Rafiki yangu mpendwa,
Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Tunaweka mipango fulani lakini mambo ambayo hatukuwa tumeyategemea yanatokea. Ni katika nyakati za aina hiyo wengi hukata tamaa na kuona hawawezi tena kupata kile wanachotaka.
Na hapo ndipo wengi wanapokosea, kwa sababu hakuna changamoto ambayo ni ngumu na haiwezekani kabisa. Kila changamoto tunayokutana nayo kwenye maisha yetu ni darasa la mafanikio zaidi. Tukiweza kuivuka tunakuwa tumepiga hatua zaidi kuelekea kwenye mafanikio tunayotaka.
Karibu kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto, ambapo tunakwenda kumshauri mwenzetu kuhusu hatua za kuchukua pale unapohamishwa kazi na kupelekwa kwenye eneo ambalo wengi wanalisema kwa sifa mbaya.
Kabla hatujaangalia hatua hizo za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu.
“Kocha nifanyeje mimi nimehamishwa kazi toka Kilimanjaro kwenda mkoa ambapo unasifika kwa kuongoza kwa maambukizi ya UKIMWI na kila mtu hakuna anayeniambia mradi wa kwenda kufanya huko ni kuniambia hali mbaya huko mimi ninataka nikatengeneze mfereji wa kipato huko niendako na mpenzi wangu atakuwa mbali kila mtu ananiambia huko UKIMWI upo nenda na mke na sijaoa ila nina mchumba!” – Hendry S. L.
Moja ya changamoto za ajira ni kutokuwa na maamuzi ya mwisho kwenye maisha yako. Hivyo unajikuta kwenye mabadiliko ambayo hayaendani na mipango uliyokuwa nayo awali. Lakini pia mabadiliko ya aina hii yanakufundisha vitu vingi. Kwa sababu huenda unakuwa umezoea eneo moja na kuona maisha ndiyo hayo unayo, lakini unapopelekwa eneo jingine, unakwenda kuona kumbe kuna maisha ya tofauti na yale uliyozoea. Wapo watu wengi sana ambao wamefanikiwa baada ya kuondoka kwenye yale maeneo ambayo walikuwa wameyazoea, hasa kama ni maeneo waliyozaliwa na kukulia maisha yao yote.
Kuhusu kuhamishiwa kazi eneo ambalo lina changamoto fulani, kama hii ya maambukizi makubwa ya ukimwi; kwanza kabisa acha kuwasikiliza hao wanaokupa habari mbaya pekee. Ni kweli eneo linaweza kuwa na maambukizi makubwa ya ugonjwa fulani, lakini ninaweza kukuhakikishia kwamba siyo kila mtu kwenye eneo hilo atakuwa na ugonjwa huo. Pili unajua maambukizi ya ugonjwa huo, ambayo yapo ndani ya uwezo wako wa kujidhibiti, hivyo hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Tatu kinachokupeleka kule ni kazi, kama utakwenda kufanya kazi kweli, na kuacha kupoteza muda au kuwasikiliza wanaokupa habari za kukutishia, wala hutapata muda wa kutafuta na kuupata ugonjwa huo.
Kuhusu kwenda kutengeneza mifereji mpya ya kipato, hilo ni muhimu sana, na unapofika, yasome mazingira, angalia uhitaji wa watu na angalia taaluma na uzoefu ulionao kisha ona ni kwa namna gani unaweza kuwasaidia wale wenye uhitaji. Jitoe sana kwenye kufanya kazi na angalia kila namna ambayo unaweza kutoa thamani zaidi kwa wale wanaokuzunguka. Utakapofika eneo lako jipya la kazi utakutana na wazoefu ambao watakuambia nini huwezi kufanya, wasikilize lakini usifuate mengi wanayokuambia. Kwa sababu wengi huwa ni waoga waliozoea na watapenda na wewe uwe mwoga pia ili muweze kwenda sambamba. Wewe angalia namna unaweza kuongeza thamani zaidi.
Kuhusu kuambiwa uende na mke ili usipate ukimwi, huo ni ushauri ninaoweza kusema ni wa kijinga sana unapewa. Kupata au kutokupata ukimwi ni tabia na siyo kuwa una mke au huna. Kuna watu wapo kwenye ndoa na wanapata ukimwi, na kuna watu hawapo kwenye ndoa na hawana ukimwi. Wewe kazana kujenga tabia njema kwako binafsi, kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana. Kama tayari una mchumba ambaye mna mipango ya kuona, lakini siyo sasa, huna haja ya kuharakisha kwa sababu watu wanakuambia kuoa ndiyo kinga ya ukimwi. Endesheni mahusiano yenu vizuri na kila mmoja awe na nidhamu ya hali ya juu. Na kama utafanya kazi kweli, hutapata muda wa kwenda kutafuta ukimwi.
Kwa mfano, watu wengi wanafanya kazi masaa 8 mpaka 10 kwa siku, wanakuwa na zaidi ya masaa nane ya kupoteza. Haya masaa nane ndiyo wanaenda kukaa kwenye vijiwe, kukaa maeneo ya starehe ambapo wanaanza kujazana ujinga na hatimaye kutengeneza mahusiano ambayo yanawaletea magonjwa mbalimbali. Sasa kama wewe utaamua kufanya kazi masaa 16 kwa siku, na ukabaki na masaa mawili tu ya kufanya vitu vingine, utajikuta huna hata muda wa kufikiria ujinga.
Wao wanakuambia kinga ya ukimwi ni kuoa, mimi nakuambia kinga ya ukimwi ni kufanya kazi. Fanya kazi hasa, yaani fanya kazi mara mbili zaidi ya wengine wanavyofanya. Kazi itakuchosha na itachukua muda wako na hutapata muda wa kufikiria au kupanga ujinga mwingine.
Mwisho kabisa nikuambie hili, acha kuwasikiliza wale wanaokupa habari mbaya, usiende eneo lako jipya la kazi ukiwa na mtazamo hasi na eneo hilo. Nenda ukiwa na hamasa ya kufanya kazi, nenda ukiwa na hamasa ya kuongeza thamani zaidi. Na nenda ukiwa tayari kuulinda muda wako na kuuweka kwenye kazi tu. Na jiambie kuanzia sasa kwamba wewe ndiyo kiongozi mkuu wa maisha yako, wewe ndiye utakayefanya maamuzi yote muhimu ya maisha yako, na hata kama jamii nzima itachagua kuangamia, wewe utasimamia misingi yako na hutaangamia.
Nikutakie kila la kheri kwenye eneo lako jipya la kazi, sasa una uhuru mkubwa wa kwenda kuanza maisha mapya, na kuondokana na mazoea fulani ambayo ulikuwa umeshayajenga kwenye eneo la zamani, ambayo hukuweza kuyavunja. Sasa nenda katengeneze mazoea mapya, mazoea ya maisha ya mafanikio na kwa hakika utapiga hatua kubwa.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog