Rafiki yangu,

Juma namba 15 la mwaka huu 2018 ndiyo linatupa mkono, juma linakwisha, ni imani yangu kwamba siku nyingi zijazo, ukiangalia nyuma, utaweza kuona ni kitu gani cha tofauti umefanya kwenye maisha yako kwenye juma hili la 15 la mwaka 2018.

Kama hakuna cha tofauti unachoweza kuona umefanya kwenye juma hili la 15, maana yake ulichofanya ni umelipoteza. Yaani kwa kuamua kabisa, umechukua siku saba, masaa 168 na kuamua kutupa hovyo tu, kitu ambacho siyo kizuri kama unataka maisha ya mafanikio.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano niliyojifunza na kukutana nayo kwenye juma zima. Mambo haya yanaweza kukusaidia kwenye juma unalomaliza na hata juma unalokwenda kuanza. Lengo ni kila juma liwe na kitu cha tofauti kwenye maisha yako, upange na kuchukua hatua kila juma ambazo zinakusogeza karibu zaidi na maisha ya mafanikio unayotaka kuishi.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Karibu kwenye tano za juma hili la 15, tujifunze na kuchukua hatua ili kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.

#1; KITABU NILICHOSOMA; NGUVU YA AKILI KWENYE KUPONYA MWILI.

Sehemu kubwa ya maradhi tunayopata, huwa yanasababishwa na jinsi tunavyochagua kuishi maisha yetu. Kwa dunia ya sasa, dunia ya kasi, dunia ya vitu vingi vya kufanya kuliko muda tulionao, kila mtu yupo kwenye mwendo. Hili linafanya wengi kuwa na msongo wa mawazo, na hili linapelekea mwili kuwa dhaifu na kuweza kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.

Mwandishi wa kitabu THE HEALING POWER OF MIND, Tulku Thondup anatuambia kwamba akili zetu zina uwezo wa kutibu kila aina ya maradhi ambayo miili yetu inapitia.

Tulku ambaye ni mbudha, anatuambia kwamba kwa asili, akili zetu ni safi, ni chanzo cha furaha na afya njema. Lakini tunapokutana na dunia, ikatujaza uchafu, ikafanya tuende kasi na kuweka furaha kwenye vitu vya nje badala ya kuanzia ndani, ndipo maisha yanapoanza kuwa magumu.

Suluhisho la yote, ambalo Tulku anatushirikisha ni kufanya tahajudi (meditation). Tulku anatuambia, iwapo mtu utatenga muda wa kufanya zoezi la tahajudi kila siku, basi utaweza kutuliza akili yako na kuondokana na msongo wa mawazo. Hilo litaimarisha mwili wako na kuweza kujikinga na magonjwa mbalimbali yanayoshambulia mwili.

Na siyo Tulku tu anayesema hili, bali tafiti za kisayansi na kiafya zinaonesha wale wanaofanya tahajudi kuwa na utulivu mkubwa wa akili na kuwa na afya imara.

Hivyo rafiki yangu, tenga muda wa kufanya tahajudi kila siku, anza na muda unaoweza kupata, iwe ni dakika tano, kumi au hata nusu saa. Weka nidhamu kwenye kufanya zoezi hili na ongeza muda kadiri unavyokwenda.

Kwa wale wasioelewa kabisa tahajudi inafanyikaje, kwa kifupi sana ni kwamba zoezi la tahajudi ni kutuliza mawazo yetu ambayo kwa asili yanarukaruka kama tumbili wanavyoruka kwenye miti. Hivyo ili kuyatuliza, unafanya zoezi rahisi la kuelekeza mawazo yako kwenye eneo moja na kuzuia yasirukeruke. Na sehemu rahisi ya kuelekeza mawazo yako ni kwenye pumzi zako.

Unachofanya, unachagua eneo ambalo ni tulivu, unakaa wima, kwa namna ambayo utakuwa umetulia, kisha pumua kwa kuhesabu pumzi zako. Hakikisha mawazo yako yote umeyaelekeza kwenye pumzi, unapovuta hewa ndani na kutoa nje. Unaweza kuhesabu mpaka kumi kisha kuanza tena. Wakati unafanya hivyo, utapata ushawishi wa kupeleka mawazo yako kwenye mambo mengine, kataa ushawishi huo.

Fanya zoezi hili kwa muda mrefu kadiri uwezavyo, na kadiri unavyoweka mawazo yako kwenye pumzi zako, ndivyo unavyozidi kuimarisha akili yako na kuituliza pia.

Maelezo haya ni kwa kuanza, ukitaka kupiga hatua zaidi kwenye tahajudi unahitaji kuendelea kujifunza zaidi na zaidi.

SOMA; MINDFULNESS; Jinsi Kuzurura Kwa Akili Zetu Kunavyotugharimu Kwenye Maisha Na Jinsi Ya Kuzituliza Akili Zetu.

#2 MAKALA YA WIKI; KWA NINI HUPASWI KULALAMIKIA CHOCHOTE.

Kama kuna mtu ulimwamini sana, ukampa nafasi, halafu mtu huyo akakutapeli, au kukusaliti, je si anastahili kulaumiwa na kulalamikiwa? Jibu ni ndiyo kama hutaki kujifunza na kuzuia hilo lisitokee tena kwenye maisha yako.

Kuna vitu ambavyo huwa tunajishawishi kwamba tumeonewa na tunastahili kuwalaumu wengine. Lakini mimi nimekuwa nakuambia kitu kimoja, usilaumu wala kumlalamikia yeyote yule kwa lolote lile, hata kama amefanya wewe ukiwa hujui.

Kwenye makala ya wiki hii nimekutajia maeneo matano ambayo wengi tumezoea kuyalalamikia ambayo hayapaswi kabisa kulalamikiwa. Soma makala hii kama hukupata nafasi ya kuisoma, yapo mengi ya kujifunza; Ninaposema Usilalamike Wala Kulaumu Yeyote, Namaanisha Hivi (Mifano Mitano Ya Maeneo Uliyozoea Kulalamika Ambayo Hayakusaidii Chochote). (https://amkamtanzania.com/2018/04/13/ninaposema-usilalamike-wala-kulaumu-yeyote-namaanisha-hivi-mifano-mitano-ya-maeneo-uliyozoea-kulalamika-ambayo-hayakusaidii-chochote/)

#3 NILICHOJIFUNZA; UNACHOJIAMBIA UNAPOWAKOSOA WENGINE.

Umewahi kuona kwamba hata ufanye nini watu huwa hawakosi cha kukosoa? Usipofanya kazi watu watakukosoa, ukifanya kazi kiasi watu watakukosoa na ukifanya kazi sana bado watu watakukosoa.

Kila mtu anaweza kukosoa, kila mtu anaweza kutoa ushauri ambao yeye anaamini ndiyo ushauri sahihi na kila mtu anapaswa kuufuata.

Lakini chukua muda wako na angalia watu kwenye kile wanachokosoa, utagundua hawana au hawawezi. Kwa mfano, anza kufanya kazi sana, halafu angalia watu gani watakaokuwa wanakukosoa kwa ufanyaji wako kazi, wale ambao hawafanyi kazi sana.

Ongea kuhusu fedha sana na utaona wale wasio na fedha wakikukosoa kwamba unaongelea fedha sana.

Na lile neno maarufu kwamba FEDHA HAINUNUI FURAHA, unajua ni watu gani huwa wanalitumia sana? Wale wasio na fedha. Hutakutana na mtu mwenye fedha kweli halafu akaanza kukuambia kwamba FEDHA HAINUNUI FURAHA.

Hivyo rafiki, usiumie sana pale watu wanapokukosoa wakati unafanya kile ambacho ni sahihi na kinaleta matokeo kwako, wanakukosoa kwa sababu wao hawawezi kufanya unachofanya wewe.

Na upande wa pili wa shilingi, kama unakosoa wengine, maana yake unadhihirisha kwamba kile wanachofanya wewe huwezi kufanya.

Maana kama ungekuwa unaweza ungefanya, na usingepata muda wa kuanza kukosoa. Na kama kweli kuna kitu unafanya kwenye maisha yako, unapata wapi muda wa kuanza kufuatilia kila ambacho kila mtu anafanya na kuweza kukosoa?

Kuwa bize na kufanya yale yako, kama wazungu wanavyosema MIND YOUR OWN BUSINESS na uache wengine wafanye yao.

SOMA; HIKI NDICHO KINAFANYA MAISHA YANAKUWA MAGUMU KWAKO

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KAMA UNATAKA USHAURI KUTOKA KWANGU, UNAUPATA HAPA.

Kadiri huduma yangu inavyozidi kukua, ndivyo inavyokuwa vigumu kwangu kuwasiliana na kila mtu kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja. Zamani nilikuwa naweza kupokea kila simu, kujibu kila ujumbe na hata kumjibu kila anayeniandikia, lakini kadiri huduma inavyokuwa inakuwa vigumu kuwasiliana na kila mmoja anayehitaji kupata kitu kutoka kwangu. Hivyo nimekuwa nashauri mtu yeyote anayeniandikia akitaka nimshauri kwenye vitu fulani, hasa biashara na fedha, kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ambapo kwanza atapata mafunzo mazuri ya kila siku, na inakuwa rahisi kuwasiliana.

Hivyo kama umekuwa unajaribu kunifikia kwa njia mbalimbali hunipati, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, utakuwa karibu zaidi na mimi, utapata ushauri mwingi kupitia yale wengine wanayouliza na hata kujibu, na hata zile changamoto unazopitia ambazo utawauliza wengine.

KISIMA CHA MAARIFA ni jamii ya kipekee na ya tofauti kabisa ambayo tunaitengeneza, ambayo kuwa ndani yake ni fursa ya kipekee kabisa ya kuwa na maisha bora. Kupitia KISIMA CHA MAARIFA utajifunza, utajitathmini na utayatawala maisha yako badala ya maisha kukutawala.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kama bado hujajiunga, nitumie ujumbe sasa ka njia ya wasap namba 0717396253 na nitakupa maelekezo ya kujiunga.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KINACHOKUZUIA KUFANIKIWA.

“People become successful the minute they decide to”. – Harvey Mackay

Kama mpaka sasa bado hujafanikiwa na wala huoni dalili za kufanikiwa kwenye maisha yako, basi tatizo ni moja, HUJAAMUA KUFANIKIWA.

Unaweza kuona hicho ni kitu rahisi sana kusema, lakini nakuambia MAAMUZI ndiyo kitu kinachokuzuia. Na ninaposema maamuzi simaanishi zile ahadi unajipa kila siku na baada ya muda unasahau na kurudi kwenye maisha uliyozoea.

Ninaposema MAAMUZI, namaanisha kwamba unakata mzizi wa fitna, unasema hivi ndivyo nitafanya na unafanya kweli, ije mvua lije jua wewe hujui kitu kingine bali kufanya. Pale watu wanapokuambia huwezi au haiwezekani huelewi hata wanaongelea nini, unaishia kuwashangaa.

Ni wachache sana wanafika kwenye hatua hiyo ya maamuzi, ndiyo maana wachache sana wanafanikiwa.

Wengi, asilimia karibu 99, leo wakisoma ufugaji wa kware ni fursa, wanaenda kujenga banda na kuanza kufuga kware, kesho wakisoma ufugaji wa sungura ni fursa, wanabomoa mabanda ya kware na kujenga ya sungura. Utawakuta kila mwaka wanazunguka na kila aina ya fursa, mwishowe wanachoka na hakuna wanachopata.

Kama umesikia ufugaji wa kware ni fursa, unafanya utafiri kama kweli ni fursa, na ukiona ni fursa kweli, basi unaingia kufuga, na hapo hutaacha mpaka upate yale mafanikio uliyoyaona wakati unapanga kuanza. Iwe itakuchukua mwaka 1, miaka 10 au hata miaka 50, wewe utafanya, kwa sababu umeamua.

Lakini kama kila siku utakuwa unahangaika na kila kitu kipya, leo CRYPTOCURRENCY, kesho FOREX, keshokutwa hatujui hata ni nini, hutaweza kufanikiwa, niamini kwenye hilo.

Rafiki, tunakwenda kuanza juma namba 16, pangilia juma hilo kabla ya kulianza, fanya maamuzi ya nini utafanya na fanya kile tu ulichopanga kufanya. Usikubali kuyumbishwa na vitu vipya ambavyo watu wanahangaika navyo, fanya utafiti wako, jua kila unachopaswa kujua kisha fanya maamuzi na ishi maamuzi hayo. Kwa kifupi MAFANIKIO NI KUFANYA MAAMUZI NA KUISHI MAAMUZI HAYO.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji