Rafiki yangu mpendwa,

Huwa tunakosea sana tunaposema tunatafuta mafanikio.

Hii ni kwa sababu mafanikio hayawezi kutafutwa, kwa sababu kinachotafutwa ni kilichojificha au kigumu kupatikana. Lakini mafanikio hayajajificha, wala siyo magumu kupatikana.

Na kama utasema unakimbiza mafanikio, basi utayakimbiza maisha yako yote na hutayapata.

Mafanikio hayatafutwi, bali yanavutiwa. Unapata mafanikio kama matokeo ya aina ya mtu unayekuwa. Ikiwa na maana kwamba unafanikiwa pale unapokuwa mtu wa aina fulani ambaye mafanikio yanaenda kwake.

Tunaweza kusema kwamba, mafanikio yapo muda wote, ila yanachagua yaende kwa mtu wa aina gani.

Hivyo kama unataka kufanikiwa zaidi, lazima ujue aina ya mafanikio unayotaka yanaenda kwa mtu wa aina gani, mtu mwenye sifa gani. Ukishajua unakuwa mtu wa aina hiyo na unaweza kufanikiwa zaidi.

MIMI NI MSHINDI

Kitu kingine kizuri kuhusu mafanikio ni kwamba hakuna darasa ambalo unapaswa kusoma na kufaulu ili uweze kufanikiwa. Badala yake unapaswa kuwaangalia wale waliofanikiwa ni watu wa aina gani, na wewe unakuwa mtu wa aina hiyo na utayavutia sana mafanikio kwako.

Kwenye makala ya leo, nakwenda kukushirikisha sifa saba ambazo zinayakaribisha mafanikio kwa mtu. Ukiweza kujijengea sifa hizi saba, zikawa sehemu ya maisha yako, mafanikio yatakuja kwako bila ya shida yoyote.

Sifa ya kwanza; maandalizi bora.

Mafanikio yanaenda kwa wale watu ambao wana maandalizi bora. watu ambao wanajua ni nini wanataka na wanapaswa kufanya nini ili kupata kile ambacho wanakitaka. Watu ambao wanajifunza kila siku ili kupiga hatua zaidi. Watu ambao wanajua siyo kila wakati watapata kile wanachotaka, hivyo wamejiandaa kwa matokeo ya tofauti na wanavyotegemea.

Maandalizi bora ni tabia unayoweza kujijengea kwa kuwa mfuatiliaji wa karibu wa chochote unachofanya, na kuwa tayari kwa matokeo yoyote utakayoyapata na usikate tamaa.

SOMA; Najiwasha Moto, Njoo Unione Nikiungua (Azimio La Miaka Kumi Ijayo Ya Maisha Yangu).

Sifa ya pili; kujiamini wewe mwenyewe.

Hakuna mtu aliyefanikiwa ambaye hajiamini yeye mwenyewe. Kila aliyefanikiwa sana anajiamini yeye mwenyewe, hata pale jamii nzima ilipowaambia kwamba hawawezi au haiwezekani. Ili uyavutie mafanikio makubwa kwako, jiamini sana wewe mwenyewe. Amini kwenye uwezo wako wa kufanya makubwa, amini kwenye kuwezekana kwa kile unachotaka na amini kwenye matokeo ya kile unachofanyia kazi.

Jijengee tabia ya kujiamini wewe mwenyewe kwa kujua kwamba wewe ni wa tofauti, wa kipekee na unaweza kufanya makubwa sana. Yale watu wanasema hayawezekani ni kwa sababu hakuna ambaye alishawahi kuyafanya, hivyo kama wewe utajitoa kuyafanya, kwa sababu una uwezo mkubwa, yatawezekana.

Sifa ya tatu; ushirikiano sahihi.

Hakuna mtu ambaye ameweza kufanikiwa yeye mwenyewe. Kwenye mafanikio hakuna jeshi la mtu mmoja. Na dhana kwamba mtu ni tajiri wa kujitengeneza yeye mwenyewe, haipo, ni kutaka tu kujisifia. Kila kitu unachokitaka kwenye maisha yako unakipata kutoka kwa wengine. Hivyo kwenye mafanikio, ili uvutie mafanikio makubwa, lazima ushirikiane na watu sahihi wanaoendana na mafanikio hayo. Lazima wawe watu ambao wanajua wapi wanakwenda, wanajiamini na siyo watu wa kukata tamaa. Shirikiana na watu wanaokata tamaa haraka na utaona jinsi safari itakavyokuwa ngumu.

Tengeneza ushirikiano sahihi na wale watu ambao wanajua nini wanataka, wanataka makubwa na wapo tayari kulipa gharama kuyapata. Wasiwe watu wa kukata tamaa na msamiati HAIWEZEKANI usiwe kwenye kamusi zao. Katika kila mtu unayeshirikiana naye, kumbuka matokeo yako ni wastani wa matokeo ya watu watano wanaokuzunguka. Chagua kwa umakini ili yeyote asikurudishe nyuma.

Sifa ya nne; kujifunza wewe mwenyewe.

