuri kwa wengine, kama unataka wengine wawe tayari kukupa unachotaka, kuwa mtu wa kufanya badala ya mtu wa kuahidi na kutoa sababu.

Nikukumbushe na kukujuza kama ulikuwa hujui, ya kwamba hakuna anayekulipa kwa kile unachojua, bali utalipwa kwa kile unachofanya. Matokeo unayozalisha ndiyo yatakayopelekea wewe kulipwa, kupata unachotaka kupata.

Ondoka kwenye kundi la wasemaji na nenda kwenye kundi la wafanyaji. Fanya, na fanya makubwa, chukua hatua kubwa, ambazo wengine hawathubutu hata kuzifikiria. Chukua hatua kubwa kiasi kwamba watu wanakuambia haiwezekani, kisha weka juhudi na upate matokeo, sifa zako zitakuwa maradufu zaidi.

Kama unataka watu wakujue, usipige kelele, ambacho ndiyo wengi wanafanya hivyo, bali kuwa mtu wa kuzalisha matokeo, na kumbuka matendo yanaongea kwa sauti kuliko maneno.

Mwisho, nikukumbushe kwamba huhitaji kutoa maelezo yoyote, bali unahitaji kufanya. Kama utafanikiwa hutakuwa na haja ya kujieleza, maana matokeo yataonesha yenyewe. Na kama utashindwa, huna hata haja ya kujieleza na tumia muda huo kwenye kufanya zaidi.

Sema ukweli mara zote na kuwa mtu wa kufanya, siyo wa kusema, tabia hizi mbili ukiziishi kwenye kila siku ya maisha yako, utajijengea sifa bora kwa wengine na zitakuwezesha kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha