Habari za siku mpenzi msomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ni matumaini yangu ya kuwa umzima na unaendelea na jukumu la kuboresha maisha yako kwa kujifunza hapa, karibu sana. Leo katika makala hii ya leo tutaangalia ni kwa nini malengo mengi huwa hayafakiwi pamoja na kuwa huna tuna mipango na mikakati mizuri ya kutufikisha kule tunakotaka kufika kimaisha.
 

Mara nyingi huwa kuna sababu nyingi, ambazo hupelekea malengo mengi kutokutumia katika maisha yetu. Kwa bahati mbaya sababu hizi huwa hazijulikani na wengi hali ambayo husababisha wengi kujilaumu na kujiona kama vile wana mkosi au laana. Kwa kuzibaini sababu hizi na kuziepuka, hiyo itakusadia wewe kufikia malengo yako kwa sehemu kubwa. Je, ni sababu zipi zinazosababisha usifikie malengo yako?
Hizi Ndizo Sababu 4 Zinazosababisha Usifikie Malengo Yako.
1. Malengo yanapishana na imani.
Kuna wakati tunakuwa na malengo,lakini inakuwa ni vigumu kuyafikia kwa sababu yanakuwa yanapishana na imani zetu potofu. Kuna watu ambao wanapenda kuwa na fedha nyingi, ingawa ndani kabisa ya mawazo yao ya kina walilishwa imani  kuwa fedha ni ibilisi, fedha zina mushkeli zikiwa nyingi na mengine ya aina hiyo kuhusu kipato.
Mtu kama huyu anaweza asing’amue kwamba hivyo ndivyo anavyofikiri kwa sababu imani hizo ziko kwenye mawazo yake ya kina. Atahangaika kutafuta fedha, lakini itakuwa vigumu sana kuzipata kwa sababu lengo lake hilo linapishana na imani zake, ambazo ndizo yeye mwenyewe . 
Wakati mwingine mtu utakuta anatafuta mafanikio, lakini ndani kabisa ya mawazo yake kuna hofu ya kulogwa. Pengine mazingira aliyokulia yamemfundisha kwamba, akipata mafanikio makubwa ni lazima atalogwa. Bila kujua, atajikuta akipata mafanikio madogo sana kwa sababu tayari imani yake imemfunga kupata mafanikio makubwa.
Lakini siyo suala la imani tu, bali kuna wakati malengo yetu yanaweza yakawa yanasigishana yenyewe kwa yenyewe. Kijana anakuwa na lengo la kucheza sana mpira hadi awe mchezaji wa kimataifa, lakini wakati huohuo anataka kuwa msomi mkubwa sana na mgunduzi. Muda wa kucheza mpira unaweza ukawa unaingiliana na ule wa masomo au wa masomo kuingiliana na ule wa mpira. Kama hilo litatokea na haliwezi kufanyiwa kabisa ufumbuzi, kuna uwezekano wa malengo yote mawili kutofikiwa, kila moja litaliuwa lingine.
Imani, mila na hata aina ya malengo yetu(kama ni zaidi ya moja) ni lazima vikaguliwe vema. Je imani na mila na desturi zetu hazina mchango kwenye kutufanya tukwame kabisa kusogea? Je, hatuna malengo ambayo yanashindana yenyewe kwa yenyewe?
 
2. Kuvunjwa moyo na waliokata tamaa.
Kuna wakati tunaambiwa na wenzetu au jamaa zetu kwamba malengo yetu fulani ni upuuzi au hayawezi kufikiwa. Kuna wakati tunachekwa au kuonekana kama tuliochanganyikiwa kwa sababu ya malengo yetu fulani. Kama hatujiamini kiasi cha kutosha, ni rahisi sana kwetu kuwaamini watu hao ambao kwa kawaida wengi wamekata tamaa au wana kijicho.
Kwa hiyo, tukiwa katika kujaribu kufikia malengo fulani katika maisha ni lazima tutarajie kuvunjwa nguvu kwa maneno ya kukatisha tamaa. Kama kweli tumeamua kufanikiwa katika jambo fulani, hatupaswi kujali kuhusu maneno hayo, bali kusonga mbele kwa nguvu zaidi. Hii haina maana kwamba tusisikilize ushauri, hapana. Tunapaswa sana kusikiliza ushauri wa wengine, lakini tupime kati ya ushauri na uvunjaji moyo.
Tukumbuke tu kwamba, sisi ndio tunaojua hasa ni kwa nini tumeamua kuingia kwenye kufanya jambo fulani. Ni Wengine mara nyingi watajua kwa juujuu tu, undani tutakuwa nao sisi. Hivyo sisi ndiyo ambao tutatakiwa kusimamia kile tulichoamua.
Ndiyo maana tunashauriwa kutomwambia kila mtu kuhusu malengo yetu. Kama ni ushauri ni vizuri tukaomba kwa mtu au watu ambao tunawaamini, watu ambao siku zote wanayatazama maisha kwa matumaini na ushindi. Tukiwakabili waliokata tamaa na kutarajia kupata ushauri, tutapata maudhi badala yake.
3. Kutilia mashaka uwezo wako.
Kama unataka kufikia mafanikio makubwa unayoyataka, kitu pekee ambacho unatakiwa kukiogopa na kukiacha kabisa kama itawezekana mara moja ni kujitilia mashaka wewe mwenyewe. Nijuavyo mimi ni kwamba, kwa kadri unavyojitilia shaka wewe mwenyewe kuhusu uwezo wako, njia ya kufika mbali inakuwa inajifunga yenyewe bila hata ya wewe kujua hilo.
Ni rahisi kuweza kujitilia mashaka na kuambiwa na wengine kwamba wana wasiwasi kuwa hatuwezi au tunachotaka kukifanya ni kikubwa sana au siyo saizi yetu au vizingiti vingine. Inawezekana watu hawa wanatuambia wakiwa wanaamini kwamba wanatusaidia, siyo kwa chuki, kwa sababu wenyewe ni watu wasiojiamini.
Kama ungekuwa ni mtu wa kufanya uchunguzi hata kidogo ungegundua kitu hiki, muda ambao mtu anautumia katika kutilia mashaka uwezo wake katika kufanya jambo, ni muda ambao angeweza kuutumia katika kujipanga upya, kujiandaa na kutenda tena. Lakini kama nilivyobainisha mara nyingi hadi sasa, ni kwamba tunapotilia mashaka uwezo wetu, itakuwa ni vigumu kwetu kufanya jambo na likawa kamili. Tutajikuta tunafanya makosa ya wazi kwa sababu hicho ndicho tulichotarajia.
4. Kushindwa kukubali vizingiti.
Haina maana kwamba tukiwa na malengo hatutakumbana na vizingiti au changamoto nyingi, hapana. Hata kama malengo yetu ni mazuri kwa kiasi gani, vizingiti ni jambo la kawaida na pengine ni lazima. Kama tutaelewa jambo hili na kuwa watu ambao hatutarudi nyuma kirahisi pale tutakapopambana na vizuizi ni lazima tutafanikiwa.
Kwa baadhi ya watu, vizuizi au matatizo katika shughuli au mipango yao huvichukulia kama laana, kama dalili ya kutofahahamu, kama dalili ya kushindwa, jambo ambalo huwavunja nguvu ambapo huacha shughuli hizo au kuzifanya kwa ‘nifanyaje’. Inapofika mahali pa kufanyia ‘nifanyaje’ ni wazi tunakuwa kama tumeshindwa tayari.
Siri ya kufanikiwa katika jambo lolote ni mtu kuwa king’ang’anizi. Kuna watu ambao hata siku moja hawako tayari kuweka ‘silaha’ chini hadi pale wanapofikia kwenye kuanguka na kufa, yaani shughuli sasa imethibitika kwa asilimia mia moja kwamba haiwezekani kabisa. Wengine kuingia kwenye tatizo mara moja tu, kwao ina maana ya kushindwa.
Ukweli ni kwamba, hata kama tumeshindwa kabisa katika kufikia malengo, hatupaswi kuamini kwamba huko kushindwa. Ni lazima tutumie kushindwa  huko kwa ajili ya kujifunza mambo muhimu na ya msingi ambayo hutusaidia kusimama baadaye.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
TUNAKUTAKIA KILA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.
TUPO PAMOJA,
IMANI NGWANGWALU,