Kuna vitu ambavyo kila mtu anafundishwa, kwenye jamii, kwenye mfumo wa elimu na hata maisha kwa ujumla. Hivi ni vitu vya kawaida, ambavyo ukivifuata kama vilivyo, utavutia maisha ya kawaida tu. Hutaweza kupata mafanikio makubwa kwa kutumia vile ambavyo umefundishwa na wengine. Wale waliofanikiwa zaidi ni watu waliotumia muda wao kujifunza wao wenyewe, kwenye yale maeneo ambayo ni muhimu zaidi kwao. Wakajitoa kubobea kwenye kile wanachotaka, wakajua vitu ambavyo wengine wote hawajui na hata kuvikubali hata kama vinaenda kinyume na namna walivyofundishwa awali. Ni ujuzi wa aina hii ndiyo umewawezesha wengi kuvutia mafanikio makubwa kwao.

Jijengee sifa ya kujifunza wewe mwenyewe kwa kuchagua yale maeneo ambayo unayapenda zaidi, kisha kujua kila kitu kinachohusiana na maeneo hayo. Jifunze sana na asiwepo yeyote anayejua zaidi yako. Jifunze na kuwa tayari kupokea mambo yanayoenda tofauti na ulivyozoea au ulivyofundishwa awali. Mafanikio makubwa yanafuata maarifa ya kipekee ambayo wengi hawana.

Sifa ya tano; kukubali majukumu.

Kuna watu wa aina mbili hapa duniani, wapo watu ambao wanayakubali majukumu yao na kuchukua hatua. Na wapo watu ambao wanayakataa kabisa majukumu yao na kutafuta sababu kwa nini hawawezi kuchukua hatua. Mafanikio hayajawahi kwenda kwa mtu yeyote ambaye siyo wa kukubali majukumu. Mafanikio yanawapenda wale wanaokubali majukumu na kuchukua hatua na siyo wale wa kutafuta sababu kila mara. Huwezi kukuta mtu aliyefanikiwa akikupa sababu kwa nini hajafanya kitu fulani au kwa nini hajapata kitu fulani, utamkuta tayari anacho, au anakifanyia kazi.

Kuwa mtu wa kukubali majukumu yako na kuchukua hatua. Kila unapotamani kutoa sababu kwenye jambo lolote lile, nyamaza na rudi kuchukua hatua. Sababu zako hazitamsaidia yeyote na zaidi zitayafukuza kabisa mafanikio yako. Kubali majukumu na chukua hatua.

SOMA; Ninaposema Usilalamike Wala Kulaumu Yeyote, Namaanisha Hivi (Mifano Mitano Ya Maeneo Uliyozoea Kulalamika Ambayo Hayakusaidii Chochote).

Sifa ya sita; kuziona fursa na kuchukua hatua.

Fursa huwa zipo kila mahali, wala siyo kitu cha kutafuta kama wengi wanavyoambiana. Na wala hakuna fursa mpya, fursa zimekuwepo wakati wote, upya wa fursa ni upya wa maarifa ambayo mtu unakuwa umeyapata. Macho hayawezi kuona kitu ambacho akili haijui. Hivyo unavyojifunza zaidi ndivyo unavyoziona fursa zaidi. Watu waliofanikiwa sana wanaonekana ni watu ambao wanaziona fursa zaidi kuliko wengine. Na hili ni kweli, kwa sababu wanajua wanachofanya kuliko wengine. Ila kinachowatofautisha zaidi ni wakiona fursa wanachukua hatua.

Kadiri unavyoendelea kujifunza kuhusu kile unachotaka, utazidi kuona fursa zaidi, chagua ni fursa zipi unazoweza kuweka juhudi na chukua hatua mara moja. Ukishaona fursa inakufaa, usipoteze tena muda wako, chukua hatua. Hivi ndivyo utakavyoyavutia mafanikio kwako.

Sifa ya saba; kuchukua hatari.

Hakuna mafanikio ambayo yamewahi kuwa salama, hakuna na hayatakuja kuwepo. Mafanikio kwa wote yamekuwa ni matokeo ya kuchukua hatua ambazo ni hatari, hatua ambazo mtu angeweza kushindwa na kupotea kabisa. Watu wote waliofanikiwa ni watu ambao walikuwa tayari kuchukua hatua ambazo zilionekana ni hatari kwa wengi. Walichukua hatua ambazo kila aliyewazunguka aliwaambia hazitafanya kazi, ni kujitesa na watashindwa. Mafanikio yana tabia ya kwenda kwa wale ambao wako tayari kuchukua hatua za hatari.

Ukishajua nini unataka hasa kwenye maisha yako, kuwa tayari kuchukua hatua hatari ili kukipata. Kuna wakati utajikuta unafanya mambo ambayo hata wewe mwenyewe huna uhakika nayo, lakini kwa sababu unajiamini, unafanya, na yanakuletea mafanikio makubwa. Kama unataka kuyavutia mafanikio, ondoa dhana ya hatari na salama kwenye maisha yako na kuwa tayari kufanya kila kinachopaswa kufanywa ili kupata kile unachotaka.

Mafanikio hayajawahi kuwa magumu, ila watu ndiyo wamekuwa wanakazana kuwa wagumu. Hawataki kujijengea tabia zinazovutia mafanikio, lakini wanaishi maisha yao yote wakikimbiza mafanikio, kitu ambacho hawakipati. Jijengee tabia hizi saba ulizojifunza hapa, zifanye kuwa sehemu ya maisha yako na utaanza kuona matokeo makubwa sana kwenye maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji